JUMA LA SABA
Vurugu la Dhambi — Mwelekeo Binafsi
Mwongozo: Kuweka Wazi na Kutegua Fumbo la Dhambi Zetu

Juma lililopita tulipitia uwepo wa dhambi na udhambi wetu katika mtazamo wa upendo mkuu wa Mungu.  Juma hili tunajipa muda wa kuchungua mwelekeo au mfumo wa udhambi wetu ili kwamba tuweze kutambua kwa undani zaidi upendo wa Mungu na hamu kubwa aliyonayo Mungu ya kuhusiana nasi kwa karibu zaidi.

Sote tunajua ukweli kwamba kitambaa hufanywa kwa nyuzi nyingi zilizowekwa kwa mpangilio fulani ambao hukifanya kiwe kilivyo; na pengine nyuzi hizi huwa za rangi mbalimbali na hufumwa katika mpango maalum wa kukipa kitambaa sura aitakayo mfumaji.

Nasi hapa tunajaribu kuzichungua nyuzi za dhambi, ili kutambua jinsi dhambi zinavyozalika na mfumo au mwelekeo wake.  Kwa kufanya hivi tunategemea kutambua jinsi dhambi itokeavyo kati yetu.  Ni kipi hasa kinacholeta mvuto wa kutenda dhambi na ni mivutano ipi ipo moyoni mwangu?  Naweza kuanuisha motisha unaojenga ndani yangu silika ya kupingana na matakwa ya Mungu?  Naweza kutaja misingi ya ukosefu wa uhuru wangu? Najua chimbuko la hofu yangu?

Ukosefu wa uhuru huunga mkono na kustahimilisha dhambi, na pamoja hufanya changamano halisi la uovu.  Kwa hakika hakuna yeyote aamkaye asubuhi na kusema: “Nadhani leo nitaonyesha chuki sana kwa wenzangu; nimeamua kuwa mchoyo na mgomvi leo.”  Tena hakuna yeyote yule ambaye iwapo atapewa uhuru kamili wa kuchagua tabia yake kila siku atachagua kuwa mlafi, mzinzi, muonevu n.k.  Hakuna yeyote ambaye katika uhuru kamili na wa kweli atapendelea kusikia maskini na wagonjwa wakizidi kulia na kulalama katika mateso yao.  Sote tunajua kuwa ukweli wa udhambi wetu hauji kirahisi kiasi hicho.  Tunatenda dhambi kwa kuchagua kile ambacho tunadhani ni chema, kile ambacho tunadhani ni halali yetu na kile ambacho tunafikiri kuwa tunakihitaji.  Kama kila siku hatudhamirii wala kupanga kutenda dhambi, ni vipi basi uchaguzi wetu huangukia katika kutenda dhambi?  Tujaribu basi kuchungua jinsi tunavyosogelea na kuangukia katika shimo la dhambi.

Katika juma hili lote, tujaribu kuongeza zaidi tamaa ya kupata msaada wa Mungu.  Kama vile tunapokuwa karibu kufanyiwa upasuaji usiokwepeka lakini wa hatari hospitalini—tunaongeza sala zetu kwa Mungu na tunawageukia wote watujuao na kuwasihi watuombee kwa Mungu; Kadhalika hapa tufanye hivyo hivyo, tukimwomba Mungu kwa juhudi zaidi na kuwasihi watakatifu wa Mungu kutuombea ili kupata utambuzi moyoni wa udhambi wetu.  Hapa naweza kuwawazia watakatifu wote waniombeao kuwa wana shauku kubwa ya kuniona huru.  Naweza kuchukuwa muda kidogo na Mama Maria, na kumwomba aniombee kwa Mwanaye ili nipate utambuzi huu muhimu sana.  Naweza kuhisi ukaribu wake kwangu katika wakati huu.  Kisha naweza kumgeukia Yesu uso kwa uso, na kumpa shukrani zangu nyingi kwa neema ambazo tayari nimepokea katika mafungo haya, na kumwomba aniombee kwa Mungu Baba, anipe neema ya kuona mfumo wa udhambi katika maisha yangu.  Mwishowe namgeukia Mungu aliyeniumba na kumwomba anipe moyo ulio wazi kupokea uhuru ninaojaliwa.

Kwa kadiri ninavyopata utambuzi wa fumbo na usiri wa udhambi wangu, ndivyo ninavyoongezewa hisia za huruma na upendo wa Mungu katika kifo na ufufuko wa Yesu Kristu—kunipenda kiasi cha kukubali kwa hiyari kufa ili mimi nipate uzima.

Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili

Ukweli, upole wa moyo na shukrani yakinifu ni neema ambazo tuna kiu ya kuzipata katika juma hili.  Ni njia gani ya hakika ambayo tunaweza kutuwezesha kuiweka mioyo yetu wazi kupokea neema hizi kutoka kwa Bwana ambaye pia kiu ana ya kutuzawadia hizo neema?

Kwanza ya yote, sharti tupitie mwongozo tuliopewa juma lililopita, hususan pale tulipoonywa kutokufanya mazoezi haya bila mwongozi.

Muhimu hapa ni kuwa na mtazamo mmoja wa kina—hapa natoa mifano michache.  Kama mojawapo ya dhambi niliyokumbuka ni kuwa miaka mingi iliyopita nilikuwa na uhusiano mchafu na mwenzangu, juma hili linanipa fursa ya kuzigundua na kuzipokea neema zinazohusiana na udhambi wangu huo (kila dhambi kubwa inatoa nafasi kama hiyo).  Kishawishi hapa ni kujiambia kuwa dhambi hiyo si kitu tena kwani niliitenda muda mrefu uliiopita, niliiungama nikapata msamaha wa dhambi, na hivyo basi nisijisumbue nayo kwa kuwa haitatokea tena.  Kwa nini kufufua majonzi na maumivu yaliyopita?  Muda huu waweza kufaa kupokea neema kadhaa mpya.  Naweza kuomba kutambua mfuatano wa matukio, watu na hisia zilizoniongoza hadi nikatenda dhambi hiyo au kwa maneno mengine naweza kuomba neema ya kutambua mfumo au muundo hasa wa dhambi hiyo.  Naweza kuomba utambuzi wa ulaghai na uzembe vinavyofanya msingi wa udhambi huo; pia naweza kuomba kufunuliwa upungufu, udhaifu na kiu niliyokuwa nayo wakati huo na uchoyo au ubinafsi ulioambatana na hali hizo.  Nikiendelea na mtiririko huo huku nikiwa na tumaini thabiti kuwa upendo wa Mungu na huruma yake vitanifunulia ukuu wa upendo huo wa Mungu, hakika nitapokea neema ya Mungu.  Labda naweza kugundua kina hasa cha udhambi wangu huo hakikuwa udhinifu, bali jaribio la kukwepa upweke au majonzi niliyokuwa navyo vikitawala hisia zangu.  Labda katika upitiaji wa udhambi wangu huo kwa uaminifu nitaweza kupewa neema ya kutambua kuwa dhambi yangu hasa ilikuwa ni kutomgeukia Mungu wakati nilipokuwa na mahitaji yaliyosababishwa na upweke na majonzi niliyokuwa nayo; kuwa sikumtegemea au hata kumsikiliza alipoonyesha utayari wake wa kunipa neema ambazo zingenisaidia wakati huo.  Ninapokuwa katika matatizo, natafuta kile ambacho kinanifumba macho nisiyaone matatizo hayo, kunikwepeshea maumivu ambayo ni dhahiri, kufunika aibu ya makosa yangu n.k.  Labda naweza kuona mfumo wangu wa kutokuwa tayari kuukubali msalaba katika maisha yangu—kuifisha nafsi yangu—kwa kuwa sikuwa nimepokea kiini cha uhuru niniopewa katika kifo cha Kristu msalabani kwa ajili yangu.  Na kile ambacho kinaweza kunivutia katika hicho kina cha upendo wa Mungu ni shauku ya kujua maliwazo na amani ya upendo ninavyopewa hapo, pale yote yanapowekwa wazi mbele ya mwanga wa upendo wa Mungu.

Iwapo  mojawampo ya maeneo ninayoyachunguza wiki hii ni namna mbalimbali za upungufu wangu katika kupenda, juma hili linaweza kuwa madhubuti katika kujua mchangamano wa kukwama kwangu kama vile katika tope kwenye njia nisiyojua itokapo wala ielekeapo; hivyo basi naweza bila kusita kupokea mwaliko wa kujisalimisha mimi na moyo wangu katika upendo anipao Mungu.  Ni msingi gani basi unafanya mipaka ya mahusiano ninaouweka?  Vipi kuhusu jinsi marafiki zangu na mimi tunavyohukumu bila pingamizi, na hata kuwashambulia wale ambao tunaamini ni wadhambi?  Ni upungufu gani wa upendo unaunda picha yangu mbele ya wengine?  Ni kipi kimekuwa msingi wa udororaji wangu katika kujihusisha na usaidizi kwa masikini?  Ni katika majibu ya maswali haya ndimo naweza kugundua neema ninazopewewa.  Hapa ndipo nitagundua haja ya kupata uponyaji wa kina wa sehemu zangu ambazo zimejificha ndani sana ya maisha yangu.  Kwa sababu sijioni mwenyewe kama mdhambi mkubwa, naweza mara nyingi kukwepa kutazama mifumo na vikwazo vinavyochangia kutokuwa kwangu mfuasi halisi wa Yesu—mfuasi wa Yesu kwa moyo wote.  Hapa ndipo ninapoigundua shauku ya Mungu ya kuumiliki moyo wangu wote; na bila shaka ni hapa pia nagundua kiini cha sala ya Mtakatifu Agostino: “Ewe Bwana, Mungu wetu, umetuumba sisi kwa ajili yako, na tazama mioyo yetu haitulii hadi ituliapo ndani yako”  na tunaweza kuongeza: kupumzika katika penzi lako la ajabu, lililo juu ya yote tuwezayo kuomba au kudhania.

Katika juma lote hili, lolote lile nitakalogundua litakuwa la kuniundia picha ionyeshayo jinsi ninavyopendwa na Mungu.  Mara moja baada ya nyingine, iwapo nitapenyeza mfumo huo kwa undani, nitagundua sura au taswira yangu mwenyewe ambayo inatatanisha, mara nyingi ikiwa inabadilikabadilika, chafu na isiyonivutia.  Nitashangazwa sana kugundua kuwa Mungu anampenda mtu huyu—nashangazwa sana na uwezo huu wa Mungu kumpenda huyu ambaye amejionyesha kuwa mtumishi asiyeaminika, aliye na moyo uliogawanyika.  Hapa ndipo Mungu anapofanya ufunuo wake.  Ni hapa ndipo tunagundua sisi ni nani hasa na kutambua uhitaji wetu wa mkombozi.

Kuna tafakari moja zaidi ambayo inaweza kutusaidia sana juma hili, hasa tujapojichunguza na kuyaangalia maisha yetu tukiwa tumezama katika sala.  Maishha yetu, kama ilivyo nyumba, daima yana sehemu ya mbele ipendezayo zaidi.  Tunaweza pia hapo kupanda maua, kupaka rangi nzuri ili hata wapitanjia waone jinsi tunapoishi palivyo safi na pa kupendeza.  Ndani ya nyumba pana sebule ambapo tunawakaribisha na kuketi na watu wanaokuja kututembelea na ni hapa tunawakaribisha kupata kinywaji au chakula.  Hata hivyo kuna sehemu zetu za siri ndani ya nyumba kama vile bafu na chumba cha kulala ambapo huendelea maisha yetu yaliyo ya undani zaidi, usiri na binafsi.  Hata hivyo tunaweza kuwa na chumba kingine ambapo tunahifadhi vitu visivyopendeza sana, vitu vilivyochakaa lakini hatuoni sababu ya kuvitupa au penye vitu vikuukuu tulivyovifunga katika maboksi ya mbao au chuma ambapo viko salama japokuwa maboksi hayo yanakusanya vumbi kila siku.  Kwa kuwa hatuingii mara kwa mara katika sehemu hii kunaweza kuwa kumevamiwa na panya, mende au mchwa na kufanya uharibifu wa vitu vingine bila sisi kutambua wala kujali.  Juma hili, tujaribu kujitafakari kuwa tunaingia katika chumba hicho kilichotengwa na kufungua lile kufuli ambalo hatujalifungua kwa munda mrefu sana.  Sipaswi kuwa na woga ninapoingia katika chumba hicho huku nikisindikizwa na Yesu, ambaye atanionyesha yote yaliyo humo.  Kuna vitu vilivyochakaa na ambavyo sitaki kumwonyesha mtu mwingine yeyote.  Kuna vitu vya kutia aibu hapo ambavyo nimevificha.  Ninapotembea ndani ya chumba hiki na Yesu anayeshuhudia yote, najaribu kumwaza akiniambia hapa ndani kuwa ananipenda sana, hapa mbele ya uchafu huu wote.  Naweza kumsikia akiniambia kuwa ananipenda mimi kikamilifu—ananipenda mimi mzima kama nilivyo.

Usilikwepe wala kuliogopa juma hili ukidhani litakuwa la kutisha na lenye hasara tupu.  Ukifanya hivyo utakuwa unatelekeza neema iliyo kubwa hasa.  Katika juma hili lote namna ya kujichunguza yaweza kuwa katika kujiuliza iwapo ninakua au kusonga mbele katika upendo wa Mungu; yaani katika kuwa na shukrani kwa upendo wake kwangu mimi binafsi ambaye ni mdhambi ila napendwa sana naye.  Hivyo basi mtazamo hautakuwa upande wetu bali upande wa yule apendeleaye kuijaza mioyo yetu ambayo bado inahitaji kutulizwa—upande wa yule atupendaye hata katika udhambi wetu.

Kwa Ajili ya Safari: Kuliwazwa Katika Majonzi Yetu

Sala ihusianayo na dhambi binafsi ina maana kadhaa.  Kusali kwenyewe ni kujipatia tena hali ya ukarimu ambayo nilikuwa nayo katika uhusiano wangu na Mungu na viumbe vyake.  Zawadi ya maisha yangu ipo katika hali ya mahusiano: Mungu mwenyewe katika nafsi yake kuwasiliana nami mwenyewe katika nafsi yangu.
Mfumo wa udhambi wangu binafsi upo katika jinsi nilivyogomea kuwasiliana na Mungu na hivyo kukataa kuona zawadi hizi kama zitokazo kwa Mungu, ila tu kama hoja ya kujizungumzia mimi mwenyewe.

Kusali kuhusu mfumo wa udhambi wangu unaweka kiini chake katika yale ninayoogopa, ninayoyahitaji, na hali zinazofanya madai au zinazozinduka kiasi cha kuhisika pale ninapopoteza mahusiano na zawadi nilizojaliwa katika jumuiya yangu na pia mimi kama kiumbe binafsi.  Matendo hutokana na misimamo ya dhamira, ubunifu na udhanifu wetu; hivyo basi woga huo na njaa huundika kuwa matendo ambayo tunaweza kuyaita dhambi binafsi, japokuwa kwa mtazamo mwingine si binafsi.  Kwa kifupi tu, udhambi huu ni pale ninaposahau au kukataa kuwa kila nilichonacho ni zawadi binafsi ya Mungu kwangu.  Katika juma hili tunasali na Yesu, na kukutana na wale ambao ni waaminifu kiasi cha kuukubili ugonjwa wao, udhaifu wao na majeraha yao.  Awali Yesu aweza kukutana nao katika hali ya kuwatibu, nao hapa sharti wazikabili nafsi zao katika hali ya unyenyekevu.  Sharti waukubali ukweli wa hali binafsi walizonazo. Tunaposali kuhudu dhambi zetu na mifumo ya kutojali wengine, sisi, kama yule Mwana Mpotevu (Yohana 15), sharti tuzinduke na kujirudia sisi wenyewe kwanza.  Yesu hukutana na wale ambao wamejirudia na kukabili nafsi zao wenyewe katika udhambi na udhaifu wao.

Ni muhimu sana kwa wele wanaotafakari mifumo ya dhambi kufanya hivyo wakiwa wameketi miguuni pa Yesu ambapo wanaweza kupata mguso wa macho yake yenye huruma.  Kufanya tafakari hiyo ya historia na mfumo wa udhambi wetu katika hali ya upweke hutudidimiza katika fedheha na kutufanya tujichukie.  Ukweli ni kwamba tafakari hii si ya kudhalilizha, ila ni utangulizi wa kurehemiwa.  Hatupotezi muda pale tunapoketi katika miguu ya Yesu na kuliwazwa katika mahangaiko yetu iwapo zoezi hili litatupa uhuru wa kweli na wa kudumu.

Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...
Bwana Mungu wangu,
Sina uhakika nianzie wapi, ila nadhani ni vema nikianzia na upendo wako.  Kama siuhisi wala kuutambua, sioni ni vipi naweza kuendelea na mafungo haya zaidi yapa.  Hapa nimeketi katika mwanga hafifu, nikizungukwa na kuzengwa na dhambi zangu zilizo kama funza wauvamiao mzoga.  Ninapoangalia kwa karibu zaidi, dhambi zingine zinaelekea kuongezeka.  Nayatafakari maisha yangu na kuona dhambi za msingi, na ninapoangalia tena, naona mfumo wa dhambi hizo, jinsi zinavyofuatana, kusababishana na kuungana mkono; na nagundua kuwa ni dhambi zile zile zinajirudiarudia, wakati mwingine katika sura tofauti kidogo, lakini zinafanana katika kiini.

Mungu wangu, tazama ninavyowatendea watu wenzangu: kwa hasira tena bila subira, daima kuamrisha na kutaka kushika usukani wa yote.  Maisha yangu yanaonekana kuwa yanatawaliwa na tamaa ya kutaka kuonekana mwadilifu, hata hivyo najua kuwa ndani nina sehemu nyingi ndogondogo zilizo na ubinafsi na uchoyo wa hali ya juu, sehemu zilizo katika giza tororo.  Ni nini kilicho ndani yangu kinifanyacho nikugeuzie mgongo na kukwepa hata kuitazama zawadi ya upendo unayonipa?

Tafadhali nakuomba Bwana wangu, niache nihisi tena uchungu wa kutenganishwa nawe.  Nipe nafasi ya kujua ni nini hasa matokeo ya kutenganishwa na upendo wako na kujikuta nikiwa nipo mbali na uso wako.  Nipe uhuru Mungu wangu—ninasue kutoka katika vitu ambavyo nimevithamini sana hata kuvipa umuhimu visivyostahili katika maisha yangu.  Gusa sehemu za maisha yangu ambazo zinahitaji sana uponyaji wako: gusa ubinafsi wangu unaonifanya nisahau jinsi ninavyotamani kuwa daima nawe.

Nisaidie niwageukie wengine kwa moyo wa huruma na msamaha; msamaha uleule na huruma ileile uliyonipa mara yingi kwa moyo wazi.  Ni vipi ninapata na hasira haraka hivyo na ninakosa kuwasamehe wenzangu, kisha nakugeukia wewe bila kuwaza, pale mimi ninapohitaji msamaha wako?

Nishike mkono taratibu Bwana wangu; na taratibu nivute karibu nawe.  Nipe kitulizo cha moyo wangu ambao unavunjika kwa sababu ya kutengana nawe.  Nifundishe kuwapenda na kuwathamini watu wengine kama vile unavyonitendea mimi.  Mara nyingi nimekuomba uniondolee ugumu wa moyo wangu ninaouelekeza kwa wenzangu
Napenda kukueleza kama vile Mtakatifu Petro alivyofanya: “Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!” Yesu akamwambia Petro, “Usiogope…”

Niponye, nishike mkono, kuwa nami daima Mungu wangu.

Maandiko Matakatifu:
Matayo 8:1–13
Luka 9:23–25
2 Wakorinto 12:8–10
Luka 5:1–11
Luka 5:17–26

Matayo 25:31–46

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO