JUMA LA SITA
Vurugu ya Dhambi—Uasi Binafsi
Mwongozo: Wakati wa Kuitambua Nafsi Yangu kwa Undani

Baada ya Mfalme Daudi kuzini na Bethsheba na kumuua kwa makusudi Uria mumewe Bethsheba, Nabii Nathani alimjia akimletea fumbo.  Mtu tajiri aliyekuwa na kondoo wengi aliiba kondoo mmoja, mali pekee ya jirani yake maskini. Mfalme Daudi alijawa na ghadhabu juu ya uovu huo wa tajiri.  Ndipo Nathani alipomwambia Daudi: “wewe ndiye huyo mtu tajiri”.

Kila tunapoangalia dhambi ya kutisha ya ulimwengu wetu ambao Yesu aliufia msalabani, sharti tusite na kuwaza kuhusu uasi kama huo dhidi ya Mungu katika maisha yetu ya kila siku.

Tunamgeukia Mungu juma hili tukimwomba neema ya utambuzi wa dhambi zetu kama zilivyo, kwa nje na kwa undani wake.  Hii ni kwa ajili ya kutusaidia kutambua, kwa mapana na marefu, upendo wa Mungu kwa kila mtu binafsi.  Tunataka kutambua dhambi zetu kwa kutumia kiwango cha hisia zetu.

Nimetenda nini?  Ni kipi nimeshindwa kukitenda?  Je, hii ni tabia yangu au ni silika yangu?  Ni katika kipindi kipi cha maisha yangu?  Ni lini tangu mwanzo wa uhai wangu hadi sasa nimetenda kinyume na mapenzi ya Mungu?  Ni lini nilijitungia au kujifanyia sheria zangu mwenyewe?  Ni vipi nimekosa uaminifu: kwa wenzangu au kwangu mwenyewe?  Ni lini nilikuwa mkatili au mdhulumu? Nimepata kuwa na tamaa mbaya na uroho wa madaraka, mabavu, ulimbikizaji wa mali na ubinafsi?  Ni kwa vipi nimetunga sababu za uongo za kutetea vitendo vyangu vya uovu?  Ni kwa vipi nimekuza na moyo baridi kwa Mungu na kwa wenzangu?

Ni uovu gani ninauendeleza au kuundia nafasi ya kuendelea?  Ni nani wanaendelea kuumia au kuathiriwa vyovyote na ubinafsi wangu?  Ni vipi nimekuwa kiziwi kwa vilio vya masikini, kwa kutopenda kujishirikisha na kujiaminisha kuwa hilo halinihusu?  Ni vipi nimejifungia mwenyewe katika ulimwengu wangu peke yangu ili nisisubumbuliwe na mahitaji ya wengine?  Ni vipi starehe, raha na fahari zangu zinakuwa mzingo kwa wengine?  Ni vipi nimeshindwa kutambua, kujali, kuchunguza, kujihusisha, kusikiliza miito ya nyakati na kutafuta mabadiliko yanayohitajika?  Je! Maskini wananichukulia mimi kama msemaji na wakala au wakili wao?

Huu ni muda wa kujitambua kwa undani zaidi tukiwa na nia inayoongezeka ya kujua kuliko nyakati zote zilizopita, mapana na marefu yasiyopimika ya msamaha na upendo wa Mungu.  Hii si kwa ajili ya kufanya ukukandamizaji bali kuleta uhuru.  Tutagundua kwa namna zetu wenyewe tumeukana msalaba wa Kristu na kujitahidi kukwepa mapenzi ya Mungu.  Hata hivyo kila tunapofunga siku moja tutakuwa tukigundua kuwa msalaba unaashiria upendo mkuu ajabu ambao unatupa uhuru kutoka katika utumwa wa dhambi.

Hili kweli ni juma la kusema “asante” na tena kusema hivyo tukiwa na hisia zinazoongezeka za shukrani kwa Mungu.  Tujitafutie nyakati fupi fupi katika siku za juma hili kumpa Yesu Mfufuka shukrani zetu kwa maneno yetu wenyewe yabubujikayo kutoka katika hisia zetu za ndani kabisa—hisia zinazotokana na utambuzi wa upendo mkuu wa Mungu aliotufunulia kupitia msalaba wa Kristu.

Ushauri na usaidizi katika juma hili ni vya maana sana.  Masomo na sala zinazopendekezwa vina uzito wa pekee.  Ni vizuri pia ukisoma katika mtandao michango ya wenzako wanaofanya mafungo haya; nawe unashauriwa kuchangia tafakari zako, hata bila ya kujitaja jina iwapo ndivyo upendavyo.


Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili

Juma hili ni muhimu katika mafungo haya kwa kuwa linatuweka tayari kwa majuma yaliyo mbele yetu.  Tunajua wazi kuwa si juma rahisi kwa kuwa si utamaduni au mazoea yetu kuchunguza mioyo yetu mbele ya Mungu.
Tunapoanza, kuna tahadhari kadhaa ambazo tunapewa.  Kwanza kabisa, kama una mfadhaiko wa akili uliothibitishwa na wataalamu wa saikolojia, ni vema ukifanya mazoezi ya juma hili ukiwa na mwongozi wa kiroho.  Nia pekee ya juma hili ni kujawa na shukrani moyoni kwa ajili ya upendo wa kina na huruma kuu ya Mungu kwa ajili yangu.  Mwongozi wa kiroho atahakikisha kuwa mfungaji hatoki nje ya nia hii hasa wakati anapokutana moyoni mwake, kwa upande mmoja uso kwa uso na matendo yake yaliyo kinyume na mapenzi ya Mungu, na kwa upande mwingine Mungu anayeonyesha upendo na huruma yake kuu katika sadaka ya mwanaye pale msalabani.  Sharti maono haya mawili yawekwe katika hali ya kumfanya mfungaji aone anavyopendwa na kusamehewa sana, na siyo akwame katika mfadhaiko wa jinsi anavyomkosea Mungu.

Kwetu sote, sharti tujue kwamba mwitikio wa asili pale dhambi na uovu wetu vinapowekwa bayana ni aibu halisi.  Hii ni neema ya kwanza ya juma hili.  Neema ya pili ni utambuzi wa kushangaza kwamba namjua Mungu kwa undani zaidi pale moyo wangu unapofurishwa na upendo mkuu wa Mungu; naam, upendo mkuu kwangu mimi japokuwa mdhambi.  Neema hizi mbili za juma hili zinaambatana.  Kama najitahidi kukwepa aibu ya dhambi, inakuwa vigumu sana kwa Mungu kunipa nguvu ya kupata neema ya pili.

Kwa wale kati yetu ambao tumewahi kuaibishwa sana kwa kutukanwa au kudhalilishwa kwa namna yoyote ile kiasi kwamba mtazamo wa nafsi zetu umeathirika vibaya sana, kwa mfano kuwa na usugu wa aibu; neema ya aibu ya dhambi na uovu wetu sharti vifikiwe na kuhisiwa katika kutofautiana kwake na aibu haribifu.  Aibu kwa dhambi zetu haitujii kutudhalilisha, bali kutuonyesha ukweli wa uchafu wa dhambi, nasi hatupendi uchafu; na pia madonda yanayosababishwa na dhambi, nasi hatupendi kuishi na madonda.  Neema za juma hili zinaweza kuwa vyanzo vya tiba ya nafsi zetu iwapo tumekuwa na mtazamo unaozikana nafsi zetu kwa sababu ya kudhalilishwa kwa namna fulani.  Kwa yeyote apendeleaye uponyaji huu, tunashauri aendelee na mafungo haya akisaidiwa na mwongozi wa kiroho.

Hadi kufikia hapa, hatupaswi kuogopa kumwomba Mungu atuonyeshe sisi ni nani—atuonyeshe sis ni wadhambi wanaopendwa na Mungu.  Hebu na tupitie mbinu kadhaa za kuweza kutusaidia katika juma hili.

Inatupasa tuwe makini tunavyoanza juma hili.  Ukweli kwamba tunasali kuomba neema za Mungu, unatuambia toka mwanzoni kwamba hatutarajii kupata yale tunayotamani kwa juhudi zetu pekee.  Kwa maneno mengine, hii si kazi yetu binafsi, bali zawadi kutoka kwa Mungu.  Hivyo basi tunaanza kwa kuomba neema ya kuongozwa, kuelekezwa na kuonyeshwa njia.  Naweza kumwomba Mungu kuimulika njia anayotaka niione.  Naweza pia kumwomba Mungu anisaidie kuona sehemu katika maisha yangu ambapo nimekuwa muasi.

Inaweza kuonekana kana kwamba kuliweka juma hili moyoni katika maisha ya kila siku ni vigumu zaidi kuliko ilivyokuwa majuma yaliyopita, ila hii si kweli.  Naweza kutafuta nyakati za kukumbuka na kutafakari kama ilivyokuwa kawaida.  Naweza kuchagua kula chakula cha mchana peke yangu au kutafuta muda wa ziada wa kutembea kimya katika sehemu yenye ukimya nikiwaza na kutafakari; au pia naweza kuamua kuchelewa kulala kwa muda wa nusu saa au kuamka mapema nusu saa kabla ya muda wa kawaida na kuutumia wakati huo kutafakari na kuwaza.  Kilicho cha maana na kiini cha mafungo haya kinabaki kile kile—kuiunganisha siku yangu yote na hisia sahihi ya uwepo wa Mungu, kuanzia muda mara ninapoamka hadi muda mara kabla ya kulala.  Hisia hii hujawa zaidi na utambuzi wa jinsi Mungu anavyokuwa nami katika “safari” ya maisha hapa duniani.  Basi tunaweza kusema juma hili, kama katika majuma mengine, nakazia macho na kuwa na hadhari na yale ninayofanya katika siku na hivyo kuwa na mabadiliko chanya ya moyo mbele ya Muumba wangu.

Kuwa yakini kuna umuhimu wa pekee, na kuwa na mpango mathubuti ni jambo la hekima.  Kwa mfano, mwanzoni mwa juma hili naweza kupanga kuitafakari miaka ya ujana wangu, kisha katikakati ya wiki nikapitia miaka ya kati ya maisha yangu (baada ya ujana), na nikatafakari juu ya maisha yangu wakati huu katika sehemu ya mwisho ya juma.  Hatupendelei kuwa na hali isiyo dhahiri katika yote haya.  Tunapenda kupitia matendo dhahiri, mienendo iliyo wazi, tabia zisizobadilikabadilika, matokeo halisi ya maamuzi yanayojulikana, nafasi za kupenda zilizopita na jinsi nilivyokuwa kiziwi kwa vilio vya maskini.  Katika haya yote nitakuwa makini na mkweli iwezekanavyo.

Baadhi yetu tunaweza kushawishika kusema kuwa hatujatenda maovu mengi katika maisha yetu; hatukukosa uaminifu kazini wala hatukuwakosea wenzetu wala kukosa upendo kwa watu wengine; daima tumewafikiria maskini na kwa ukarimu kutoa muda na mali kuwapa usaidizi; na kuwa tumewafundisha watoto wetu kutenda mema tu.  Kwa maneno mengine tunasema sisi si watenda dhambi. Sharti tuwe makini zaidi katika kuchunguza mioyo yetu kuona iwapo kuna hata chembe ya majivuno na utoaji wa hukumu kwa wengine au kutokuwa na huruma kwa wale walio katika hali ngumu ya maisha.  Tukimwomba Mungu kutuonyesha hasa ni vipi hasa tunapaswa kujishitaki kwa makosa yetu, Mungu atatujalia neema ya kuona aibu kwa makosa hayo, badala ya kufumba macho na kujidanganya kuwa hatuna makosa.

Kwa baadhi yetu, tukitafakari kuhusu dhambi tunaweza kujikuta tukijiwa mawazoni na dhambi moja au dhambi za namna moja ambazo tunatambua zinatusonga.  Mmoja aweza kusema: “kila ninapotafakari dhambi, najiwa na mawazo ya tabia ya muda mrefu ya ulevi”.  Mwingine kila mara atafakaripo dhambi anaweza kujiwa na hisia ya hatia kwa kitendo cha udhinifu au unajisi alichotenda muda uliopita.  Mwingine anaweza kuwa kila akiwaza kuhusu dhambi, sura ya mtu anayemchukia sana inamjia na haoni ni vipi na lini anaweza kumsamehe kwa aliyowahi kumtendea. Kama hili litakuwa katika mtazamo wetu katika juma hili na kuwa njia ya Mungu kutuonyesha upendo na huruma, hii itakuwa ni neema ‘nono’ sana.  Hata hivyo, sharti tupingane na kishawishi cha kuishia hapo — kuona kwamba tafakari ya dhambi moja ni upeo wa yote.  Hebu na tuyaweke bayana maisha yetu yote.  Kwa wengi wetu ni jambo lisiloeleweka, jinsi ambavyo tumemwasi Mungu kwa kushindwa kumsifu, kumtukuza na kumtumikia. 

Tunataka kujua na kufaidika na upendo na huruma ya Mungu, si kwa kuwa tumetenda hili wala lile; tunataka kushuhudia upendo wa Mungu kwetu sisi kama tulivyo — tumekuwa akina nani na kwa sasa tunatambulika kama nani.

Mwishowe hili linaturudisha tena kwa Yesu: na tuifunge kila siku kwa kuzungumza na Yesu, tukimfunulia mioyo yetu jinsi rafiki afanyavyo kwa rafiki yake mpendwa, huku tukiwa tunajazwa hisia za shukrani kwa Yesu.
Jaribu kujihimiza kuchangia neema ulizopata katika juma hili, ama na mtu aliye karibu nawe au kwa kupitia kurasa za Kuchangia katika mtandao huu.  Tusikome kamwe kuombeana.

 

Kwa Ajili ya Safari: Upendo wa Mungu Uletao Wokovu

Sanamu ya Pieta iliyopo katika Basilika la Mt. Petro huko Roma, sasa imetunzwa salama katika uzingo wa kioo.  Kuna wakati sanamu hii ilikuwa wazi bila usalama wowote.  Kazi hii nzuri sana ya sanaa ilipata kuvamiwa na kuharibiwa vibaya na mtu aliyekuwa amepungukiwa akili.  Kwa sasa kazi za sanaa, hususan sanamu na michoro yenye zenye umashuhuri ulimwenguni, inalindwa na kutuzwa katika namna kama hiyo.  Hii ni kwa nini?

Dhambi ni sehemu ya uumbaji wa Mungu ambao pia unatufikishia kazi nzuri kama vile kazi za kupendeza za usanii wa binadamu, misitu, mito, fukwe na mandhari nyingine zinazovutia.  Dhambi pia ni sehemu ya uumbaji wa Mungu unaotuletea watu wengine: tunaohusiana nao moja kwa moja na tusiohusiana nao, tunaowajua na tusiowafahamu. Mwanzoni na kwa kiasi fulani kati ya Mazoezi ya Kiroho ya Mt. Inyasi, tunatafakari uumbaji wa Mungu na jinsi Mungu anavyoendeleza upendo wake kwa viumbe vyote.  Kwa maneno rahisi, dhambi ni tendo ambalo linatokana na tabia zangu za ubinafsi, uchoyo, uroho na pale mahusiano na chochote kati ya viumbe vya Mungu yanapochukua nafasi ya mahusiano ya Mungu na viumbe hivyo.  Hii inatukumbusha maadili ya kumwona Mungu katika kila kitu, na kukiona kila kitu ndani ya Mungu.

Kupitia mahitaji yangu ya ufanisi, naweza kuwa nimechukua kisu cha mezani kilichotengenezwa kwa madini ya fedha na kukitumia kuvunjia nazi.  Dhambi si pale kisu hicho kinapovunjika, bali ninapokosa kuheshimu kikomo cha uwezo wa madini ya fedha yalivyoumbwa na Mungu akatupa sisi. Dhambi pia ni kutokujali umuhimu kwa mtu mwingine, wa madini hayo ya fedha yanayofanya kisu hicho.

Unaweza pia kuchunguza tabia yako kwa kiwango cha Amri Kumi za Mungu na kugundua kuwa hujavunja hata amri moja.  Dhambi ipo zaidi katika mahusiano yetu na wengine, kuliko katika kutekeleza amri.  Muhimu zaidi ya Amri Kumi za Mungu ni maagano binafsi ambayo Mungu ameweka nasi kupitia uumbaji wake wote.  Dhambi huwa pale tunapokiuka, tunapodharau, tunapoacha kujali uhusiano wetu na Mungu, na kwa uhuru kamili kupendelea uhusiano wetu na kitu au mtu kuliko uhusiano wetu na Mungu—katika hili ubinafsi wetu au kimimimimi chetu huwa ndicho kichochezi.

Mtakatifu Inyasi anatupa taswira ya Mungu afanyaye kazi wakati wote kutupenda, kutuvutia katika upendo wake na kutupatia mahitaji ya kutuhimili katika maisha yetu.  Huruma ya Mungu ni kazi yake iliyo juu ya zote.  Huruma hii haipo tu katika kusamehe uvunjaji wa maagano ya Mungu nasi, bali ipo zaidi katika nia yake kubwa ya kutufanya zaidi na zaidi wenye kutambua, kufahamu na kuguswa na uwepo wake katika yote anayotupa.  Kutusamehe ni sehemu ya Mungu aliye pekee mwenye uwezo wa kutoa haki kamilifu, na hivyo kuendelea kumuumbia kila mmoja wetu sura ya huruma.

Yesu hakurudishwa nyuma na marafiki zake, wala kukatisha tamaa na wale waliopingana naye.  Daima alizungumza, alienda huku na kule akitekeleza kazi yake ya kutoa na kutambulisha ufunuo wa ukweli kamili.

Katika kusali juma hili ndani ya ulingo wa kutisha wa vurugu na dhambi, kaa karibu na picha (taswira) ya Yesu msalabani. Yupo hapo kufunulia kwa upande mmoja uovu wa dhambi na kwa  upande mwingine jinsi Mungu aukabilivyo uovu huo kwa mwitikio wa upendo.  Tunaweza kutazama chochote tukiwa tumesimama hapo pembeni ya Yesu msalabani.  Neema tunayotafuta juma hili ni shukrani kwa upendo wa Mungu ambao bila kukoma unaendelea kutukomboa, ukitufutia madeni yetu na kumenyeka ili kutushindia uzima, uzima katika ukamilifu wake.

 

Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...

Yesu Mpenzi,
Sitamani hata kufungua macho!  Mimi si kama Mfalme Daudi tu?  Naweza kujawa na ghadhabu juu ya hadithi ninayosoma kuhusu mambo ya ulimwengu huu—udhalimu wa viongozi madikteta, vifo kutokana na njaa wakati wengine wakitumia nafaka kutengeneza mafuta ya magari na uonevu kwa binadamu wasio na hatia. Wanawezaje kuwatendea binadamu wenzao namna hiyo?  Wanawezaje kuacha ubeberu wa viwanda uendelee, unyonjaji wa jasho la wafanyakazi udumishwe au mauaji ya kimbari yafanyike?  Lakini sasa ninapokusalia Mungu wangu, ninaona udhambi wangu unaanza kudhihirika.

Sijifikirii mimi kama mdhambi—mimi si mdhambi halisi.  Lakini hapa nasongwa na mapungufu yangu.  Tazama jinsi ninavyoyaita, ‘mapungufu’ tu! Nitazame Bwana, sitaki kukubali kuwa hayo ninayoyaita ‘mapungufu’ ni dhambi!  Hata hivyo ukweli unabaki pale pale: hayo ni madhambi yangu.  Ninajiona jinsi nilivyo mrahisi kuwahukumu wengine, na jinsi nifanyavyo haraka kuamua iwapo juhudi ya mtu fulani inastahili kusifiwa au la.  Ninaona aibu ninapoona jinsi nilivyofumbia macho chuki na dhuluma nyingi nilizonazo.

Mabaya yote haya ni sehemu yangu.  Bwana, natamani kujikimbia; natamani kukukimbia.  Ni vipi naweza kukutazama usoni nikiwa na madhambi hayo yote?  Hata hivyo, tafadhali Bwana, nakuomba unirehemu. Nataka kuguswa na pendo lako hadi ndani kabisa ya uhai wangu, na najua kwamba sharti kwanza nipokee msamaha wako.  Nionyeshe ukweli wa jinsi nilivyo, na dosari zangu zote.  Si jinsi ninavyowatendea wenzangu tu, bali naona hili ni jambo linaloingia ndani zaidi katika maisha na uhai wangu. Tazama jinsi ninavyowadharau na kuacha kuwajali wenzangu!  Najisingizia nina shughuli nyingi sana hata siwezi kupata muda wa kujihusisha na mambo ya wengine.  Najidanganya kuwa si shauri langu iwapo wengine ni maskini au hawana makazi.  Ninayo familia yangu ninayopaswa kuijali na kuitunza, na maisha yangu yanatosha kunipa cha kushughulikia.  Ninayo jumuiya yangu na nadhiri zangu ambazo ni mzigo wa kutosha, mizigo mingine ni ya wengine, mimi hainihusu.

Yesu wangu, nionee huruma na kuniponya.  Nisaidie kuishinda hali yangu ya kukuasi.  Ponya moyo wangu unaopinga kuwapenda watu wengine na kukataa kukupenda wewe.  Nionyeshe jinsi ninavyochagua kukudharau na kufumbia macho na masikio mafundisho yako.  Nionyeshe jinsi ninavyotenda dhambi dhidi yako na dhidi ya kaka na dada zangu.  Nifumbulie ubinafsi na uroho wangu, umimimimimi na uchoyo wangu.  Nionyeshe jinsi woga wangu unakuwa njia ya kuniweka mbali nawe.

Baki nami Bwana, na nipe msaada wako.  Nipe nafasi ya kulionja pendo lako.  Ruhusu ugumu wa moyo wangu ulainishwe na upendo wa moyo wako.  Niache nitunze upendo wako moyoni mwangu wakati wote, na kuachana na ugumu wa moyo, uasi, vurugu, chuki na dhuluma.  Nisaidie niwe wazi kwa wenzangu kama nilivyojiweka wazi kwa pendo lako.  Leo hii, usiku huu, nipe nafasi niukumbatie msalaba ambao mara nyingi nimeusaliti.  Nikiwa nimejawa shukrani, niache niwe nisiyejiweza mbele ya ajabu ya upendo wako kwangu.

Asante Bwana.  Asante kwa upendo wako usio na mwisho na kwa msamaha wako usio na kikomo.

Maandiko Matakatifu:
1 Yohana 1:8-2:2
Luka 15
Luka 7:36-50
Luka 18:9-14
Luka 19:1-10
Zaburi 51

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO