JUMA LA NNE
Picha Thabiti—Kuwa Katika Urari wa Maisha
Mwongozo: Mifano ya Uhuru wa Kiroho

Juma hili tunasonga mbele kutoka katika utoaji shukrani na sifa kwa Mungu; kutoka katika mtazamo wa picha kubwa ya mpangilio wa viumbe vya Mungu — kwenda kuiishi picha hiyo thabiti ya uumbaji wa Mungu.  Kuiishi picha hiyo kubwa ipasavyo ni kukubali nafasi yetu katika uumbaji wa Mungu — ni kuwa katika urari wa maisha.

Katika juma lote hili, tuna shauku ya kuvutiwa na watu ambao wanaonekana kuwa katika hali ya kuikubali sababu ya kuumbwa kweo na hivyo basi kuvitumia viumbe vingine vyote katika hali huria inayotokana na kuikubali nafasi yao baina ya viumbe vya Mungu.

Mt. Inyasi wa Loyola anaweka hili katika maneno rahisi:

Sharti tutumie zawadi ya viumbe vya Mungu pale ambapo vinatuwezesha kuitekeleza nia ya kuumbwa kwetu, na sharti  tuviweke pembeni vile ambavyo havitusaidii kuitekeleza nia hiyo au vinakuwa kikwazo katika kuiishi sababu ya kuumbwa kwetu.

Ili kufanya hivyo, sharti tujiweke katika hali ya huria, ya kutojifungamanisha na chochote, kiasi kwamba hatupendelei afya kuliko maradhi, utajiri kuliko ufukara, heshima kuliko dharau, maisha marefu kuliko maisha mafupi; Na wala hatupendelei chochote kile kwa jinsi kilivyo, ila tu iwapo kinatusaidia kuitekeleza sababu ya kuumbwa kwetu.

Tunaweza kuona wazi ni kiasi gani tunakuwa katika hasara pale tunapojifungamanisha na viumbe vingine na kukosa urari wa maisha—hatuwi huru katika kuchagua jinsi ya kutumia vitu vilivyoumbwa na Mungu.  Pale ambapo matakwa na uchaguzi wangu vinanivuta kuwa na msimamo wa kusema “nataka afya yangu; nataka mafanikio; nataka kujitunza mwenyewe; sharti nihehimiwe na kusikilizwa,’’ hapo ni wazi kuwa sipo katika urari wa maisha bali nimeegemea upande mmoja, upande wa nafsi yangu tu.

Hata hivyo tunavutiwa tunapomwona mtu  akiwa wazi na huru katika kupenda wengine, kujitolea binafsi, kuishi vema na wengine nk.  Mtu huyo bila shaka kafahamu kilicho sahihi hasa.

Juma hili na liwe la kutaja na kuvutiwa na watu ambao wanaonekana kuwa mfano mzuri wa wa kuwa huru.  Ukitaka rejea kitabu chako cha picha ulichotumia katika majuma yaliyopita, labda pia unaweza kupata picha za watu hawa.  Kila siku katika shughuli zetu wiki hii,  tunaweza kujiweka katika utambuzi wa jinsi watu wanavyoishi wakimsifu, wakimtukuza na kumtumikia Mungu, wengine kwa ushujaa thabiti na wengine labda katika hali ya unyenyekevu, bali wengine katika hali ya kawaida tu.  Ni watu gani wanaotuonyesha njia ya kufahamu na kutenda kilicho sahihi hasa?


Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili

Ni watu gani wanaotuonyesha njia sahihi?

Njia nzuri ya kutuwezesha kuanza juma hili vema ni kuorodhesha katika karatasi majina ya watu wanaokuvutia maishani.  Anza na watu usiowajua sana, kama vile wale uliosoma historia au mawazo yao — labda Mtakatifu Inyasi, au Mtakatifu Fransisi, au labda Mtakatifu Teresia wa Avila; au Mama Teresa au hata Nelson Mandela.  Wanaweza kuwa watu ambao katika wakati fulani wa maisha yako walikuvutia sana: pengine mtu aliyekuwa na bidii katika kufanya kazi au kuitunza familia yake; au tajiri ambaye kiwanda chake kiliteketea kwa moto lakini aliendelea kuwalipa wafanyakazi mshahara ingawaje hawakuwa wakifanya kazi hadi alipokijenga kiwanda upya.  Baada ya hapo ni vema yakifuata majina ya watu unaowajua binafsi ambao wanakuvutia matika maisha — anaweza kuwa ndungu aliyeishi maisha ya uadilifu bila kutetereka katika hali ya ugumu wa maisha iliyomkabili au pia anaweza kuwa padre au mchungaji anavutia katika kuhubiri na kuishi anayohubiri.

Baada ya kumaliza kutengeneza orodha hii, tunaweza kulitumia juma hili katika kutafakari juu ya sifa za kila mmoja wao ambazo zinatuvutia.  Ni vipi maisha yao yalibaki katika urari? Walikuwa huru katika jambo gani?   Walikuwa huru kutenda jambo gani? Walikuwa huru kwa ajili ya jambo gani — ni yapi waliyachangua au wanayachagua na kuyapendelea?

Msichana katika picha ya wiki hii alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu kimoja huko Marekani.  Alikuwa alijitolea wakati wa likizo kufanya kazi katika kiliniki ya muda mfupi katika kijiji kimoja duni huko Amerika Kusini.  Tazama uso wake—unadhani anahisi nini moyoni?  Alihitaji uhuru kidogo tu kwenda kujitolea katika nchi nyingine, ila tunaweza kuona wazi kuwa katika kutumikia anapokea mengi kuliko anayotoa.

Hili si juma la kujihukumu.  Tunaweza kutambua zaidi kiasi cha ukosefu wa uhuru katika maisha yetu, ila huu si wakati wa kujigeuzia macho.  Utakuwepo muda baadaye wa kuweka pamoja neema zote tulizopokea na kuzipa nafasi zifanye kazi pamoja kutushindia uhuru wetu wa kiroho.  Hii ni hatua itakayofuata katika safari yetu hii ya kiroho—tuache tamaa ya kutenda mema iutangulie utendaji wa mema.  Hili ni juma la kushinda na mkusanyiko unaoongezeka wa sura za watu wanaovutia, wenye sifa na dhamira zinazotuonyesha wazi nguvu au faida ya kuwa huru.
Katika juma hili kumbuka kulipa nafasi katika moyo zoezi hili la kupitia sura zinazokuvutia. Uamkapo, jipe muda wa sala fupi ya kuonyesha shauku yako: “Bwana, natamani kuvutiwa katika juma hili.  Fanyiza siku hii inivute karibu zaidi na jinsi watu wanavyoishi katika uhuru wa hali ya juu.” Niwapo njiani kwenda kazini, ninapofanya matembezi mafupi, ninapokuwa natayarisha mlo, sitengani na orodha yangu — natambua kuwa ipo moyoni na akilini mwangu; na kwa namna fulani naguswa na neema zinazoambatana na waliyoyatenda.  Ninapotaka kulala nasali: “Asante Bwana kwa nafasi ulizonipa leo ambapo moyo wangu ulisisimshwa na watu wanaonivutia.”

Kuchunguza maendeleo yangu katika juma hili, natazama kuona nimetafakari watu wangapi katika orodha yangu ya watu wanaonivutia.  Kuna majina mapya yanayonijia.  Haitakuwa rahisi kuiongoza tafakari yetu juma hili.  Ni rahisi zaidi kwetu kutafuta makosa kwa watu kuliko kuona yanayotuvutia. Ninapoona napoteza mwelekeo katika juma hili, ni vema nikirudia kusoma kurasa hizi ili kuupata tena mwongozo.  Kukusudia na kujiwekea ahadi au lengo la kubaki katika mwelekeo wangu sahihi — yaani kutambua nafasi yangu baina ya viumbe vya Mungu—inakuwa njia ya kupinga kila kinachonipa mvuto hadaa na kunipotosha.

Kumbuka daima kusema “Asante” katika juma hili.

Kwa Ajili ya Safari: Uhuru wa Kweli

Katika juma hili tupo katika utangulizi au dibaji ya Mazoezi ya Kiroho ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola.   Ni kama ufunguzi wa tamasha la muziki ambao tunategemea kuuzoea na kuburudika nao tutakavyokuwa tukiendelea kuusikiliza.  Tunategemea kukua katika kupendezwa na Mazoezi ya Kiroho kadiri tutakavyokuwa tukisonga nayo mbele.

Ugumu katika lile tunalosikia katika ufunguzi wa juma hili unaweza kutufanya kwa kiasi fulani kukosa raha na kujiuliza iwapo kweli tunataka kuendelea na mafungo haya.  Karibu na mwanzo wa Mazoezi haya, Mtakatifu Inyasi anatuonyesha maana ya uhuru ambayo kaitumia.  Najua kwamba kila mmoja wetu anapendelea maisha marefu, afya, heshima na mali ya kutosha.  Lakini mara baada ya sala ya taratibu tunaweza kuanza kutilia mashaka msimamo wetu: ni kweli tunataka vitu hivi? Kwa nini?  Waliovipata wamefaidika vipi? Hakuna ambao hawakuvipata na bado wakaishi maisha ya raha mustarehe? Kuendelea kufanya mazoezi haya inatupasa kujitenga na kujikwamua kabisa kutoka katika hamu na mivuto asilia ambayo inajionyesha katika kupendelea maisha marefu, afya nzuri, mali nk.  Huku ni kupata uhuru wa kutotawaliwa na hamu zetu za asili ambazo tukizipa kibali kisicho na masharti, daima hututaka tuchague kuishi kwa starehe, na starehe hiyo isiishe, na starehe hiyo ni kuwa na afya, utajiri na kuheshimiwa katika hali hiyo.  Hii ikiendekezwa yaweza kumfumba mtu macho awe tayari kufanya chochote kupata hasa mali; bila kujali uharibifu anaoufanya kwa watu wengine, kwa viumbe vya Mungu na hata kwake mwenyewe.

Mt. Inyasi anatuonyesha wazi kuwa hamu hizo asili ambazo ni kawaida ya kilimwengu, kama tusipokuwa makini na kuzitawala, zinaweza kuwa zinatupeleka zinapotaka, zinatutawala, zinatuweka kifungoni na kutufanya watumwa wake; hivyo basi kuharibu maisha yetu.  Hapa tunaalikwa kuchunguza mambo ambayo mara nyingi yanatutoa nje ya urari wa maisha.  Kwa mara ya kwanza katika mafungo haya, tunashauriwa kutazama iwapo tupo huru vya kutosha kupambana na utumwa wetu. Ni katika kufanya hivi tu ndipo tutakapokamilisha dibaji au utangulizi wa mazoezi ya kiroho na kuwa tayari kusonga mbele, huku mazoezi yanayofuata yakipata maana yake halisi.

Sharti tuwe wazi hapa: Mtakatifu Inyasi anadhani kuwa kama binadamu wa kawaida, ninayo mielekeo potofu.  Niko tayari kukubali waziwazi ukweli huu?  Baadaye Mtakatifu Inyasi atakuwa akitukaribisha kumwangalia Yesu kama kamanda mwadilifu wa maisha yetu na ya ulimwengu mzima—kiongozi atuwekaye katika mwelekeo na mpangilio sahihi wa yote.  Mtakatifu Inyasi anapotumia neno kutofungamana hana maana ya “kutojali”, bali anaweka mkazo mkali wa kuonyesha mwelekeo wa mafungo haya.  Hapa anaonyesha wazi jinsi ambavyo “kujali kupita kiasi” kunavyoweza kutufanya tusimtumainie Mungu Mtumainiwa, na hivyo kukosa uhuru wa kweli.  Tunavyosonga mbele tutajikuta tukiwa huru kumwangalia, kumsikiliza na kumfuasa Mungu kama Kamanda mwadilifu!

Katika juma hili tunaongozwa kuwa na uhuru utokanao na tafakari ya kweli na kujitolea binafsi katika moyo wa sala na ibada vinavyotendeka katika muda na neema aliyotuzawadia. Uhuru wa msingi katika juma hili ni utambuzi wa hali yetu ya mivuto na kibinadamu na kilimwengu, ambayo inapong’olewa makali na nguvu zake hadaa tukutanapo na kumpokeapo Yesu, hutiishwa na kuwa chini ya Mungu kama kamanda aibadilishaye kuwa chanzo cha urari ama ulinganifu wa maisha.


Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...

Bwana Mpendwa,

Ilikuwa rahisi zaidi juma lililopita.  Nliangalia na kutafakari urari na ulinganifu wa maisha katika dunia.  Niliweza kuuona katika jinsi uumbaji wako ulivyokuwa katika mpangilio thabiti—jinsi misimu ilivyobadilika, jua lilivyowia na kuchwea na katika mengi ya kustaajabisha.  Yote haya yalinionyesha ukuu na upendo wako ila hayakutisha hata kidogo wala kunigharimu chochote.

Lakini sasa ninakaribishwa kuangalia mlingano huo au kutokuwepo kwa mlingano huo katika maisha yangu.  Ninashtushwa ninapojikuta nikiulizwa iwapo nipo tayari kuziweka wazi sehemu zangu nilizoficha ambazo zinafanya maisha yangu yasiwe na mlingano kamili.  Ni kweli maisha yangu hayako katika mpangilio mzuri.  Ukweli huo unasisimua mambo fulani ndani yangu.  Kuna sehemu za maisha yangu ambazo zimeegemea sana upande mmoja hata najikuta nikilemewa upande huo kama vile nina maradhi fulani—labda naweza kusema haya ni maradhi ya kiroho!  Naogopa kutembea, naogopa kuanguka na zaidi naogopa kuonekana nimeanguka.  Basi naketi tu kivivu na kuangalia wenzangu wakipita na kusonga mbele.  Nabaki nikiwa nimejifungamanisha na kuvutiwa na jinsi wenzangu wanavyopita na kusonga mbele, ila sifanyi chochote kuhusu mvuto huo, naogopa kuanguka na kufedheheka.  Hii inanipa huzuni kwa kuwa nitakacho ni kusonga mbele nikutolee maisha yangu.

Nakusihi Bwana, nipe neema ya kuona jinsi ya kuyaweka maisha yangu katika usawa.  Nawezaje kuwa na hali ya utulivu na amani moyoni? Niwezeshe ee Bwana, kuwa katika amani hata pale ninapokuwa nimezungukwa na maadui wawezao kuharibu afya, uhai na mali ila hawawezi kamwe kuharibu jinsi unavyonijali.  Nipe uwezo wa kujitoa kikamilifu kwako na kukutumainia, uwe kamanda ninyekuamini wa mwelekeo wa maisha yangu; na wala tena nisiongozwe na fedha, majivuno, na woga wa mawazo ya watu kuhusu ninavyoonekana.

Lakini bado naogopa — ni nini hasa unachotaka nitende, Bwana wangu?  Ni nini na kwa kiasi gani napaswa kukifutilia mbali katika maisha yangu?  Naweza kufanya hivyo?  Tazama ninavyovutwa huku na kule, nikitaka maisha yangu yawe katika usawa na katika mwelekezo wako lakini bado nasita kuacha chochote nilichonacho sasa, nang’ang’ania vyote.  Hakika huu ni woga wangu tu; na katika woga huu nakugeukia na kufungua mikono na moyo nikiomba msaada wako.

Ee Bwana Mungu, nakusihi nisaidie kuishi maisha yangu katika hali ambayo inanisogeza karibu zaidi nawe.  Nisaidie kujitenga na yote ambayo hayanisaidii katika hilo.  Asante sana kwa upendo wako na kunijali kwako.  Asante sana kwa kuniumba na kupendelea mimi niwe katika njia yako.  Asante Bwana wangu!


Maandiko Matakatifu 

Waefeso 2
Warumi 8
Matayo 10:29-31

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO