JUMA LA MARUDIO
Kutua Kwa Muda Ili Kupitia Neema Tulilizopokea
Mwongozo: Neema za Kutuingiza Ndani Zaidi

Week 16
JUMA LA KUMI NA SITA

JUMA LA KUMI NA SABA

Tunatua tena kidogo ili kutoa nafasi kwa neema tulizopokea kupenyeza ndani zaidi mioyoni mwetu. Tunafanya mafungo haya huku tukiendelea kawaida na maisha na shughuli zetu za kila siku. Sasa tumezizoea sana tafakari zetu za kila siku na tayari zimekuwa zikituletea furaha. Tunajitayarisha kusonga mbele kuelekea kweny tafakari ambazo Yesu atatuonyesha kuhusu safari ya maisha yake.

Juma hili halitupeleki katika maeneo mapya, ila linatuingiza ndani zaidi katika eneo tulilopo.  Tunalianza juma hili kwa kuzitazama shauku zetu.  Naifanya upya shauku yangu, uchu wangu na uchaguzi wangu kuwa na Yesu—kutaka kumjua kwa ukaribu zaidi, kumpenda kwa undani zaidi na kumfuata kwa moyo zaidi. Juma hili si lenye harakati nyingi ndani moyoni au mawazo makali akilini.  Hii ni juma la kufanya uthibitisho.  Juma zima, kwa kutumia njia zangu mwenyewe, nakusudia kufanya kumbukumbu ya nia yangu kuu itawale akili na moyo wangu wakati wote, au nafanya bidii katika muda ninaopata kusema tena na tena “Ndiyo, hiki ndicho ninachotafuta;  Hiki ndicho ninachochagua—Kuwa nawe Yesu wangu.”

Juma hili ni la kuziimarisha neema tulizopokea maishani na mioyoni mwetu kwa kuzifurahia.  Najua kuwa huku kuimarisha uhusiano na Yesu kunanibadili, kunanipa uhuru, na kunanifundisha mengi kuhusu Yeye—yote kwa sababu nampenda huyu anayenipenda kwa pendo kamilifu na lisilo na masharti. Nahisi na kufurahia upendo huu juma lote.  Napendezwa na jinsi ninavyokua, napendezwa na yote yanayowekwa wazi ndani yangu.

Juma lote hili nitatua na kutulia, labda kwa namna ya pekee katika nyakati ngumu kuliko zote, na kutabasamu nikiwa na tabasamu la ndani kabisa moyoni linaloimarika.  Mali na heshima havinivutii kiasi hiki.  Natabasamu kwa kuwa naelewa ukweli huu na pia kwa kuwa ninavutiwa zaidi na namna ya Yesu ya kuishi—kujiengua kutoka katika njia ya majivuno.na kiburi na kuwa katika njia iongozayo kuelekea unyenyekevu mbele ya Mungu.

Kila usiku katika juma hili, maneno ya shukrani yatoke ndani kabisa ya moyo wangu.  Machafuko, mabaya au magumu—hata maaguko na dhambi zangu za siku—hazininyang’anyi shukrani yangu kwa Mungu wangu, bali vinaiimarisha.  Ninashukuru kwa kuwa Yesu ananivutia kwenye furaha ambayo sikuwahi kuitambua.  Ni furaha ambayo haitegemei kufaulu kwangu katika lolote, bali maisha yangu kuwekwa pamoja na ya Yesu Kristu, katika Mikono ya Mungu.

Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili
Juma la marudio ni tofauti sana na majuma mengine katika mafungo.  Hapa tunatulia pale ambapo tunapata mazao. Tunafaidi, kupendezwa na kufurahishwa na zawadi tulizopewa.  Pia tunatazama jinsi tulivyokuwa tukipendezwa, kufaidika na kufurahishwa katika mida mbalimbali tulipokuwa na wependwa wetu.  Tunabaki mahali pamoja kwa muda wa kutosha kuburudika na zawadi za mapendo ya Mungu.  Kutokusonga mbele haraka haraka kuanza jambo jipya kunaimarisha mapendo mioyoni mwetu.
Tunatumia mbinu zile zile tulizokuwa kukitumia katika majuma yaliyopita.  Mida mifupi mifupi lakini yenye malengo maalum katika siku yetu ndiyo inayotoa nafasi mafungo haya kufanyika. Labda juma hili tutakuwa tukitilia maanani zaidi hisia zetu, hususan zile ambazo zinaelekea kutupa furaha kubwa moyoni, hata wakati tukiwa katika migogoro na misukosuko mingi ya maisha ambayo inaelekea kutupotezea furaha.  Misukumo ndani ya mioyo yetu inatusaidia kuwa waangaalifu wa jinsi Mungu anavyofanya kazi ndani yetu.  Tunaizoea na kuwa wasikivu zaidi wa lugha ya Mungu ndani yetu kwa kuwa waangalifu katika kutambua na kutofautisha kati ya misukumo au mivutano ya moyoni inayoelekea kutoka kwa Mungu na ile ambayo inatokana na mambo yasiyo adilifu (machafu, matusi, vitisho), mambo ambayo yanapingana na kukua kwetu kiroho.  Tunapokuwa katika mwelekeo wa kumwacha Mungu, msukumo ya moyoni wa Mungu ni wa kutusumbua au kutupa pingamizi.  Msukumo usiotoka kwa Mungu hutuliwaza na kutupa uvivu na kila aina ya sababu za kuonyesha uzuri wa njia hiyo ya kuishi.

Tunapokuwa katika njia inayotuelekeza kwa Bwana, kama sehemu tulipofikia katika mafungo haya, tunaweza kuamini kuwa Bwana anatupa furaha kuu moyoni, hisia za kukombolewa, ujasiri (uimara) na amani.  Bwana anatupa kitu ambacho kinatusisimua moyoni na kusema “Hiki ni chema.  Hii ni sahihi.  Hili linatoka kwangu, liamini.” Pia, pale tunapokuwa na shauku ya kumjua Yesu, kumpenda na kumfuata, tunategemea kutakuwa na shauku pingamizi kutoka kwa msukumo usiotoka kwa Mungu.  Shauku pingamizi hizi hutujia kwa kutufanya tuwe na mashaka au wasiwasi, kuvurugikiwa au hata kuwa na huzuni ambayo chanzo chake hakitambuliki waziwazi.  Misukumo hii huzihuisha tabia za hapo zamani ambazo kwa sasa hazina maana tena na kuzifanya imara sasa.  Tunaweza kuifukuzia mbali misukumo hii miovu kwa urahisi sana kwa kusema huku tukitabasamu, “Najua kinachotokea na kuendelea hapa na sikihitaji.  Nachagua maisha na amani ambayo ninapewa.  Kwaheri.”

Sala ya Mielekeo Mitatu

Tamaa yetu ya kuwa na Yesu inavyozidi kuongezeka, tunaweza kufanya zoezi hili rahisi lenye kuonyesha uzito wa shauku zetu na uthabiti wa nia zetu.  Hii ni kwa kujifanyia igizo lenye uhalisi ambapo tunazungumza na Mariamu, Yesu Kristu na Mungu Baba katika mahusiano yao kwa wao na yao na mimi.  Mazungumzo haya ni kama vile kujiambia, “Hakika nazitaka neema hizi.”

Tunaweza kwanza kumgeukia Mariamu, mama mpendwa wa Yesu, ambaye tulitumia muda wetu kumtafakari katika majuma yaliyopita.  Tunaweza kumwomba amwombe mwanaye kwa niaba yetu, atupe neema hizi.  Hapa ni vema kuzitaja neema tunazohitaji.  Tunaweza kusema tunahitaji kuelewa njia hizi za kuwa na shauku na kupewa umaskini wa roho na hata umaskini wa mali kama hivyo vitatuwezesha kumtumikia Mungu zaidi na kusaidia kuokoa roho zetu.  Kama inasaidia, sala yetu kwa Mariamu inawenza kuhitimishwa kwa sala ya Salamu Maria.

Kisha tunaweza kumgeukia Yesu na kumwomba amwombe Mungu Baba, kwa niaba yetu, atupe neema hizo.  Iwapo tunaona ni vema, sala yetu kwa Yesu imalizikie na sala ya ‘Sala ya Mt. Inyasi: Roho ya Kristu...’.

Mwisho, tunamgeukia Mungu na Baba yetu na kumwomba atupatie hizo neema. Sala inayofaa kuhitimisha mazungumzo yetu na Baba yaweza kuwa Sala ya Bwana (sala ya ‘Baba Yetu...’).
Tusisahau kwamba maendeleo yetu kiroho ni zawadi kutoka kwa Mungu, na vilevile zawadi moja hutufungulia njia kupokea zawadi zingine.  Tumeona jinsi neema tunazopokea zinatutayarisha kupokea neema mpya.  Tunachohitaji ni daima kuwa tayari kupokea na kuamini kuwa Yule aliyetufikisha hadi hapa katika safari hii ya kiroho ataendelea kuwa mhisani wetu mwaminifu hadi mwisho.

Kwa Ajili ya Safari: Kristu Mwanadamu

Kuna kitendawili kimoja cha zamani ambacho kinasema, “Ni umbali gani mtu anapaswa kuingia mwituni kabla mtu huyo hajaanza safari ya kutoka mwituni?”  Katika Mazoezi ya Kiroho hakuna mstari wa kati ambao mtu anapouvuka anaanza safari ya kutoka.  Baada ya kufika umbali kiasi hiki, labda tumekwishagundua kuwa hakuna kutoka.  Ila hatupo katika mtego wala kunaswa kwa nyavu; bali tumeingia katika mwenendo wa maisha ambapo taratibu tunapata kutambua kuwa tunahitaji mwokozi, na kisha mwokozi huyu ni nani kwetu.

Juma hili tunaalikwa kutafakari uhalisi na ubinadamu wa Kristu anavyoendelea bila kikomo kuishi katika harakati za maisha yetu.  Hapa yupo mtu kamili, aliyezaliwa na mwanamke, mtu kama sisi kwa kila namna: kukua na kujifunza mambo mengi kupitia matukio katika maisha yake.  Kwa kifupi tunamtafakari Kristu aliyechukua ubinadamu wetu katika ukamilifu wake (na tunaposema ukamilifu hatuna maana ya mambo ya raha tu, bali pia yenye kuumiza na kuteseka).

Ni wapi kulikuwa mstari wa kati katika maisha ya Yesu?  Hapa tuna fumbo: Yesu alipoingia katika maisha ya uanadamu, alimweka kila mtu katikati ya maisha yake ya milele.  Kaingia ndani ya harakati za maisha yetu na hakuna mwisho katika hili, hivyo basi hakuna sehemu maalum ambapo anaanza kutoka.  Tunasali katika siku hizi bila kuchoka, huu ukiwa moyo wenye msimamo ndani ya upendo wake ulio ndani ya safari ya maisha yetu.

Woga wa asili wa mwanadamu wa kutelekezwa na woga wetu wa kuwa peke yetu vinakuwa mlango wake wa kuingia na kuwa kwa ajili yetu, na kuwa nasi.  Tunamshuhudia akikutana na wanyonge, wagonjwa, maskini, wanaotengwa, wanaodharauliwa na wote wale wanaowakilisha nafsi zetu zilizoangukia dhambini.  Kila mtu anajua kiasi gani watu mbalimbali ‘wanatutia kinyaa’ kwa sababu ya ubinafsi wao, hasira zao na uchoyo wao.  Tunaweza kusali kwa kutumia hisia tulizonazo kwa watu hawa, na tukiwa na hisia hizo, tunamwangalia Yesu akiwakumbatia, akiwagusa na kuwabariki watu kama hawa.  Tunaanza kusali kwa kutumia utofauti kati ya njia yake ya kuhusiana na watu na njia zetu za kuhusiana na watu.  Hata hivyo, tunavyozidi kumjua na kuwa karibu naye, namna hizo za kutazama na kutenda zinabalika.

Kile kilicho kigumu sana katika kufanya mabadiliko yoyote ni kuwa tumeridhika na tumevizoea sana vile ambavyo vinaonekana kwa asili kuwa vizuri na sahihi.  Si kwamba Yesu amekuja kuwa mfano; yeye ni jinsi maisha yanavyostahili kuwa na aliyaishi katika hali ya kutukaribisha nasi tuishi kama yeye.

Tunasali tukiwa na kusitasita kwetu, tukijiambia moyoni, “…yawezekana nadanganywa,” na udhaifu wetu katika kuitikia mialiko ya Yesu.  Tunajijua tulivyokuwa muda uliopita, na ni wazi kuwa tumepiga hatua mbele.  Tunatishwa na mapungufu yetu katika kutimiza ahadi zetu au kutekeleza yale tuliyonuia kwa muda ujao.  Tulichonacho cha uhakika mikononi ni ‘jinsi tulivyo sasa’ na neema ya kuweza kuangalia yaliyo ndani yetu na yanayotuzunguka sisi na ulimwengu wetu, ambao unaendelea kuhitaji mfululizo wa kupakatwa na Yesu.

Tunakuwa wakarimu juma hili kuweka muda wa kuchunguza hima ya Yesu katika kuishi maisha yake, upekee au utofauti ulikuwepo katika maisha yake; na shauku aliyonayo ya kuendelea kuishi hivyo ndani na miongoni mwetu.  Kuongoka kwetu si kwa kimaadili bali zaidi kwa kimantiki na kimsimamo.  Kuongoka kwetu tunakuona katika mahusiano na mitazamo yetu kwa watu wengine na mambo yanayohusu utu.  Watakatifu wengi mashuhuri katika historia iliwabidi kuishi maisha yao ndani ya uwepo wa maisha yao yaliyopita.  Iliwabidi kukabili jinsi udhaifu katika uaminifu wao ungeweza kuwa.  Pia walikabiliana ya kile ambacho Yesu alikikabili: kuwa na upendo binafsi na wa kuaminika kwa Mungu.  Kuongoka kwetu pia siyo jambo lisilowezekana kwa Mungu.  Upendo wa Mungu hauna ila, na miitikio yetu ni mizuri kiasi cha Mungu kutubariki na kuendelea kukomboa ulimwengu huu.

Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...

Yesu mpendwa,
Ninapopitia majuma kadhaa yaliyopita ya mafungo haya, navutiwa sana na wazo kutoka katika mwongozo wa juma lililopita: ‘Pale tunapoona ukweli kuwa yote ni zawadi, hatuwezi tena kujipima kwa kiwango cha yale tuliyojikusanyia au kujilimbikizia.’  Kinachonishangaza, Ee Yesu Mpendwa, ni kuwa wazo hilo linanivutia; Siogopeshwi vyovyote na hilo bali navutiwa nalo!  Inaonekana tofauti sana na jinsi ninavyoishi maisha yangu, lakini naona ni wazi kuwa kuna uhuru mkubwa katika kuishi hivyo.

Nataka kuukubali umaskini wa roho unaoniitia—nataka kutosheleza kiu hii niliyonayo moyoni.  Hisia hiyo ni mwaliko wako kwangu kujiunga nawe katika aina ya maisha unayoishi kwa kuwa unajua hivyo ndivyo nitakavyokuwa na furaha zaidi.  Unajua vema kuliko yeyote ninavyokuwa mtupu moyoni baada ya kupata mafanikio ‘makubwa sana’. Hata hivyo mafanikio ambayo yanaonekana yana thamani ndogo sana ndiyo yanayokuwa na maana zaidi.
Nataka kupokea kwa moyo umasikini unaonieleza katika fedheha.  Fedheha si jambo ambalo kwa kawaida natafuta, lakini katika hali hii napaona pale ambapo inatofautiana kabisa na heshina na mafanikio, mali na utajiri; vitu ambavyo nimekuwa nikivitumia kujaza sehemu zenye giza na zilizo tupu katika moyo wangu.

Ninapoiangalia picha ya mafungo ya juma lililopita, wanawake wawili ambao ni wahanga wa mabomu ya ardhini, najikuta nikiegemea huo ukuta wenye nyufa.  Ni nguvu gani za uovu zimewagarimu miguu yao?  Ni wanafamilia wao wangapi wamepotea katika harakati hizi za kujipatia nguvu, mali na heshima?  Kisha naona maandiko matakatifu yaliyonukuliwa chini ya picha: “Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Maskini wa roho humtegemea Mungu tu, naye huwabariki—hawa ni wana wa ufalme wa mbinguni.

Hicho ndicho nikitamanicho, zaidi ya chochote, maishani mwangu.  Tafadhali Mungu wangu, nifundishe kukutegemea.  Nionyeshe jinsi ya kuyatoa maisha yangu kwako, na kwa ajili yako.  Niongoze katika njia ya maisha uliyoichagua wewe mwenyewe.

Napenda sana kujiwekea lengo la mwaka mpya, ila hili nalitaka wakati huu, sasa hivi—ila naweza kweli kuhimili hii hamu yangu?  Ushauri “Kwa Ajili ya Safari” wa juma hili umeelezea hili vema kabisa: “Iliwabidi kukabili jinsi udhaifu katika uaminifu wao ungeweza kuwa.”  Tafadhali tazama, ee Yesu, peke yangu siwezi kuendelea kutaka hili.  Nahitaji kutambua mwito wako katika hili na mara nyingi sipendi kusikiliza.

Najua kasoro niliyonayo katika uaminifu wangu na sitambui kuwa yote ni zawadi katika maisha yangu.  Tafadhali nisaidie kuelewa kutoka sehemu ya ndani zaidi kuliko pale ambapo daima napenda kufikia—kuelewa kuwa mwito huu ni rahisi zaidi, una fedheha zaidi, kuna umaskini zaidi na ni njia ambayo unaitumia kuniongoza kufikia furaha ya kweli.