Nitaanzaje Kufanya Mafungo Haya?

Kila Juma la mafungo lina Ukurasa Mwongozo ambao huelekeza jinsi ya kufanya mafungo katika juma hilo.  Ukurasa Mwongozo unatoa mada ya wiki husika, hususan neema ya kusalia (kuomba) katika juma hilo.  Kwenye upande wa kulia wa Ukurasa Mwongozo wa kila juma kumewekwa zana za kukusaidia katika juma hilo.

  • Picha: Hii hutupa mwelekeo au shabaha ya juma husika.  Kuna maelekezo hapo kuhusiana na kuiweka picha hiyo kama taswira ya mbele ya kompyuta yako(tarakilishi yako).
  • Hatua ya Kwanza: Hapa pana mwongozo zaidi kwa ajili ya kuanza juma husika na kutoa mtazamo sahihi wa tafakari katika juma la mafungo.
  • Mkoba wa Safari: Padre Larry Gillick, S.J. huandika tafakari yake fupi ya juma hilo kama usaidizi wa kuingia na kuenenda vema katika safari hii ya kiroho.
  • Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo: Msaada katika kusali kwa lugha na maneno yangu mwenyewe.  Hapa nakaribishwa kuwa na mtazamo sahihi wa mafungo kama sala yangu.
  • Kusoma: Kusoma Maandiko Matakatifu au machapisho mengine yanisaidiayo kuomba neema ya wiki husika.
  • Sala: Hiki ni chanzo kikuu cha kustawisha tafakari katika juma la mafungo.

Kila Juma ni tofauti na majuma mengine kwa neema zinatotafutwa na yale yanayofanyiwa tafakari.  Hata hivyo, juma moja huanzia pale lililopita lilipoishia kiasi kwamba kuna mwelekeo mmoja kwenda mbele, hatua kwa hatua.
Mafungo haya yanatumia misukumo ya ndani ya Mazoezi ya Kiroho ya Mt. Inyasi wa Loyola kutusaidia kukua na kukomaa katika uhuru wa kiroho, na uwezo wa kuwa na uhusiano wa upendo mkuu na Mungu, hata wakati tukiwa tunabanwa na harakati na changamoto za maisha ya kila siku.

Nianze lini Mafungo? Unaweza kuanza mafungo wakati wowote.  Kama jinsi utakavyoona michango ya sala na tafakari za watu mbalimbali katika mtandao huu, kuna watu wanaofanya sehemu moja au nyingine ya mafungo ufanyayo kila wakati, sehemu nyingi duniani na katika lugha mabalimbali.  Pia tunatoa nafasi kwa yeyote apendaye kufanya mafungo kwa kufuata Kalenda ya Kiliturjia ya Kanisa—kalenda ambayo huanzia kati ya mwezi wa tisa.  Nafasi hii ni nzuri zaidi kwa watu wafanyao mafungo haya pamoja kama familia au marafiki, au kikundi cha waumini katika parokia au usharika fulani, au chama cha kitume katika shule au chuo.

Nifanyeje Mafungo Haya? Ni rahisi kabisa. Mwanzoni mwa juma, soma kwa makini Ukurasa Mwongozo wa juma husika, na zana za usaidizi zilizotolewa upande wa kulia wa ukurasa.  Hii itakupa mwongozo wa kutosha na kukupa mwelekeo wa mafungo katika juma husika.  Kwa kawaida, mwanzoni unakaribishwa kuitamani neema unayoomba katika juma husika kiasi kwamba nia ya kuipata inakuwa sehemu ya maisha yako.  Kiu ya kuipata neema hii inakuwa moyoni mwako pale unapozungumza au kusikiliza, unapohusiana na wengine, unapowaza, unapohudhuria mikutano, unapotenda lolote kazini au nyumbani, na katika shughuli na mahangaiko ya kila siku.  Yatupasa pia kila jioni au usiku kabla ya kulala kujipa muda mfupi kumtolea Mungu shukrani kwa yale aliyotujalia—kufanya hivi bila kukosa kunatuumbia moyo wa uhusiano wa karibu sana na Mungu.  Huku ni kuomba na kumfunulia Mungu moyo wako, na Mungu ambaye ni mwelekevu na mkarimu hukujazi neema za utambuzi wa ukaribu wake na moyo wako.

Ni Sharti Nitumie Nafasi Niliyopewa ya Kuchangia Tafakari?  Hii ni juu yako, hakuna shurutisho lolote.  Hata hivyo ushauri wetu ni kuwa ikiwa utachangia na wengine tafakari zako na utambuzi wa matendo ya Mungu katika mafungo na maisha yako, neema ulizopokea zinadurufishwa na kufanya makazi katika maisha yako.  Kuchangia huku kunaweza kuwa pamoja na mwongozi wako wa kiroho, rafiki yako, rafiki zako kwa pamoja, kikundi ambapo wewe ni mwanachama au pia na wengine ambao mnafanya mafungo haya pamoja.

Naweza kusoma michango ya wengine ya majuma ambayo bado sijayafikia katika mafungo?  Tunashauri na kukusisitizia usifanye hivyo.  Waweza kusoma Ukurasa wa Maoni kwa kwa kuwa huu una michango ya wale waliomaliza mafungo wakielezea hasa faida za kiroho na za kujengeka katika kuishi karama zetu kikristu walizopata kwa kufanya mafungo haya.  Hii inaweza kukujulisha mengi zaidi juu ya yele yawezayo kupatikana katika mafungo haya kwa mtandao.

Cha maana zaidi, mtumainie Mungu.  Mungu hapitwi na yeyote kwa ukarimu.

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO