JUMA LA KUMI NA NANE
Namna Tatu za Miitikio
Mwongozo:  Motisha

Kabla ya kurudi kwenye maisha ya Yesu, tuchukue wiki moja kuweka msingi wa tafakari zitakazofuata. Tunajua tutavutiwa ndani zaidi katika uhusiano wetu na Yesu na kuwa hii itatuweka huru zaidi katika maamuzi na chaguzi tutakazokuwa tukifanya katika maisha yetu.
Juma hili tukiendelea na shughuli na kazi zetu, tutakuwa ‘tukichambua moyoni’ simulizi ya kitafiti.  Tutafanya hali ya kufikirika lakini iliyo katika mfumo wa hali halisi ya maisha, na tutaangalia njia tatu za kuitikia hali halisi inayojitokeza maishani.

Hapa tumwaze mtu mmoja ambaye kajikuta katika hali ya maisha ambayo haimridhishi vya kutosha.  Si kwamba yupo katika kutenda maovu, ila mfumo wa kutenda alionao hautokani na kusikiliza mguso au msukumo wa Mungu katika maisha yake.  Hii inaweza kuwa ni kwa sababu ya kujifungamanisha sana na sura yake (jinsi anavyoonekana na watu) au kiasi kikubwa cha kujifurahisha kwa fahari za dunia kinachofanya furaha yake iwe tegemezi katika mali na utajiri tu.  Inawezekana pia kuwa amejiingiza katika mfumo wa kutumia vipaji vyake kufanya hila za kumfaidisha yeye, au kuwa na tabia ya kutokujali au ya uzembe katika maisha ya kifamilia au kikazi—hali ya kutokuweka juhudi yoyote bali kutekeleza wajibu tu.

Tukiwa na moja au zaidi ya hali kama hizo akilini katika juma hili, tutaangalia aina tatu za miitikio:

  1. Kutaka kujikwamua kutoka katika hali aliyonayo na kuwa msikivu wa mwito wa Mungu katika maisha yake ila kamwe hafanyi hivi.  Mtu mwenye ‘mwitikio’ wa namna hii ana nia njema tu ila haiweki nia hii katika vitendo.
  2. Kutaka kujikwamua kautoka katika hali aliyonayo ila kuishia kurazinisha mambo kiasi cha kufanya uthibitisho unaofanya ionekane kuwa namna hiyo ya kujifungamanisha na vitu au hali fulani ni kile hasa ambacho Mungu anataka.
  3. Kuwa katika hali si ya kutaka kutunza kitu au hadhi tuliyonayo wala kutaka kuiondolea mbali. Hii ni shauku ya kutaka kuwa katika hali huria kwa kuiondoa kwanza hali ya mfungamano au ung’ang’anizi.  Badala yake, mhusika anakuwa msikivu zaidi akijishikiliza zaidi kwenye upande wowote ule ambapo Mungu atakuwa akimsukumia au kumvutia kutenda muda huu na wakati huu.  Shauku yake ya kujikwamua inakuwa halisi zaidi: anataka tu kile ambacho kitakuwa cha kumtumikia Mungu zaidi.  Chochote kitakachokuwa cha kumtumikia Mungu zaidi kuliko vingine kinakuwa ndicho kinachompa motisha wa kipi achague au uamuzi gani atekeleze.

Tunapojiandaa kutafakari zaidi maisha ya Yesu, tunaomba neema za kutusaidia juma hili, labda kila asubuhi tunapoamka na kila usiku kabla ya kulala.  Tunaomba tujaliwe kuwa huru zaidi na zaidi katika kufanya miitikio yetu, kuwa yote tunayochagua yawe kwa kumtukuza Mungu zaidi na kwa wokovu wa roho zetu.

Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili

Juma hili ni tafakari nyepesi ya pili ya kututayarisha kuendelea kutafakari maisha ya Yesu.  Itatusaidia vilevile kuwa makini zaidi na wanyenyekevu katika kuitikia mialiko ya Mungu ya kutufanya huru zaidi na zaidi.

Ni muhimu sana kukumbuka kuwa hii haihusu uchaguzi au uamuzi wa kuwa mtu mwema, kinyume cha mtu mbaya.  Ni jambo lenye ugumu na utata zaidi kuliko ‘kufanaya uamuzi wa kuwa mwema’.  Tunategemea kwamba tayari tuna shauku inayokuwa ya kumjua, kumpenda na kumtumikia Yesu, ambaye ametukomboa kutoka katika dhambi zetu.

Juma hili ni la kutafakari namna za kuitikia.  Tunapoingia ndani zaidi katika maisha yanayotuvuta katika mwelekeo wa maisha ya Yesu, kifo chake na ufufuko wake; tunawaza ni jinsi gani inawezekana kukwepa uhuru ambao tunapatiwa.  Kisha tunatambua kuwa kabla ya yote katika maisha yetu, mwitikio pekee ambao tuna shauku nao ni kuwa huru.

Kuwa wanadamu ni kujijengea mishikamano na vitu, mishimano katika kujiundia tabia za kuishi, na hakika ya matunzo ya kudumu na kutambulika.  Nia ya juma hili siyo kufanya orodha ya mishikamano yote katika maisha yetu.  Nia yetu hapa ni kutafakari mwitikio wetu na kwa kifupi kuelezea shauku yetu ya kuwa huru.
Uzoefu unaonyesha kuwa tunaweza kutumia juma zima kuweka katika maneno jinsi ilivyo shauku yetu ya kufanya mwitikio.  Tunaweza kuamka asubushi na kwenda kitandani usiku tukisema maneno rahisi, “Maisha yangu yapo mikononi mwako.”  Sala ya mielekeo mitatu kupitia Kwa Mariamu, kupitia kwa Yesu, na kwa Mungu kuomba neema za kutuweka huru inaweza kuwa ya nguvu ya kutegemewa juma hili.
Juma hili, tunapokumbana mishikamano iliyo katika maisha yetu, tusiingilie ndani sana ila tukiri uwepo wake, na kisha tusali si kuomba mishikamano hiyo iondolewe, ila tuwekwe huru kutoka katika mishikamano hiyo.  Hapa na tuangalie mfano mdogo.  Kama nikiwa na aibu sana kukiri kuwa nimeshikamana sana ‘sura’ yangu mbele ya watu, naweza kuomba neema ya kuwa na shauku ya kumtukuza Mungu tu, wala si kujitukuza.  Naweza kuweka hili katika maneno jinsi ninavyotamani kutumia ‘sura’ yangu si kwa kuwavutia watu kwangu kwa ajili ya nia zangu binafsi bali ili niweze kumtumikia Mungu zaidi, na kupata wokovu wa roho yangu, kwa kutokujali iwapo sura yangu inapendeza au haipendezi.  Shauku yangu itakuwa moja tu, kuwa katika hali yoyote ile ambapo nitamtumikia Mungu zaidi.
Inawezekana kutokea kuwa katika juma hili kukawa na ugumu usiotarajiwa. Tunaweza kugundua vipingamizi vizito katika kutafuta kuwa huru.  Tunaweza kujikuta tunaingia ndani katika baadhi ya mishikamano yetu.  Tunaweza kugundua sauti kutoka ndani ikituambia au hata ikipaza sauti, “Sitaki kusalimisha mengi kiasi hicho, sitaki kuwa maskini wa roho na nina hakika sitaki hata kuonja umaskini wa mali.” Ni katika wakati huu ambapo jambo pekee lenye nguvu kubwa ni kuomba neema, kwa kutumia sauti iliyo ndani moyoni mwangu ambayo ina shauku ya kuwa zaidi na zaidi pamoja na Yesu na kuwa kama Yesu, na kuendelea kualikwa na Mungu kuwa katika kuungana na Yesu na kuiga maisha yake.  Tunaweza kusema, “Bwana, nahitaji kile tu kitakachonipa uhuru wa kweli na furaha halisi.”
Mwishowe, tunaweza kutoa shukrani zetu kwa Mungu, ambaye ametuleta karibu zaidi na Yesu. Tunajua bado hatujafika pale, ila tunapoelezea shauku yetu inayoongezeka ya kuwa kama Yesu, tunahisi ndani ya mioyo yetu kuongezeka kwa mvuto wa kuwa naye.

Kwa Ajili ya Safari: Uhuru Atupao Yesu

Ni vizuri sana kwetu kutokusahau nia yetu ya kufanya mafungo haya.  Tumemaliza nusu ya kwanza ya mafungo haya, na inawezekana kabisa kuwa tumepoteza kumbukumbu ya wapi hasa yote haya na sala hizi zinatuongoza.

Mtakatifu Inyasi alijua vema sana hali ya kutokuwa huru inayotukabili katika ubinadamu wetu.  Tuna masikitiko, woga, chuki, ubinafsi, tamaa za kimwili, na historia binafsi—kwa asili, vyote hivi vikituvuta katika kujitosheleza na kujikinga binafsi.  Nia zetu binafsi zinatujengea hali ya maisha ambapo nguvu zote tulizozitaja hapo mwanzo zinaungana na kuwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi na uamuzi wetu.

Nia kuu ya mafungo haya ni kutafuta mapenzi ya Mungu na kisha kuwa na shauku ya kuishi mapenzi ya Mungu katika maisha yetu.  Mambo mawili magumu yanajitokeza eneo hili. Kwanza, sharti tukabiliane na nguvu zenye ushawishi mkubwa katika nia na tamaa zetu maishani. Pili, baada ya kukabiliana na nguvu hizo na kuzitawala, tunajitoa katika kutaka kutimiza mapenzi yetu binafsi, na kujaribu kutenda kile tunachosikia Mungu anatualika kutenda. Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa huku kutenda mapenzi ya Mungu si jambo rahisi.

Mt. Inyasi anatumia asili yetu ya kuvutiwa na kumiliki vitu kama mfano wa jinsi ilivyo vigumu kujikomboa, si tu kutoka katika utegemezi wa mali (vitu), ila pia kujikomboa kutoka katika kuvutiwa na kuwa na shauku ya mali.  Mivuto au tamaa katika maisha yetu ya kuwa na mamlaka, usalama na uhuru-binafsi ni kama mvuto wa asili wa maada kuelekea kati ya dunia.  Tunajiweka katika hali ya kutokuathirika na mvuto huu asili, kwa mfano kuwa katika hali ambapo tukianguka tusiumie sana, na tunakwepa kujitupa kutoka katika sehemu za juu sana na tunapoanguka hatutegemei kudunda na kurudi juu.  Hii inakuwa asili kwetu, na mara chache sana tunajaribu kufikiria au kutafakari kuhusu mvuto wa asili kwa miili yetu.

Mt. Inyasi anatupa Mazoezi ya Kiroho yakiwa na mwaliko wa kuishi tukiwa na utambuzi na kutilia maanani mivuto ya asili rohoni, na chaguzi au maamuzi ambayo huchipukia kutoka ndani (ya mivuto hiyo).  Kristu ana mivuto yenye mahitaji tofauti. Inambidi mtu kuizoea, na kama inavyokuwa jinsi mvutano wa asili wa maada wakati tunavyojifunza kuketi, kutambaa, kusimama, kutembea, kuruka mfereji nk., tunaweza kukosea na kuanguka, wakati mwingine kuumia, ili kuweza kuziishi hizi kanuni mpya za maisha.

Tumekuwa tukisali kwa kutumia matukio katika maisha ya awali ya Kristu hapa duniani, na tukirudia katika kutafakari maisha ya Kristu, tutakuwa tukiangalia maisha yake ya kitume.  Mtakatifu Inyasi anatutaka tutue kidogo juma hili na kuchunguza kiaminifu jinsi ilivyo vigumu kuziacha kanuni asilia za mivuto binafsi, na gharama za kujaribu kuishi katika uhuru ambao Yesu anatupatia.  Ni muhimu kusali tukiwa na utambuzi wa jinsi tulivyokuwa wa ulimwengu huu.  Mwito wake ni wa taratibu na wenye uvumilivu ila wenye msisitizo wa kudumu.  Tunafikiri tunajua kile kilicho muhimu kwetu, lakini akiwa anayetupenda kuliko tunavyojipenda, anatujia na kutupa njia nyingine ya maisha ambayo tunaweza kuichagua ikiwa tunaweza kudiriki kuipa nafasi.
Juma hili tunapinga kukana kwetu kuhusu ufuataji wetu wa njia za ulimwengu.  Tunasali tukiwa na matumaini kuwa, kwa neema zake, kidogo kidogo, hatua kwa hatua tunaweza kukua katika kuvutiwa na Yesu na njia zake kiasi ambacho japokuwa tunaweza kumiliki hiki au kile, tunakuwa na uhuru na wala hatui tukimilikiwa au kutumikishwa na chochote.
Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...
Mpenzi Mama Maria,
Juma kama hili linanyenyekeza tunapoangalia mienendo katika maisha yetu na jinsi yalivyofumwa kwa ajili ya heshima na utukufu wangu na wala si wa Mungu.  Ni rahisi sana kwangu kujithibitishia kuwa natenda mapenzi ya Mungu pale ninapokuwa na shaka ndani kabisa moyoni kuwa hii ni kwa manufaa yangu.  Najiangalia jinsi nilivyokuwa nikijiweka mbali na watu.  Mama Mariamu, uliwahi kutaka kujitenga na wale waliokukosoa au watu waliotaka kukuhukumu?  Najihisi binafsi nikifanya hivyo, halafu naangalia ile mitikio mitatu ya juma hili.  Mara nyingi, kama ilivyo katika mwitikio wa kwanza, najiambia, “Ndiyo, najua inaweza kuwa si jambo zuri kila mara kujitenga na watu na mahusiano nao.”  Nitajaribu kubadilika, kujifanya mnyonge na muwazi—lakini kwa namna fulani sifikii katika kutenda hilo niililodhamiria.
Mara nyingine huwa najiambia kuwa hakuna lolote lililo baya katika kujikinga na maumivu na kuwa kufanya hivyo kunanifanya nidhibiti athari za utoto wangu uliokuwa mgumu—hivyo basi ni sawa kabisa ninapojiweka pembeni na kukwepa kuwa karibu na watu.  Zaidi ya yote, Mungu atapenda kweli nijiweke katika maumivu yanaweza kusababishwa na watu wengine iwapo watajua hasa undani wangu?
Mariamu mama yangu, mwombe mwanao Yesu anisaidie.  Nataka kutenda yote peke yangu ila siwezi.  Niombee kwa Yesu anisaidie kuona kwamba iwapo nitaomba msaada kutoka kwake, huko si kuanguka bali kujiweka wazi, na katika uwazi huu ndiyo naweza kuhusiana na wengine na kupokea msaada wake.
 

Ee Mpendwa Yesu,
Nahitaji usaidizi wako na sijui nianzie wapi.  Nafanya mambo mengi sana ambayo yananikinga na adhari mbalimbali na kunitenga na watu wengine.  Ninapoiangalia picha ya Mama Teresa juma hili, silika yangu ya kwanza ni kuitupilia pembeni.  “Siwezi kuwa mtakatifu kiasi hicho!  Kwanza ni sharti niwe kama yeye?”  Lakini labda hilo silo unalonialikia mimi, ee Yesu wangu.  Ninapoyaangalia maisha yake Mama Teresa, naona alikuwa wazi sana kwa wengine, alikuwa tayari sana kuguswa na hata kudhuriwa na maumivu na mateso yao.  Labda ananikumbusha kuwa naweza kujiweka katika hali ya kutojali au kutohisi maumivu ya wengine kama njia ya kutohisi maumivu yangu binafsi.
Yesu Mpendwa, nisaidie kuhusiana na watu katika hali ya uwazi zaidi.  Lakini labda tena si hilo hasa linalohitajika.  Labda kinachohitajika si mimi kuwekwa sawa.  Labda si iwapo najitenga binafsi na wengine, ila iwapo kila nifanyacho ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu.  Sina hakika haya yote yana maana gani sasa.  Ninachojua ni kuwa nahitaji kukujua vema zaidi na kujiweka huru kutoka katika vitu na mambo katika maisha yangu ambayo yananizuia nisiishi ulivyoishi.
Tafadhali Ee Yesu wangu, niombee kwa Baba neema ya kuchagua kile tu ambacho ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kwa wokovu wa roho yangu.  Kama hii itabidi niwe wazi zaidi kwa watu, basi naomba neema ya kunisaidia kufanya hivyo.
 

Baba Mpendwa,
Nakugeukia na kukuomba unisaidie niweze kuchagua yale tu yaliyo kwa sifa na utukufu wako na kwa wokovu wa roho yangu.  Nisaidie kuhusiana na watu katika hali ambayo si kwa ajili ya kujikinga binafsi ila kwa utukufu wako.  Pokea sala yangu ninayoileta nikinyenyekea kwako kwamba unipe mwongozo na busara ninayohitaji kuishi siku hii kwa ajili yako tu, wewe Mungu wangu.
Nisaidie kukumbuka kuwa naweza kuchanganyikiwa kirahisi na kutoka katika njia sahihi niwapo katika zoezi la kuchunguza yale hasa yanayonipa motisha mbalimbali maishani.  Ee Baba Mungu, mara nyingine kujichunguza sana kunanifanya niwe mbinafsi na kuacha kuona yanayotokea kwa wengine.  Nisaidie daima nikutazame wewe na jinsi ninavyoweza kukutumikia na jinsi ninavyoweza kuishi maisha yangu katika hali inayokupendeza.

Maandiko Matakatifu:
Luka                 18:18-30
Luka                 9:57-62
Matayo            6:24-34
Wafilipi           3:7-16
Zaburi              131