JUMA LA KUMI
Mwaliko wa Kupenda — Ambatana Nami Tafadhali
Mwongozo: Wito wa Ubatizo Wetu

Jaribu kuwaza kama vile rafiki yako karudi sasa hivi kutoka katika nchi iliyo na umaskini na matatizo yanayokithiri; nchi ambapo wengi hufa kwa vita, ukosefu wa chakula na magonjwa ya kila namna. Jaribu kuwaza mwito atakaokufikishia:

Rafiki yangu, niliyoshuhudia yamebadilisha maisha yangu kabisa. Moyo wangu bado unaguswa na mtoto mdogo niliyemkuta katika wodi ya watoto katika hospitali. Nasikia mwito kutoka ndani kabisa moyoni kurudi tena katika nchi hiyo na kujitolea kusaidia maskini ingalao kwa mwaka mmoja. Kama mimi na wewe tukipata nafasi ya kuweza kwenda huko, utakuwa tayari kuambatana nami tafadhali? Najua mimi na wewe tunaweza kufanya kazi pamoja kutenda jambo la kuwafaa maskini hawa. Katika kutenda kazi nitahitaji sana upendo wako kutiwa moyo na kuungwa mkono na wewe. Hakika nakuhitaji. Najua kuwa haitakuwa kazi rahisi kila wakati, lakini tukiwa pamoja bega kwa bega, hakika hatutalemewa kiasi cha kushindwa. Na najua dhahiri ni kwa kiasi gani tukifanya kazi pamoja kusaidia wengine kutaongeza upendo baina yetu, pale tutakapoona tunakamilisha jambo la taadhima pamoja. Tafadhali ambatana nami.

Katika juma hili zima, tutakuwa tukitafakari nguvu ya mwito huu kama vile umetoka kwa mtu tumpendaye hasa. Utakuwa na matokeo au athari gani kwangu? Kama huyu ni mtu nimpendaye, vitisho vya hali ngumu ambayo inaweza kutukabili katika kutoa msaada inaweza kutukatisha tamaa tuuweke pembeni mpango huu? Vilevile katika juma hili tutalinganisha mwito huo na mwaliko tuupokeao kutoka kwa Yesu Kristu:

Katika majuma kadhaa yaliyopita, imekuwa furaha niliyokuwa nikiitamani—kukuonyesha wazi wazi jinsi ninavyokupenda. Hakika ni kwa kiasi kikubwa sana nilipenda wewe utambue shauku yangu kubwa ya kuiweka huru roho yako. Na sasa kwa kuwa umeniomba nikufunulie ni jinsi gani waweza kuyaitikia mapendo yangu kwako, najawa na shauku ya kukualika uambatane nami.

Tafadhali tembea nami; ambatana nami katika kutekeleza kazi niliyotumwa na Baba Yangu. “Kwa kuwa Mungu kanituma mimi kuleta Habari Njema kwa maskini, kutangaza uhuru kwa waliofungwa, kufungua macho ya vipofu, na kumweka huru yeyote anayeteseka.”

Hakika nakuhitaji wewe. Nahitaji wewe uwe huru moyoni kuniunga mkono. Najua kuwa haitakuwa rahisi kila wakati; lakini tutakuwa pamoja, kila wakati ukiwa nami katika mapendo. Ukiwa nami katika harakati za kupenda, tutakua pamoja katika upendo kwa namna ambayo siwezi kukuelezea kikamilifu kwa lugha ya kibinadamu. Jinsi utakavyokuwa nami katika kufa kwa “maisha ya upendo-binafsi” katika mwito wetu, ndivyo utakavyokuwa nami katika ukamilifu wa uzima wa milele. Tazama, utawala wa Mungu u karibu. Pamoja tunaweza kuwashirikisha wengi katika Ufalme huu. Tafadhali ambatana nami.

Jaribu kutafari mwito huu juma hili. Acha uguse moyo wako—uhisi moyoni. Mwito huu hakika ni mwito wa ubatizo katika Kristu. Mwito huu si tungo batili ya fikara zetu au ubunifu wa kisanii. Ni mwito halisi na si ndoto tupu. Tazama ni jinsi gani tumependelewa kupata mwito huu wa mapendo!

Kama kawaida faidika kwa kutumia yale unayopewa katika mtandao huu. Bofya katika picha uliyopewa ili kuikuza, na ukipenda kuifanya taswira juu ya kompyuta yako, fuata maelezo unayopewa. Tudumu katika kuombeana sote tufanyao mafungo haya, hata kama hatuonani uso kwa uso. Jaribu pia kuchangia na wengine neema unazopokea.

Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili


Tafakari yetu juma hili ni juu ya mwito wa upendo. Kwa majuma kadhaa yaliyopita, tumekuwa tukiona jinsi upendo ulivyo na nguvu ya kuleta mabadiliko au mageuzi pendelevu. Kama wadhambi tunaopendwa na kupendeka na Mungu, tumeshuhudia miguso miwili ya kiroho: upendo wa Mungu kwetu, na mvuto wa hamu yetu ya kuuitikia upendo huo. Katika mazoezi haya, tumepata utambuzi na ufahamu kuwa uhusiano wetu na Mungu si uhusiano batili au wa masihara. Hakika, kila jambo katika maisha yetu linabadilika kwa kadiri tunavyoingia ndani zaidia katika uhusiano huu na mungu.

Yawezekana hapo awali ulitenda mema na kukwepa kutenda maovu kwa kuwa ulifuata amri, sheria au wajibu kama mkristu au raia mema; sasa matendo yako mema ni matokeo ya kutafuta njia ya kuonyesha shukrani kwa yule aliyeonyesha mapendo kwako hata katika muda ule ambapo ulijionyesha wazi kuwa si mtu mwaminifu wala rafiki wa kutegemewa.

Kwa sababu hiyo, sehemu ya kwanza hapa ni kuhusu mwaliko au mwito wa upendo kama jinsi ambavyo yawezekana tulishuhudia katika kuhusiana na tumpendaye. Kila mmoja wetu anaweza pia kuongeza katika tafakari hii uhusiano wake wa sasa na ampendaye. “Upendo” huu usiwe wa kiubunifu au tungo za kimawazo—uchukue yote yanayotukabili tunaopendana. Pengine mimi na mwenzangu wa ndoa tulikaribisha mambo yaliyoleta chuki na kuharisha ndoa yetu—sasa tumeamua kufanya mabadiliko makubwa katika jinsi tunavyoishi maisha yetu ili kusalimisha uhusiano wetu. Kama ulivyo, uhusiano wa mapendo ya kweli sharti uwe na vipengele viwili: kutokuwa rahisi, ila wapendanao daima watakuwa pamoja katika ugumu na uzito wake. Furaha ya wapendanao ni katika kuchukua ugumu na uzito wa mapendo yao kwa umoja.

Na sasa tunapotafakari mwito wa Yesu, unaweza kutugusa zaidi katika mtazamo wa mwito wa kimapendo katika mahusiano, ila hapa mahusiano ni baina yetu na Yesu Kristu. Masomo kadhaa tuliyokuwa nayo majuma kadhaa yaliyopita yana vipengele vya mwito kama huu. Baada ya Yesu kuhubiri akiwa amemeketi katika mashua ya Petro (Luka 5:1-11), alimkaribisha Petro katika maji yenye kina kirefu na kumwonyesha uwezo wake wa uvuvi. Ukweli unamwonyesha Petro jinsi gani asivyostahili hata kuwa karibu na Yesu. Ndipo hapa Yesu anapotoa mwito wake wa mapendo kwa Petro. Anamweleza Petro kuwa akipenda, wanaweza kufanya kazi pamoja. Tunamwona pia yule mwanamke, wakati Simoni Mfarisayo alipomwalika Yesu nyumbani kwake kupata chakula cha jioni (Luka 7:36-50)—yule mwanamke alionyesha wazi jinsi mapendo yalivyo na nguvu ya kutugusa na kutuletea mabadiliko chanya: wokovu, msamaha, uzima, uhai nk. Yesu anamwambia mwenyeji wake kwamba tofauti katika ya kupenda nusunusu na kuwa na mapendo ya kweli inahusiana na kiasi cha msamaha wa dhambi tunaopokea. Mwanamke yule, kwa kutambua udhambi wake ulivyokuwa mkubwa, kapata uwezo mkubwa zaidi wa wa kupenda.

Kwa kiasi kikubwa, kumfuasa Yesu ni mwitikio kutoka ndani moyoni. Ni mwitikio wa kiroho. Sote tunaweza kukiri kuwa mara nyingi katika siku zilizopita tumekuwa na shughuli na harakati nyingi sana hata kushindwa kuusikia mwito wowote—hii ikiwa na maana kuwa hatuwezi kuuitikia mwito ambao hata hatukuusikia. Sasa tukiwa watu tulioguswa na upendo wa Yesu unaoponya na kusamehe; sasa tukiwa na mioyo yenye kiu na hamu kuu ya kuonyesha shukrani zetu, tunaweza kusikia wazi sauti ya Kristu mponyaji mwenye huruma. Sauti hii inatuita na kutualika kupenda kama yeye alivyotupenda.

Bila kufanya pupa kuuitikia mwito, juma hili tulifanye liwe la kusikiliza. Nia yetu ni kuguswa kwa undani kabisa na mwaliko huu—kupata kushuhudia waziwazi kile ambacho mwito huu unafanya katika mioyo yetu. Labda tungependa kutumia kalamu na karatasi kutunza kumbukumbu ya mwaliko huu tuupatao kutoka kwa Bwana. Labda tungependa pia kushuhudia kwa wengine neema tulizopekea kwa kuziandika katika mtandao huu, ili kwamba wote wafanyao mafungo haya waweze kufaidika na ushuhuda wako, nawe uweze kufaidika kwa shuhuda za wenzako.

Kama ukipenda, juma hili ni muafaka kabisa kutumia mwili wako katika kusali. Waweza kuketika katika kiti kwa utulivu na unyamavu na kuisikiliza sauti mwito wa mapendo ndani kabisa ya moyo wako. Waweza kuweka wazi mikono au kuinyanyua juu kama ishara ya kupokea mwito huu. Waweza pia kufanya ishara zozote kwa kutumia viungo vya mwili wako kama ishara ya kuwa wazi kupokea mwito wa Kristu na kumshukuru kwa kukutendea mambo haya makuu. Yote haya ni sala ya nguvu ya kutumia mwili kuonyesha utayari wako kupokea mwito wake, na kutoa shukrani ya dhati kwa zawadi hii ya kimungu.

Sote daima tujikumbushe kuwa tupo safarini. Katika safari hii ya maisha, tunakua kiuhusiano na Mungu kila siku, kuanzia pale tunapoamka hadi pale tena tunaporudi kitandani tunapofunga siku. Katika safari hii ya maisha, katika usiri wa mioyo yetu, utambuzi wa jinsi tunavyopendwa na Mmoja unaongezeka, na uhusiano wetu na Mmoja huyu unakua hasa tunapogundua kuwa hata pale tunapokosa uaminifu kwake, daima hatuachi bali anatuonyesha mapendo zaidi kwa huruma na msamaha.

Kwa Ajili ya Safari:
Kumjua Yesu Kristu


Sala zetu kwa majuma matatu yaliyopita zimekuwa juu ya upendo wa Mungu uletao wokovu. Tumekuwa vilevile tukijitahidi kumjua hasa ni nani huyu anayetupenda kiasi hicho na kwa kina cha ndani kama hicho, na kwa muda usiokadirika, bila kuchoka wala kukatishwa tamaa!

Upokeapo barua au ujumbe ambapo autumaye hakuweka jina wala sahihi yoyote kujitambulisha, hakika waweza kuidharaulia mbali na hakuna atakayekushangaa ukiichukulia kama mzaha. Lakini, kama ukipokea kifurushi kizuri chenye zawadi nzuri na ya thamani, na ndani yake kuna kadi ionyeshayo herufi za mwanzo za majina ya mtumaji, hakika utavutiwa zaidi kutaka kumjua mfadhili huyu. Hii inaonyesha wazi kuwa ndani kabisa ya mioyo yetu kuna “kitu” kinachotuvutia kutaka kumjua yeyote atuonyeshaye mapendo, alama au ishara yoyote ya mapendo. Si ajabu kujikuta tukijiuliza: “ni nani huyu, na kwa nini anitendee mema kiasi hicho? “Anapenda mimi nimrudishie nini, au nimjibu vipi?” Haya ni maswali ambayo yanafunga sehemu ya kwanza ya Mazoezi ya Kiroho, na kufungua sehemu ya pili.

Hakika tumepokea kikamilifu zawadi ya kuumbwa kwetu, na tena kuumbwa upya au kufanywa viumbe wapya katika upendo wa Yesu Kristu, upendo uletao wokovu. Ni nani Mungu huyu aliyetupenda hata akajifanya mwanadamu akawa Mungu-Nasi? Ili aweze kutushirikisha mwito uletao uzima? Ni Mungu wa namna gani huyu aliyejishusha kuwa katika mwili, hali na mazingira ya kiumbe wake? Anakuja kwetu si katika hali ya usiri, si katika kuficha jina lake hata kidogo, bali akituambia wazi wazi Jina lake na kututambulisha waziwazi.

Sala yetu na iwe kulitafakari Jina lake analotumia kujitambulisha kwetu, tuombe tuzidi kumjua zaidi Yeye mwenyewe kama zawadi kubwa kupita zote tulizopokea, na zawadi nyingine nyingi sana alizotupa na anazozidi kutupa kila siku. Kuwa macho, kuwa mwangalifu kwani kila mmoja wetu wakati mmoja au mwingine huwa anapinga mafundisho ya Huyu anayetupenda sana. Huwa tunapinga miongozo yake na njia za ajabu azitumiazo kutualika katika upendo wake.

Pamoja na wake kwa waume wengine tulioingia ndani kabisa ya upendo wake, ni ajabu kuwa mara nyingi tunajikuta tukijiwa na maswali na woga, tunajikuta tukisitasita na tukijiwekea udhuru usio kweli na kukosa uaminifu. Cha ajabu zaidi ni kuwa huku kumkana atupendaye hatimaye huwa sehemu muhimu katika “kusalimu amri” na kujikabidhi kabisa katika pendo lake. Labda sasa tungependa kujua ni kipi tunachoalikwa kutenda. Juma hili tunaalikwa tusali tukitumia yale yaliyotujia au yanayotujia moyoni kabla hatujasalimisha kikamilifu kwa Kristu:

• maswali tuliyoshindwa kuyajibu: kwa mfano kwa nini Huyu atupende kiasi hiki?

• kusitasita kwetu kusonga mbele tukijiashiria hatari katika hatua ya kujisalimisha na kupoteza “umimi” wetu,

• woga tunaokuwa nao moyoni kwa kutokujua kwa akili zetu hatima ya kufuasa mwaliko wa upendo wa Kristu.

Haya yote yametusibu katika akili na pia katika moyo, na ni kawaida kwetu kama wanadamu. Ni katika hali kama hizi za maswali, woga na kusitasita ndipo Kristu alipokutana na Mtume Petro, Nikodemo, watakatifu wengi na wengi zaidi waliosikia mwito wake. Tusali tukitumia ukweli wa maisha yetu, na mahusiano yetu na Kristu bila kuogopa sehemu zile tulipoonyesha udhaifu. Tukumbuke kwamba yeye hutukuta katika “ukweli na uhalisi” wa maisha yetu. Hivi basi sharti tujue ni nini kinachotuogopesha au kututisha, ni nini kinachotusumbua moyoni au akilini nk.. na ni katika utambuzi wa ukweli huu ndipo yeye anaweza kutujia na kuwa jibu, ukweli mpya na maisha mapya. Ni hapa ndipo anapokuja na kuwa Mungu-nasi, akitufunulia mapana na marefu ya upendo wake yasiyofikirika, kuelezeka, wala kupimika. Taratibu na tumshuhudie Huyu mpendwa wetu akituondolea mbali misukosuko na mashaka tuliyonayo, moja baada ya lingine.

Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...

Bwana Wangu Mpendwa,

Mengi yameugusa moyo wangu kwa hali ya pekee katika juma hili la mafungo. Nimepata taswira mpya kabisa ya jinsi ninavyotenda na kuzungumza kulingana na mengi yatendekayo moyoni mwangu. Nimegundua jinsi gani ambavyo huniachi katika umaskini wangu wa kutokukujua, kukukimbia na hata kukuasi; na kuona jinsi utumiavyo haya yote kuonyesha jinsi gani unavyonipenda mimi. Nimegundua kuwa sauti yako inialikayo kuhusiana nawe Muumba wangu katika mapendo daima haififii hata pale ninapofunga au kufungwa masikio yangu ya kiroho na mambo ya kidunia.

Ninaguswa sana moyoni ninaposoma mazungumzo ya mtungo katika mwazo wa Mwongozo wa juma hili juu ya Rafiki anayerudi karika nchi ambayo nawaza kuifananisha na “Shimo la Kifo”. Jinsi anavyoniambia kuwa angependa kurudi huko kwenye “Shimo la Kifo” kusaidia kuokoa watu, na ananisihi niambatane naye. Itakuwaje ikiwa kweli mtu nimpendaye sana ndiye kweli anayerudi nyumbani kutoka katika nchi kama hiyo ya kutisha na kunipa mwaliko kama huo huo? Je nitaambatana naye? Bila shaka nitaambatana naye. “Mradi” huu utakuwa na maana sana kwetu na jinsi tutakavyoishi tukipendana katika nchi hiyo yenye shida tukisaidiana kusaidia wengine. Hakika upendo watu utakuwa na mguso wa ajabu, pale tutakapojaribiwa na mazito ya huko, na pia kufanya kazi bega kwa bega kama wapendanao kuonyesha upendo kwa wengine.

Je, Bwana mwaliko wako ni kama huu? Je ungependa nitafakari mwaliko kutoka kwako kwenda sehemu ambayo sijawahi kufika? Labda ni sehemu mpya kabisa, ila wakati huo huo ni hapa hapa nyumbani! Ila ni tofauti, nami najikuta ni mtu tofauti! Ila je, wewe Bwana wangu Mpendwa utakuwa nami katika yote? Kama nikitishika, utakuwa hapo kunipa motisha na kunirudishia tumaini? Nasikia sauti yako ukiniahidi kuwa si tu utakuwa nami, bali utakuwa ndani yangu, na kuwa katika wakati huu wote upendo baina yangu na wewe utakuwa ukikua na kuongezeka.

Katika majuma yaliyopita, nimekuwa nikishangazwa na kuongezeka kwa kina cha mapendo kati yangu mimi na wewe, Yesu wangu. Nahisi uwepo wako daima ninapokuwa katika sala, na wakati mwingine hata nashtuka katikati ya sala nikijiuliza iwapo naota ndoto. Ni kama vile napagawa ninapotafakari mapendo makubwa kutoka kwako, mimi ambaye siyastahili hata kidogo. Hata hivyo katika ukimya wa sala, najua bayana mapendo yako ni halisi, si bandia. Najua kuwa unanipa zawadi ya upendo wangu kuongezeka kina ndani ya moyo wako mtakatifu. Hii inanifanya daima niwe na kiu ya kuwa nawe.

Yesu wangu, wacha nikae kimya na kutulia katika mwito wako huu. Nahisi unaniitia kitu fulani, ila sina hakika ni kipi hasa. Nahisi utupu fulani ndani yangu ambao najua ni wewe tu uwezaye kuujaza. Kwa sababu hii natamani sana kusogea karibu nawe.

Kuwa nami Bwana ninapotafakari mwaliko na mwito wako kwangu. Kuwa nami wakati wote. Jaza nafasi tupu iliyo ndani yangu. Nipe uwezo wa kulihisi pendo lako daima. Asante sana kwa kwa mwaliko huu unaonitumia. Tafadhani nijalie uvumilivu wa kushinda na mwito wako juma hili lote—kusali nao na kuwa mvumilivu hata ninaposhawishika kutenda kinyume cha mwito huu. Bwana nifundishe kuwa mvumilivu katika kupenda kama wewe unavyonivumilia daima.

Maandiko Matakatifu
Luka 4:14-20
Marko 1:16-20
Luka 5:27-31
Luka 9:57-62
Luka 12:32-34

 

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO