JUMA LA PILI

Hadithi ya Maisha Yetu: Kuingia Zaidi Ndani Yake
Mwongozo: Kuangalia kwa Makini Zaidi Hadithi za Maisha Yetu

Kama tulivyopitia “kitabu cha picha” cha hadithi za maisha yetu wiki iliyopita, zimetujia kumbukumbu ambazo zimetuonyesha uwepo wa Mungu katika safari ya maisha yetu hapa duniani.  Zoezi letu juma hili litatusaidia kuingia zaidi ndani ya hadithi za maisha yetu.

Njia mojawapo nzuri ya kupenya ndani zaidi katika hadithi za maisha yetu ni kujiuliza na kujibu maswali yaliyo muhimu.  Ni kweli tunaendelea kufanya mafungo haya ya kiroho kwa mtandao kati ya maisha yetu yenye harakati na changamoto nyingi katika juma hili na tutaendelea kuweka taswira fulani katika akili na mioyo yetu iwe “dirisha” kupitia kwalo tunaangalia na kutafakari juma zima, kama vile tulivyofanya katika juma la kwanza (angalia Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili).  Maswali haya muhimu ni rahisi kuyakumbuka na ni muhimu kwa kututayarisha kwa majuma yanayofuata.  Kama jinsi Mungu “alivyotuunga pamoja tumboni mwa mama zetu,” kama ituambiavyo Zaburi ya 139, kadhalika matukio mbalimbali na yale tunayotutokea katika maisha yetu huendelea kutufanya kuwa watu tulio leo hii. 

Tusikilize kwa makini majibu ambayo katika juma hili yatatufunulia kina cha uwepo na kazi za Mungu katika maisha yetu:
Ni neema gani muhimu na utambuzi gani muhimu au wenye kumbukumbu za majonzi zilinijia juma lililopita?
Katika juma lililopita, nilipenda kufanya mazoezi haya, na yalinihamasisha kuendelea na mafungo?

Ni lipi lililonivutia katika kukipitia “kitabu cha picha ya maisha yangu” juma lililopita?
Katika maisha yangu, ni wapi nilijihisi kujulikana bayana na Mungu?

Kuna sehemu ya maisha yangu ambayo imekuwa vigumu kudhani kuwa Mungu anaijua?  Je, hii ni kwa sababu inaniwia vigumu kukubali kuwa Mungu anaweza kunipokea katika hali hiyo?

Ni wapi kuna njia panda katika hadithi ya maisha yangu?  Maisha yangu yangeweza kuelekea kulia au kushoto— Mwenyezi Mungu alijionyesha vipi katika katika jinsi hadithi ya maisha yangu ilivyoendelea baada ya hapo?

Najikubali nilivyo leo hii?  Kama sivyo, sehemu ambazo sizikubali naweze kuziweka mbele ya Mungu?  Kama najikubali nilivyo, niko tayari kujitolea nafsi yangu kwa Mungu kama shukrani?

Kuna maeneo katika maisha yangu ambapo nahisi Mungu anapenda nionyeshe mapendo yake zaidi, nimpe nafasi ayafanyie mabadiliko chanya au kuyatumia zaidi kwa manufaa ya wengine?

Katika juma lote hili, naacha moyo wa shukrani uwe daima nami katika yote.  Namtolea Mungu shukrani kwa baraka ya jinsi alivyounganisha hadithi ya maisha yangu na uwepo wake wa kimapendo kwangu.  Juma hili naendelea kushuhudia na kuhisi kukua na kuimarika kwangu — kuendelea kuumbwa na yule aliyeanza kunitengeneza ndani ya tumbo la uzazi la mama yangu.

Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili

Maswali uliyojiuliza yanahusu juma hili, na hii itafanya uendelee kuyakumbuka katika juma hili.  Yanatusihi tugeuzie macho picha, kumbukumbu, njia panda na kumbukumbu bayana za maumivu.  Tunaweza kirahisi kusema “tazama, nimeshafanya hayo!”.  Nia yetu si kukupotezea muda:  kumbuka kuwa kumbukumbu hizi ni maalum kwa kuwa zinatoka ndani kabisa ya mioyo au maisha yetu.  Juma hili tunatakiwa tuweke pamoja hizo kumbukumbu maalum na kuzipitia tena kwa umakini sana ili ziwe njia ya kutuingiza ndani kabisa ya maisha yetu.
Kuna kiu yoyote inayojitokeza katika yale ya juma lililopita?  Swali hili litatujia mara kwa mara; ni swali linalotutaka tuwe macho na kuwa na taarifa zote, hata kama ni kuvutiwa kidogo na chochote au unapojitokeza mvuto wa udadisi wowote ndani yatu.  Kwa mfano naweza kuwa na kiu (matakwa) ndani yangu ya kutumia muda mwingi zaidi kutafakari muda fulani wa maisha yangu kwa kuwa sikupata muda wa kutosha kufanya hivyo juma lililopita.  Pia naweza kukumbuka watu muhimu katika maisha yangu ambao sijawasiliana nao kwa muda mrefu na navutiwa kuwaandikia barua au kuwasiliana nao kwa njia nyingine yoyote.

Baki pale unapopata matunda.  Mwongozo huu kutoka kwa Mtakatifu Inyasi wa Loyola ni wa busara sana.  Iwapo nimepata matunda: faraja, utambuzi wa kupendeza, hisia ya ukaribu na Mungu au hata elimu mpya—naweza kuamini kwamba hizo zawadi ni ishara kutoka kwa Mungu.  Ni sauti ya Mungu ikiniashiria mimi mtoto wake mpendwa niangalie ndani zaidi shehemu hizo kwa kuwa ana mengi zaidi ya kunipa.  Njia nyingine ya kutazama hili ni kudhani tunapokea zawadi ambayo imefunikwa na kupambwa vizuri sana.  Naweza kujua ni zawadi, hata naweza kujua mtoaji ni nani na pia naweza kumpa asante kabla hata ya kuifungua.  Mwongozo huu kutoka kwa Mtakatifu Inyasi unatualika kuchunguza zawadi na kutambua kile hasa tulichozawadiwa.

Kupata mchele safi na wali mtamu: Nadhani wengi wetu tunakumbuka msemo wa Kiswahili “wali waliwa, mchele wachelewa, mpunga wapungua”.  Katika msemo huu kumejificha taratibu kadhaa za kiasili na kitamaduni za kuutayarisha mpunga hadi ukafika mezani kwetu kama chakula kiwezacho kutushibisha na kuupa mwili nguvu.  Mpunga uliovunwa hauwezi kupikwa ulivyo, bali huwekwa katika kinu na kutwangwa kwa mtwangio.  Mtwangaji anao ujuzi wa kutosha katika kazi hiyo, hivyo basi hutwanga mpunga uliokauka vema na hujua jinsi ya kutwanga na utwangaji unapokuwa kamili.  Hapo ganda la nje la mpunga huwa limekoboka, na huanza kazi ya kupeta katika ungo ili kuondoa pumba ya mpunga.  Hufanya hivi hadi kubakiwa na mchele safi mweupe.  Huchambua pia mchele huu kuondoa vipande vidogo vya mawe au mchanga ambavyo huweza kuwa vimekusanywa pamoja na mpunga wakati wa uvunaji au ukaushaji wa mpunga.  Kinachobakia ni mchele safi ambao uko tayari kupikwa, na upikwapo kwa ujuzi wa mpishi tunapata chakula kitamu chenye manufaa kwa miili yetu.  Tazama hapa kuwa hatuwezi kuwa na mchele bila kazi ya kutwanga na kupeta mpunga, na hatuwezi kuwa na wali bila kazi ya kupika mchele.  Tunakula mpunga na mchele katika hali ya wali.  Iwapo basi tunataka wali sharti ifanyike kazi ya utwangaji, upetaji, uchambuzi na upishi.  Ndivyo ilivyo katika juma hili: yale yatujiayo katika akili na utambuzi wetu tuyafanyie kazi hadi tupate kilicho bora zaidi, kiwezacho kuliwa na mioyo yetu.  Twaweza, iwapo tunapenda kuandika taratibu tunazopitia hadi kupata kile kilicho bora hasa.

Tusisahau kuwa kuna maswali yajayoweza kujitokeza: mpunga umefanyika vipi? Ni nani anayempa mtwangaji, mpetaji, mchambuzi na mpishi nguvu na ujuzi wa kufanya hivi?  Wakati mwingine baada ya kutafakari hili tunaweza kupata hisia ya chakula kilichopikwa kutumia mchele huo: wali, biriani, pilau nk. na japokuwa hatuuoni, tunaweza kujawa na tamaa ya kula chakula hiki.  Tamaa hii ni zawadi kubwa kwa kuwa bila hii hatuwezi kuvutiwa kufanya kazi ili kupata chakula na hata tukipatapo hatuwezi kula au kufaidi utamu wa chakula bila tamaa hii.  Tamaa hii ni “neema” ya kuweza kupokea kazi ya mkulima wa mpunga, mtayarishaji wa mchele na mpishi.

Kuchekecha dhahabu: Kuchekecha dhahabu ni kama kuvua dhahabu katika mto au kijito na kuyatenga mawe hayo ya thamani mbali na mchanga na kokoto ambazo huchanganyika pamoja na dhahabu tunapovua kwa nyungo za nyavu.  Mfano wa kuchekecha maji na mchanga ili kupata dhahabu unafaa sana katika juma hili.  Jaribu kudhania katika kijito ambapo maji yanatiririka wakati wote kama mfano wa maisha yetu yenye harakati nyingi.  Unapoteresha ungo wa wavu wa kuchekechea dhahabu kwenye maji, ni lipi linatokea?  Napata ungo uliojaa vitu vingi.  Ninapoutikisa ungo huu, vipande vidogo vidogo vya yale niliyovua vinaanguka, na mwishowe nabakia na vipande vikubwa vya yote niliyovua kutoka katika kijito.  Nachunguza baina ya vipande hivi vikubwa na na nagundua kipande cha dhahabu safi.  Ujumbe hapa ni wazi: siwezi kupata kipande hicho cha jiwe la thamani kwa kuketi pembeni ya kijito kuangalia tu maji yapitavyo.  Ni lazika nifanye kazi—nichambue sehehu ya maisha yangu na kuzama ndani zaidi.  Kumbuka pia, iwapo nitapata dhahabu, ni muhimu kuipima uzito, kurekodi kipimo hicho kwa kuandika katika daftari na labda kuchangia habari hii nzuri na wenzangu katika ukurasa wa kuchangia katika mtandao wa mafungo haya.

Bado inahusu kutunza moyoni yale tunayoyathamini na kuacha mioyo yetu kuwa uwanja wa mafungo yetu. Tunapofanya mafungo haya, kila siku huwa changamoto ya kuutumia vema moyo wetu na yale tuliyohifadhi hapo.  Kuna mavumbi, mahangaiko, kelele na usumbufu mwingi katika maisha yetu ya kila siku.  Iwapo tunaweza kutunza jambo moja au mambo moyoni likabaki bila kutikiswa na misukosuko hii, tutaweza kufanikiwa kufanya jambo hilo kuwa na mguso wa maisha yetu ya kila siku.  Katika juma hili tuache mambo muhimu ya kuweka moyoni yawe yale maswali na majibu yake tutakayokuwa tukipata.  Kama tutakusudia kuwa kila jambo tunalotenda, tunawaza na tunalosema liguswe na maswali hayo, katika tafakari zetu tutakuwa tukipata majibu bora ya maswali hayo na kuyatunza mioyoni mwetu.  Tukifanya hivi, majibu hayo yatakuwa yakitakasa yoyote yale tuliyotunza mioyoni mwetu tangu awali.  Tutashuhudia mabadiliko makubwa katika maisha yetu.  Hapa tena kuandika majibu ya maswali ya juma hili ni muhimu, ikiwezekana nijijibie si kwa kutafakari moyoni tu, bali kwa kuweka majibu katika sentensi ambazo naweza kuziwaza akilini au kuzisema kwa sauti—hii husaidia kutunza kumbukumbu ya neema.

Mwishoni mwa juma tunataka kuyaweka wazi mbele ya Mungu maisha yetu yote, hususan sehemu zile ambazo hazituvutii kama zingine.  Jambo hili laweza kuonekana kama vile lisilokubalika, kama kumfunulia mwenzetu madonda yetu.  Lakini tukumbuke kuwa Mungu ndiye mponyaji.  Kuwa na ujasiri wa kumfunulia Mungu yale yasiyopendeza maishani mwetu ni ishara kuwa tumepokea neema kubwa ya Mungu—basi tumjie kwa moyo wa shukrani.
Furahia safari hii ya kiroho: tazama tunaanza kwa hiyari yetu kumpa Mungu nafasi zaidi afanye matendo yake ya upendo katika maisha yetu.  Mungu anaweza kufanya mema mengi yasiyoweza kuhesabika kwa akili wala kudhaniwa na mioyo yetu.  Tumtumainie Bwana katika safari hii ya kiroho na tuifurahie.

Kwa Ajili ya Safari: Kutazama Yale Mungu Anayotufunulia

Sala yetu katika juma hili inatuashiria kumtazama Mungu ambaye ametupenda na anatupenda kupita kiasi.  Mambo mawili yahusuyo jinsi upendo wa Mungu ulivyo yatatusaidia kusali kwa kutafakari uumbaji wake na viumbe vyake.
Upendo daima hutafuta kujionyesha.  Tunapompenda mtu huwa tunavutiwa kumfahamisha kwa maneno au kwa matendo yetu kuwa tunampenda.  Tunapenda kuwa naye mara kwa mara, kuzungumza au kuwasiliana naye mara nyingi, kumjulia hali, kumpongeza anapofanya jambo fulani zuri na kumliwaza anapokuwa katika majonzi.  Daima apendwaye anakuwa katika hali inayomkaribisha mpendwa wake aonyeshe mapendo yake.  Apendaye hufurahia akitambulika kuwa anapenda na ishara za upendo wake kupokelewa vema.

Upendo huonyeshwa matika maneno na ishara ambazo apendwaye anatazamiwa kuzielewa.  Apendaye humthamini mpendwa wake kiasi kwamba aweza kubadili namna yake ya kuonyesha upendo ili kulingana na ile ambayo inaweza kueleweka vema zaidi na mpendwa wake.  Kama apendwaye ni kipofu, kwa mfano, basi apendaye atajitahidi kujifunza lugha ya ishara ili aweze kuonyesha upendo wake.  Kama nampenda mtu azungumzaye lugha nyingine nisiyozungumza wala yeye hajui lugha yangu nitajitahidi kuondoa kizuizi hiki cha kuonyesha upendo wangu.  Apendaye hujiweka katika mazingira na hali ya yule ampendaye.

Katika kusali katika majuma yafuatayo, tutakuwa tukimtazama Mungu akitufunulia upendo wake kupitia ishara mbalimbali.  Tutaweza pia kuchunguza jinsi Mungu anavyojiweka katika mazingira yetu ili sisi tuweze kupokea upendo wake.  Tutasali kuona jinsi Mungu anavyotuvutia taratibu katika upendo wake kwa matendo yake mwanana yasiyokatishwa tamaa.

Tuanze kwa kwa utambuzi kuwa kila mmoja wetu ameumba na anaendelea kuumbwa na Mungu.  Uumbaji wa Mungu si kama wa fundi aundaye chombo, akamaliza na kukiacha hata akakisahau.  Hata baada ya kutuumba, bado Mungu anatulea na kututunza, anafanya kazi ndani yetu na kati yetu, anatupenda na daima anatafuta nafasi ya kuonyesha upendo huu kwetu na hufurahia tutambuapo na kuupokea upendo wake.  Kwa kifupi, Mungu anataka jambo moja tu: kuwa tutambue ufunuo wa mapendo yake kwetu yasiyo na mpaka wa kiasi wala muda; ufunuo huu wa mapendo yake kauweka katika hali yetu ya kibinadamu hivyo kwamba tunaweza kutambua ishara za mapendo yake na kuyapokea vema katika maisha yetu.

Ukweli kwamba sisi tumeumbwa na Mungu unaonyesha jinsi gani tuna thamani machoni pake.  Sala zetu katika majuma yafuatayo zitatusaidia kuona na kuitambua thamani hii na umuhimu wake katika maisha yetu.  Kwa namna nyingi sana Mungu anatuambia: “Tazama ujionee mwenyewe mtazamo wangu kwako; nisikilize utambue nilivyosema na ninavyokuwambia wewe ni nani mbele zangu.”  Tupo daima katika uwepo wa Mungu ambaye hawezi kuficha mapendo yake kwetu, sisi tulio kazi njema kabisa ya mikono yake mwenyewe.

Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...

Bwana Wangu Mpendwa,

Katika juma lililopita zilinijia kumbukumbu ambazo sikuzitegemea na zenye mguso mkubwa sana katika moyo wangu.  Niliposali na picha ya kitoto kinachobebwe na mamaye, niliona jinsi gani unavyonipenda.  Umenibeba vema nisianguke wala kudhurika na chochote.  Wakati mwingine napinga kuwa na taswira hii nikidhani nikitoka mikononi mwako nitakuwa huru, nikijitegemea bila kuhitaji msaada wa yeyote.

Katika juma hili Bwana wangu, nimetafakari jinsi unavyonitunza mimi binafsi.  Ulianza kunitunza tangu nilipokuwa katika tumbo la uzazi la mama yangu, nikiwa bado sijui hata sura ya mama yangu sembuse jina lako Bwana wangu.  Maneno ya mzaburi yamewasha moto moyoni mwangu: Wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani, uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu. Yawezekanaje unipende kiasi kikibwa hivyo tangu wakati huo hadi sasa?
Narudia tena katika kitabu cha picha za maisha yangu nilichokipitia juma lililopita na napitia sura ambamo uwepo wako ulikuwa dhahiri kabisa.  Haishangazi Bwana kuwa sura hizo ni za wakati mgumu sana katika maisha yangu—wakati uliokuwa wa majonzi na maumivu makubwa kwangu?  Inakuwaje sikugeukii wakati wa furaha na ushindi?  Ni nyakati hizo za faraja ya kidunia ndipo ninapojidanganya kuwa mimi ni bwana na mtawala wa maisha yangu yote, na kwamba sihitaji msaada wa wowote wala simtegemei yeyote!

Pale yote yanapokwenda vema, ninadhani akilini mwangu kuwa sharti niwe mkamilifu mbele zako, lakini ukweli ni kuwa sina ukamilifu.  Nangoja ifikie siku ambapo mimi mwenyewe nitajikamilisha na ndipo nije mbele zako, nistahili kuzungumza nawe.  Lakini tena matatizo yanaponisibu nakuja kwako mbio kuomba msaada!  Cha kushangaza ni kuwa upo daima ukinisubiri bila kukata tamaa.  Hata hivyo bado nadumu katika mawazo yangu dhaifu: sharti nijikamilish ndipo nikujie mimi na maisha yangu yote.  Kama nikifanikiwa kutatua hili tu kuhusu nafsi yangu, ndipo nitakapojitolea mimi na yote niliyonayo kwa Mungu.  Mara nagundua kuwa sasa lile ninalolitafuta, ukamilifu ninaouhitaji ni kukugeukia wewe na kujitoa kwako hivi nilivyo.  Wewe ndiwe ukamilifu wangu, bila wewe mimi si lolote.

Nishike mkono Bwana na niongoze kwenda ndani ya moyo wangu—mara nyingi naogopa kuingia huko.  Kaa nami ninapochunguza mapungufu na machafu yote niliyorundika katika moyo wangu.  Baki nami ninapoogopa hata kugeuzia macho hasira yangu, machungu yangu, majonzi yangu nk.  Hizi ni sehemu ambazo nataka kuzikwepa kabisa, lakini tazama ni sehemu ambapo nahitaji upendo wako zaidi.

Asante sana kwa kuwa nami siku hii, juma hili daima.  Nakushukuru sana kwa upendo wako na kwa kunijali kiasi hicho.  Nifundishe njia zako na kudumu katika pendo lako.

Maandiko Matakatifu:

Isaya 49:14-16
Hosea 11:1-4
Zaburi 23

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO