JUMA LA KWANZA
Tuanzie Hapo Mwanzoni: Hadithi ya Maisha Yetu
Mwongozo: Kumbukumbu Zinazotufanya Sisi Kuwa Tulivyo

Hili ni juma la kwanza la majuma 34 ya safari yetu ya kiroho.  Tunaanzia mwanzoni—hadithi ya maisha yetu.  Sala huhusu uhusiano wetu na Mungu.  Katika juma hili, tutaanza kukua katika uhusiano huu na Mungu katika sehemu zote za maisha yetu kwa kutafakari hadithi ya maisha yetu.  Hii inahusisha wazazi, ndugu na marafiki, labda hata na maadui; inahusisha matukio mengi tuliyoshuhudia na pia yaliyotokea lakini hatukuyashuhudia waziwazi kama kuzaliwa kwetu; yahusu hisia mbalimbali za ndani: furaha na huzuni, faraja na simanzi, maliwazo na hasira, vicheko na vilio nk.  Inahusu pia watu wengine waliogusa maisha yetu kama waalimu wa dini, shule na vyuo; waongozi na washauri wa kiroho, wahubiri, mapadre, wachungaji na hata wanakwaya au waimbaji.

Katika juma hili tunaweza kusikia mvuto wa kujipa muda mfupi wa kusali tukitafakari kwa undani hadithi yetu.  Cha maana zaidi ni kuwa inatupasa tuipe nafasi tafakari hii mioyoni mwetu katika juma hili.  Umewahi kujikuta ukiimba wimbo fulani unaoupenda au ulioupenda wakati ukitenda kazi bila hata ya kudhamiria kuimba?  Kuiweka moyoni hadithi ya maisha yetu ni kama hivyo.  Hadithi ya maisha yetu ipo mioyoni mwetu, na yaweza kujionyesha katika utambuzi na kumbukumbu ya mahusiano, matendo, fikra, hisia nk. zinazotufanya sisi kuwa tulivyo.  Tuipe tu nafasi hadithi hii ijisimulie kwetu kila siku—tudhamirie kuiacha iambatane na yote katika maisha yetu katika juma hili.
Tuache hii iwe taswira hai: juma hili, tupitie kitabu cha picha cha maisha yetu. Tuanzie na sura za mwanzoni: kumbukumbu za mwanzoni kabisa.  Tumpe Mungu nafasi atuonyeshe maisha yetu yalivyokuwa wakati huo.  Ni picha gani tunaipata?  Katika kila sehemu ya maisha yetu, ni lipi tunalokumbuka?  Ni picha za akina nani zinatujia?  Picha zingine ni za nyakati za furaha na sherehe wakati nyingine ni za huzuni, simanzi na maombolezo.  Zingine hata hatukumbuki kabisa zilikuwa na hisia zipi kwetu.  Hata hivyo zote zinafanya hadithi yetu na safari yatu ya maisha iliyotufikisha hapa tunapoanza mafungo haya.

Taratibu, usianze kwa kasi sana.  Chukua sehemu ndogo ya kitabu cha picha cha maisha yako.  Ukifanya zoezi hili kwa uaminifu kila siku utapata msaada mkubwa wa kujiandaa kwa majuma ya mafungo yaliyopo mbele yako.  Waweza pia kuandika sehemu ya hadithi yako au tafakari ya hadithi hiyo katika daftari kama hii inakupendeza.
Kila siku kabla ya kulala ukifunga siku yako ya shughuli zako, jipe muda mfupi ambapo kwa maneno machache kutoka moyoni mwako mpe shukrani zako yule Mungu Mmoja ambaye daima yu nawe katika maisha, hata wakati huu yungali nawe.

Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili

Katika kuanza safari hii ya kiroho, jambo la kwanza na muhimu kuliko yote ni kuwa na matumaini na imani yakini.  Mola daima yu mwingi wa ukarimu, na katika hilo hakuna wa kumfananisha.  Hivyo basi tukifanya hata mabadiliko kidogo tu katika ratiba ya maisha yetu wiki hii ili tuweze kupata nafasi ya kufanya mafungo haya, huu ni mlango mkubwa kabisa wa kumkaribisha Mungu kutenda kazi nafsini mwetu.  Njia moja ya kuhakikisha tunadumu katika matumaini na imani tulivyonavyo ni kufanya zoezi la kutambua au kujikumbusha uwepo wa Mungu.  Zoezi hili lichukue muda mfupi tu kila siku tuamkapo asubuhi, muda huo huo au tutendapo jambo hilo hilo, bila kukosa.  Kwa mfano ninapotafuta ndala zangu au kupiga mswaki, au ninapowekea chai katika kikombe naweza kumwambia Mungu moyoni au hata kwa sauti: “Bwana, najua u pamoja nami leo.”

Kila mtu atakuwa na urefu tofauti wa muda atakaotenga kufanya mafungo haya katika kila juma.  Tunashauri kwamba iwapo muda unakuwa mchache sana katika siku moja, jitahidi hata usome mwongozo wa siku hiyo.  Siku nyingine katika juma hilo unaweza kujikuta una muda wa ziada kukuwezesha kurudi nyuma na kutafakari yale uliyoacha ulipokuwa hauna muda wa kutosha.

Mwongozo wa juma hili unatupa nafasi ya kupitia kitabu cha picha cha maisha yetu.  Katika majuma haya yote ya mafungo, tutatumia zoezi na utaratibu kama huu wa kutoa nafasi au utambuzi wa tafakari au taswira fulani kuwa ndani ya mioyo yetu kila siku: yaani kuruhusu picha au sura fulani iwe sehemu ya maisha yetu, ikiambatana na yote tutendayo au tushuhudiayo.  Kila mmoja anajua kuwa kuna uwepo fulani katika katika utambuzi wa mioyo yetu. 

Wimbo au muziki unaoweza kuimbwa ndani ya mioyo yetu, nasi tukaurudia kwa sauti au kuburudishwa nao bila sisi kuimba kwa sauti ni mfano mzuri.  Mafungo haya yanatukaribisha tutumie vema kipaji hiki cha roho na akili.  Badala ya kuacha kipaji hiki kitumiwe na lolote litujialo na kujiondokea bila utashi wala utambuzi wetu, tunachagua kuwa na mtazamo makini zaidi wa utambuzi wa lile linaloingia na kutoka mioyoni mwetu: yale yanayotendeka katika maisha yetu na yale tunayotenda, maneno tuyosema na fikara zinazotujia; tunatenda jambo tukitambua kuwa tumedhamiria kufanya hivyo na si kwa msukumo tusiokuwa na habari nao.  Ijapokuwa tutakuwa tukiendelea kufanya shughuli zetu kama ilivyo kawaida katika maisha yetu ya kila siku, tutatumia mtazamo huo makini wa yote kulipa juma letu la maisha sura mpya.  Hii haina maana kuwa tutatumia muda mwingi kuwaza na kuwazua; hapana kabisa, ila tutendapo tutakuwa na utambuzi kuwa tunatenda, tuwapo na hisia fulani tutakuwa na utambuzi kuwa tunahisi, nk.  Hii haitasumbua wala kudororesha kazi zetu, bali mwishowe itatupa mtazamo mpya wa kazi na shughuli zetu.

Imekuwa wazi kuwa katika juma hili sote tumekumbushwa na kujua yaliyomo kitabu cha maisha yetu.  Hili si jipya. Lililo jipya ni kuwa nitaamua kuwa na utambuzi kuwa napitia au nasoma kitabu hiki cha maisha yangu katika juma hili kurasa moja baada ya nyingine, sura moja hadi nyingine.  Naweza kupanga ratiba, kwa mfano Jumatatu na Jumanne nitajikumbusha maisha yangu nilipokuwa mtoto; Jumatano na Alhamisi nitapitia sura za ujana wangu; Ijumaa na Jumamosi nisoma sura za maisha yangu yote ya utu uzima.  Hivyo basi, tukichukua mfano wa Jumatano yote, kuanzia ninapoamka na kutafuta ndala zangu, ninapooga na kujitazama kiooni nikichana nywele, ninapopata kifungua kinywa, ninapoelekea kazini, ninapotenda kazi pamoja na wafanyakazi wenzangu, ninaporudi nyumbani kutoka kazini, nipotayarisha au kujitayarisha kwa mlo wa jioni, ninapozungumza na familia yangu kuhusu jinsi siku yangu ilivyokuwa, hadi unapofika muda wa kupumzika kitandani—katika hayo yote ya kila siku, nitakuwa moyoni nimeambatanisha utambuzi wa yale ya ujana wangu ambayo yamenifanya niwe kama nilivyo Jumatano hii.

Zoezi hili linahusu hisia.  Kila sura katika kitabu cha maisha yangu ina hisia zinazoambatana nayo.  Naweza kuonekana jasiri na shupavu katima picha nikiwa shule ya msingi; kadhalika picha za ujana wangu zaweza kunipa hisia fulani hasa za mahusiano na marafiki.  Nikijiangalia nilivyokuwa katika nyakati mbalimbali, hisia zinazoambatana na nyakati hizo zitanijia iwapo nitazipa nafasi—hisia hizi zote zimepita ila zimeandikwa ndani moyoni mwangu, zikichangia kunifanya mimi nilivyo sasa.  Kuna hisia ambazo ni kali sana kama zinazoambatana na kufiwa na mtoto au yeyote tumpendaye, kuuguza ndugu, mafarakano katika familia au baina ya ndugu, vita na migongano ya kikabila, ugumu wa maisha wakati wa kutokuwa na ajira, nk.  Pia kuna hisia kali za furaha kama vile kumaliza masomo na kuanza kazi, kufunga ndoa, kuweka nadhiri za kitawa, kujaliwa kupata mtoto, nk.  Hisia zangu zitanisaidia kuona na kushuhudia jinsi ambavyo sura mbalimbali za kitabu cha maisha yangu zinavyoelezea hadithi ya maisha yangu, zinavyosimulia mimi ni nani leo.

Zoezi hili linahusu uaminifu wa Mungu: Maisha yangu si hadithi ya kubuni.  Katika sura zote za kitabu cha maisha yangu kuna neema niliyopewa nilipokuwa nikitafuta uwepo wa Mungu wakati huo.  Katika mahangaiko na shughuli zetu za kila siku, tunamtafuta Bwana kwa kudhamiria au hata kwa kutokudhamiria.  Ni katika kutambua uwepo wake tu ndipo tunaliwazika na shughuli zetu zinapata maana zinazostahili—yeye hatuachi daima, na kwa hilo ni muaminifu hasa.  Labda tu macho yetu wakati mwingine yanafumbwa na mahangaiko ya hapa duniani.  Iwapo katika juma hili nitamuwaza Mungu akiwa pamoja nami wakati wote—hata pale ambapo sikuhisi wala kutambua uwepo wake—hii ni neema kubwa sana ifanyayo maisha yangu kuwa kitu kimoja, ukweli mmoja.

Zoezi hili linahusu kuwa na moyo wa shukrani: katika kila kumbukumbu, sura na hisia, nijizoeze kusema “Asante”, hata kwa jambo linaniuma.  Nakumbuka hata pale ambapo sikuonyesha shukrani yoyote au nilitenda mabaya au kuwatendea mabaya wengine, Mungu alikuwa pale na hakuacha kunipenda.  Hivyo basi naiacha shukrani iguse, ipenye na kuzunguka sehemu zote ya maisha yangu.

Zoezi hili linahusu safari:  Huu ni mwanzo tu, bado tuna wiki thelathini na nne za kusafiri kiroho pamoja katika mafungo haya kwa mtandao.  Tutakuwa tukisonga mbele taratibu.  Kinachotakiwa ni kumpa Mungu nafasi ndogo tu ya kubadili maisha yetu ya kila siku, hatua kwa hatua.

Kwa Ajili ya Safari: Mtegemee Mungu Kutenda

Je, unajua ni nini lililo jema kwako?  Kujua lipi ni jema kwetu, na kulitenda jambo hilo jema ni mambo mawili tofauti.  Kwa mfano najua kwamba kufanya mazozi ya viungo ni jambo jema kwa mwili na roho; ila kwenda kwenye sehemu ya mazoezi si jambo jema tu, bali ni jambo ambalo sipendi kutenda mara kwa mara.

Kunywa vidonge vya kuongeza vitamini mwilini ni jambo jema kwetu kama watuambiavyo wataalamu wa afya.  Tumeanza kuwaamini, ila mara nyingi hatutumii vidonge hivyo wanavyotushauri.  Tunapinga kutenda yale ambayo hayatupi mara moja matokeo tunayotarajia.  Tunaweza kuanza Jumatatu asubuhi kuchagua mlo bora na utakaotuwezesha kupunguza uzito wenye madhara ya kiafya, na Jumanne tunaweza kuanza kuvunja masharti tuliyojiwekea.  Hii ni kwa sababu ya udhaifu wetu wa kutaka matokeo mazuri papo hapo.

Tunaanza majuma haya ya kufanya mazoezi ya kiroho kwa kufuata taratibu aliyotupa Mungu kupitia Mt. Inyasi wa Loyola, tukitambua kuwa tunao huo udhaifu wa kibinadamu wa kukwepa yale tunayojua kuwa mema ila hayatupi matokeo tunayotarajia haraka.

Hivyo basi, mwongozo wa kwanza ni huu: usitegemee, usiutafute wala usisitize au kulazimisha maendeleo.  Furahia na tenda unayotarajiwa hata pale, kama ilivyo kwa mazoezi ya mwili, hautayapenda kila siku.  Kama vile kuchagua mlo bora kwa afya ya mwili wako yaweza kukubidi kujitolea mambo fulani fulani kama vile muda mchache, starehe fulani au hata kuacha kuwa na sehemu unayoipenda.  Inaweza kukubidi kubadili ratiba ya maisha yako kiasi fulani, jambo ambalo hutalipenda na pengine rafiki na jamaa zako hawataridhika.  Hii ni kama sadaka fulani.  Tunamwachia Mungu awe chanzo cha ufunulio wowote, cha nyongeza au ukuaji wowote wa kiroho na wa kimaadili.
Huu ni mwongozo wa kwanza katika njia ya safari yetu: usisiishie wala kusimama hapa kwa kuwa safari hii ina faidha kubwa sana kulingana na yale yatakayokugharimu.  Amua kuendelea na safari — na safiri salama!

Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...

Bwana Wangu,
Jambo hili laonekana rahisi: kupitia kitabu cha picha za maisha yangu: naweza kweli kuliita jambo hili sala?  Naweza kujiletea kumbukumbu za awali katika maisha yangu, nilipokuwa mtoto mchanga.  Nashangaa kabisa, kitoto hiki kichanga kinahusiana vipi na mimi?

Ninapopanda ngazi ya maisha yangu najikuta shuleni nikijifunza kusoma na kupanua ulimwengu wangu, nakumbana na picha ambazo sitaki hata kuziona.  Zinanipa kumbukumbu za maumivu makali ambayo nilidhani nimeyazika mbali na sikutegemea lolote kuyafufua.  Si yote katika maisha ya utoto wangu yalikuwa mazuri—ulikuwa wapi Mungu wangu nyakati hizo?  Ulikuwepo niliposhuhudia malumbano, matupiano ya maneno mabaya na mayowe katika familia yangu?

Kulikuwa na nyakati nzuri hata hivyo—nilipokimbia huru huku na kule nikicheza na watoto wenzangu, tukikwea miti, tukitembelea sehemu za nchi zilizotuvutia kama makorongo mbalimbali na milima. Tuliketi wakati nje wakati wa kiangazi na kuimba nyimbo nzuri au kusikiliza hadithi nzuri na babu na nyanya zetu huku mbalamwezi ikimulika kama mshumaa angani.  Nakumbuka tuliporukaruka kwa furaha katika mvua siku mvua ya kwanza ya masika iliponyesha!  Katika uhuru wote huo na katika mazingira ya kupendeza nakiri kuhisi uwepo wako.

Nilipoongezeka umri, nilianza kufanya uchaguzi katika maisha.  Kwa muda fulani, Mungu wangu, sikujali uwepo wako kabisa na kutenda kama vile haukuwa lolote wala chochote katika maisha yangu.  Hata hivyo ulibaki nami kwa uaminifu bila kujali tabia yangu.  Ulioniogoza hata nilipofanya uchaguzi nikiwa na mawazo ya kujiridhisha nafsi yangu tu; ukaufanya kwa namna ya ajabu uchaguzi huo kunisaidia kujenga maisha yenye mapendo na furaha wakati huu.

Asante sana Mungu wangu, kwa uwepo wako usio na kikomo katika maisha yangu, hasa leo.

Bwana Wangu,
Najihisi kiasi fulani kukosa ridhaa.  Sala ya namna hii ni mpya kwangu na inakuwa rahisi zaidi kutumia maneno ya wengine.  Hata hivyo nilijaribu jana na haikuwa ngumu sana; ila tu sikujihisi kama vile nakusalia.
Nakurudia leo na naangalia sehemu katika kumbukumbu ya maisha yangu ambazo zinauma—kumbukumbu ambazo zinanishawishi nibadili mwelekeo, nijitenge nazo kabisa na kuzizika tena.  Kwa kweli haikuwa daima rahisi katika maisha yangu, na bado najiuliza iwapo kweli ulikuwa nami wakati na sehemu yote hayo yalipotokea.  Nahisi uwepo wako sasa, ila nakiri sikufikiri wala kushuhudia juu ya uwepo wako nami wakati huo.
Nyakati hizo ngumu zimechangia vipi kunifanya niwe nilivyo sasa?  Ni vipi mwongozo wako aminifu ulinisaidia mimi bila kuuhisi miaka hiyo yote?  Tafadhali nisaidie kuuona na kuutambua uwepo wako katika maisha yangu na kukubali kuongozwa nao.


Maandiko Matakatifu
Luka 12:22-34
Isaya 43: 1-4
Luka 11:1-3
Zaburi 8
Zaburi 139

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO