JUMA LA KUMI NA MOJA Katika Juma hili tuitikie kwa moyo mwaliko wa mapendo
tulioupata. Kupitia katika zoezi la juma lililopita, tumeweza kujua kuwa sifa
ya mwitikio wetu inategemea kina cha upendo wetu kwa yule atualikaye. Pale mpendwa wetu anapotuuliza kuhusu
mwitikio wetu kwa mwaliko wake, jibu ni “Ndiyo”. Hata pale tunapojua kuwa mwitikio huu
unaendana na gharama binafsi kubwa sana, bado mwitikio wetu haubadiliki kwa kuwa
tunajua upendo daima unatuweka katika ukaribu na umoja wa wapendanao—nasi
tunataka daima kuwa na yule
tumpendaye.
Kwa mioyo yetu, juma hili tutakuwa tukiitikia mwaliko wa
Yesu Kristu. Tunaweza kwa muda mfupi
kufanya marudio ya mwongozo wa zoezi la juma lililopita ili kujikumbusha mwito
huu na kuamsha hisia za rohoni tulizopata. Tuliguswa sana na mwaliko wa kuungana naye katika mradi wa kuwaleta
wengi katika kuwakaribisha wengi katika utawala wa Mungu. Tukiangalia kwa makini, tutaona kuwa mwito
huu unatofautiana kidogo kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kuwa tuna vipaji,
historia na malezi tofauti. Mioyoni, tumezawadiwa
neema tofauti baina ya mtu mmoja na mwingine. Hali ya maisha tuliyopitia; namna mbalimbali za kheri na shari, furaha
na huzuni, mahangaiko na starehe; vimetujengea kila mmoja namna tofauti na ya
kipekee ya kuhurumia na kuwa na wengine katika magumu yanayowasibu. Kila mmoja wetu anapata mwaliko kwa namna
yake ya pekee, kulingana na umri na uwezo tuliojaliwa hasa wa ushawishi kwa
wengine. Hivi basi tunapenda kusikia
mwaliko wa Kristu ukielekezwa kwetu binafsi, kama vile tukialikwa kwa kutajwa
majina na yule atupendaye. Hata hivyo,
kwetu sote, kuna usawa katika mwaliko na nafasi tunayopewa ya kuuitia. Bila shaka mwitikio wetu ni “Ndiyo”. Hakuna furaha ya kweli maishani ambayo
haihusishi kumfuasa Yesu Kristu. Swali
la juma hili ni kina au upevu wa mwitikio wetu—jinsi ambavyo
tunaweza kuuitikia kikamilifu mwito wa Kristu. Hatujui kwa uhakika bayana “Ndiyo” yetu mwaka huu itakuwa namna ipi na
itajumuisha yapi. Kadhalika hatuweze
kuwa na habari kamili za “Ndiyo” yetu mwaka ujayo, au miaka kumi kutoka leo.
Hivyo basi, tunaweza kufanya mwitikio ambao bado unaacha mlango wazi—tunajitoa na kukubali
kikamilifu lolote lile ambalo ni
kumfuasa Kristu. Tunaacha mlango wazi ili kwamba lolote lile limpendezalo Kristu lipate nafasi maishani mwetu. Hata
hivyo, kwa neema ulizopata majuma
yaliyopita kutokana na kupendwa na Yesu Kristu, unaweza kuwa umepata shauku
halisi ya kupinga lolote ndani yetu ambalo ni la kilimwengu, bure au lililojawa
na ubinafsi.
Tunaweza kuwa na shauku ya
kujitoa kikamilifu kwa Yesu kwa ubora wa hali ya juu kabisa; na kuwa ishara ya
wazi kuwa mwitikio wetu sio wa kuweka viwango, mipaka au vizuizi vya mwisho wa majitoleo
yetu. Ikiwa Bwana wetu atatuchagua,
tutaonyesha siyo tu utayari wetu wa
kuwa na Kristu katika umaskini wake na kuchukua kwake hali ya kibinadamu, bali
pia hamu yetu ya kweli ya kuzisalimisha
nafsi zetu tukifuata mfano wake.
Acha picha ya mwalimu na
mwanafunzi uliyopewa katika ukurasa huu iwakilishe mwitikio wetu wa kuwa na
Yesu katika kuwa na wengine wanaohitaji msaada wetu. Tumia misaada mingine unayopewa katika juma
hili hasa katika kipengele: “Kwa Maneno Haya au Mengine Yanayofanana
Nayo...” Jaribu kuchangia na wenzako
neema unazopata juma hili.
Katika juma hili acha maneno
na namna zingine za kuelezea mwitikio wako kwa mwito wa Yesu zibubujike bila
kipingamizi kutoka moyoni mwako. Una
majuma mengi zaidi mbele yako ya kukua katika shauku ya kupenda zaidi na kuendelea
kuchunguza kina cha majitoleo yetu. Juma
hili tujaribu kutafakari mwitikio wetu kwa kadiri tulivyoneemeshwa kujitolea.
Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili Kumsaidia mtu kuitikia mwaliko binafsi wa mapendo kwa
kiasi fulani ni kama kumsaidia mtu kuchagua zawadi ya kusherehekea siku ya
kuzaliwa ya ampendaye, au ya kumbukumbu ya miaka fulani baada ya tukio muhimu
kama vile ndoa, upadrisho nk. Maswali
yanayojitokeza yanaweza kuwa haya: uhusiano wake na mtu huyu ni wa karibu kiasi
gani? Kiasi gani cha fedha yupo tayari
kutumia? Angependa zawadi hii ifikishe
ujumbe gani? Na wewe pia katika umbali
uliokwenda katika mafungo haya, maswali yanayotegemewa kukujia ni kama haya:
·
Ni kwa undani kiasi gani nimeguswa na na upendo na huruma
ya Mungu?
·
Ni kiasi gani ninajawa na moyo wa kutaka kuonyesha
shukrani?
·
Ni kwa undani kiasi gani nilisikia mwito na mwaliko wa
Yesu?
·
Ni mwitikio gani “unaumbika” moyoni mwangu?
Ushauri wa kwanza kwa juma
hili ni kuanza na mwitikio ulio rahisi kuliko yote. Sema ndiyo. Jaribu kufanya zoezi la kusema “ndiyo” kwa
sauti. Je, una unajisikia vipi
unapoisema ndiyo yako kwa namna
tofauti tofauti (kama vile: sawa, naam! Enhee!, nipo..., nk) ? Unaiihisi namna mbalimbali za kiwango cha
ukweli wa mwitikio wako?
Zoezi linalofuata laweza kuwa
katika hali maalum au inayoendana zaidi na ndiyo yako. Naweza kusema ndiyo na kuwa na maana kuwa kumfuasa kwangu Yesu katika kutekeleza
kazi maalum aliyotumwa na Mungu Baba ni kuwa mwaminifu katika lolote linijialo leo.
Naweza kuhisi kuwa kuna aina maalumu ya uaminifu ambayo
imeambatanishwa na mwaliko wa Kristu kwangu; kwa mfano uaminifu katika maagano
ya matakatifu ya ndoa. Hivyo basi
itabidi ndiyo yangu iwe mahususi: “Ndiyo, nitakuwa nawe katika uzito wote wa uaminifu wa kumpenda mwenzangu wa ndoa” au “...katika kuwapenda watoto wangu”. Kwa wengine, kutokana na umaalumu wa mialiko
yao, miitikio yao inaweza kuwa: uaminifu katika kupokea na kukubali changamoto
zote za kazini, ...msamaha kwa ndugu au
jirani nk. Wakati mwingine mwitikio waweza kuwa katika hali ya kubadili hali au
tabia ambayo inapingana na mwito wetu maalum.
Zaidi, naweza kujikuta
nikialikwa kwenda sehemu ambapo niliusikia mwito, lakini sikuuitikia. Naweza pia kuifanya ndiyo yangu ibaki “mlango waz”i
zaidi, yaani kutokuwa na umaalumu wowote isipokuwa kumfuasa Kristu; “Ndiyo, nataka kuwa nawe katika hali ya
kupenda kama wewe, na nitaufungua moyo wangu wazi kabisa kutoa msaada kwa wowote
wanaouhitaji, hususan maskini.” Vilevile
naweza kuweka na kuitekeleza dhamiri ya kujihusisha zaidi katika mwaliko wa kulitumikia
Kanisa la Kristu.
Kunaweza kuwa hamu au mvuto
wa pekee unaojengeke moyoni mwangu wa kuitikia upendo wa Yesu ambao siku baada
ya siku unaongezeka katika kujibainisha moyoni mwangu, hadi kufikia hali ambayo
moyo wangu unaanza kushabihiana na wa Kristu. Naweza kujaribu kutumia maneno ya mtu aliye katika mahaba na Kristu, yaliyo na mguso wa pekee ndani kabisa
moyoni. Naweza pia kujaribu kujiweka
karibu kabisa na Kristu ili kushirikishwa unyenyekevu wake alipojishusha na
kuwa mwanadamu katika hali na wakati wa umaskini wa kila namna, na kuacha nikuguswe
na unyenyekevu huu hata kujihisi nashiriki hali yake. Kama wapendanao watendavyo, naweza kutamani
kuuweka moyo wangu ndani ya wake mtakatifu. Naweza kufanya mazoezi ya kusema kwa sauti, au kwa kuandika katika
daftari huku kukua kwa shauku yangu ya kumjua Yesu Kristu na kuingia katika
mahangaiko na umasikini na kujisalimisha kunakoujaza Moyo wa Yule Ninayempenda. Hapa, ndiyo na kiu yangu ya kuwa karibu na Kristu
vinaunganika au kufanya makutano.
Katika majuma yafuatayo,
tutatafakari yafuatayo:
·
hamu au kiu ya kuukua katika kumjua Yesu,
·
kukua katika upendo wa karibu zaidi na Yesu, na
·
kuwa pamoja katika kumtumikia Yesu.
Katika juma hili tuna uhuru wa kuacha ufahamu wa kila
mmoja wetu kwenda sehemu zozote ambazo “mpenda” mwenye shukrani anaweza
kuzichukua kama njia ya kusema ndiyo kwa mwito wa “mpendwa” wake.
Kama tufanyavyo kila juma,
tuache neema tunazosaka zidumu katika ufahamu wetu tangu wakati tuamkapo,
tukiwa kazini au katika shughuli zingine za siku, hadi wakati tunapojiandaa
kulala. Naweza kujizoeza kuvuta pumzi
taratibu, hadi kunijaza kabisa na
kupumu taratibu huku nikipitia jambo moja hadi jingine, wakati nikijianda
kwenda kazini. Pumzi hiyo ya taratibu ila ipenyayo ndani kabisa, yaweza kuwa ndiyo yangu kutoka ndani kabisa moyoni: Kuvuta pumzi, napokea mwaliko na kuitoa pumzi, nasema ndiyo. Fanya mazoezi ya kufanya mwitikio wako yakujaze
au kukuzingira wewe mzima, mipango, dhamira, mategemeo, hisia n.k. za kila siku. Vilevile, hisi nguvu ambayo inaweza kutokana
na kuongezeka kwa hali ya kupenda. Katika kadi nyingi za
mwaliko kuna kipengele kisemacho: “Majibu kwa Wasiofika...” kikiwa na maana
kuwa iwapo una udhuru wa kutokuweza kuitikia mwaliko, basi umwarifu
aliyekualika au wakala wake ambaye kawaida anuani yake na namba ya simu
vimeambatanishwa. Tupokeapo mwaliko kama
huo, kwanza tunachunguza iwapo tunao muda wa kuhudhuria mwaliko huo na iwapo
tuko tayari kwenda tunapoalikwa. Mara
nyingine katika mialiko fulani hakuna chochote cha kujiuliza: “Nitaweezaje hata kufikiria jinsi ambavyo naweza
kuacha kuitikia mwaliko huu!”
Kipengele cha kuomba majibu
kama kile cha “Majibu kwa Wasiofika...” kipo katika hali-fiche katika zawadi
nyingi na sauti nyingi ambaza Mungu huzitumia kutuita. Kuna namna mbili ya kuitikia mwaliko
unapofikishwa kwetu. Ya kwanza ni kutoa
jibu baada ya kuwaza; kuangalia faida na muda, hasara na gharama; kuchanganua
maana na uzito hasa ya mwaliko wenyewe na kiini chake; kuchunguza matokeo
yakinifu ya kutokuhudhuria na ya kuhudhuria n.k. Namna ya pili ya kuitikia mwaliko inatokana
na hisia za ndani na uamuzi hufanyika mara, bila kuwaza wala kuwazua.
Mara moja kila mwaka, Kanisa
Katoliki husherehekea sikukuu ya Yesu Kristu Mfalme. Kristu anatujia kama mfalme-mtumishi na vilevile kama mfalme-mwalikaji—huwaalika watu wote katika utumishi kwa wote
anaowaalika kwake, yaani “ulimwengu mzima”. Tunakaribishwa na Mt. Inyasi kutafakari namna nyingi ambazo tayari zimetumika
na Kristu katika maisha yetu kutuita kuingia ndani zaidi ya Ufalme wake. Katika kutuumba, Mungu katujaza zawadi nyingi
na talanta za kila namna. Mwito wa
Mfalme katika Mazoezi ya Kiroho unatusihi tumwitikie Mfalme kwa kutumia zawadi
tulizopewa katika kuumbwa kwetu na zilizoendelea kuongezeka katika maisha
yetu. Kristu aliwaalika wavuvi wa samaki
kuwa wavuvi wa roho: vilevile anatualika
kila mmoja wetu kuuitikia mwito wake kufuatana jinsi alivyo pamoja na vipawa
alivyojaliwa. Anasema “ nakualika wewe
kufanya jambo fulani kwa kuwa nimekujalia tayari karama hii na talanta ile ya
kutenda jambo hili ninalokuitia.” Mwito
wa Kristu basi unatuthibitishia kuwa ni yeye aliyetupa tulivyonavyo, ni baraka
kwa kutuonyesha jinsi alivyotubariki na jinsi ya kuzitumia baraka hizo; na ni
zawadi kwa kutuonyesha matumizi ya faida na maana ya juu kabisa ya zawadi
alizotujalia Muumba wetu.
Sali ukimsikiliza Kristu
akikuita. Acha maneno yake yaingie sana
akilini na moyoni mwako hata uwe kama unayesikiliza wimbo au muziki mzuri sasa
wenye maneno kama haya: “Njoo kwangu...
Nifuate. “Nitendalo, na liwe tendo
lako... “Nitamkalo, na liwe Neno lako... “Nikilacho, na kiwe chakula chako... Nikinywacho,
kikate kiu yako... Nilalapo, na pawe malazi yako... chukua mkono wangu, niangalie
machoni na uniambie utanifuata daima... nipe moyo wako, niuweke Moyoni
mwangu... kwa kuwa Moyo wangu una nafasi kubwa kwa ajili yako, na Nyumba ya
Baba Yangu ina vyumba vingi saaana.”
Yesu anatusihi tumfuase, ila
kumfuasa huku hakuna maana ya kufuata “njia” tu yake yeye akiwa hayupo. Kumfuasa Yesu ni kuambatana naye na
kushirikiana naye katika yote: atakuwa nasi na kutenda kazi pamoja nasi, atatenda
mengi kwa kupitia vipawa na uwezo wetu, na hatatuomba kutenda lolote lile
ambalo yeye mwenyewe hayuko tayari kulitenda. Anatukaribisha katika ushindi wake, ila pia katika hali yake ya
kibinadamu kabisa ya kuupata ushindi huo.
Tunaombwa kutafakari kuhusu
yale yanayotugharimu katika kumfuasa Kristu. Baada ya kufanya hivyo, tujaribu kusikiliza kutoka ndani kabisa mioyoni
mwetu, sauti ya Mungu ikituita kwa upole kujitolea sisi wenyewe na zawadi zote
alizotupa Mungu—vyote viwe zana ya kumfuasa.
Ni kweli tunaweza kuwa na nia na shauku kuu, lakini ukweli wa kibinadamu ni kuwa kwa nguvu zetu wenyewe, hatuwezi kuyatoa maisha yetu kikamilifu kwa Mungu bila kurudi nyuma. Petro, wa kwanza kati ya wavuvi wakubwa wa watu, aliacha yote ili kumfuata Yesu, na kwa miaka mitatu tunamwona akisitasita na kuonyesha woga. Katika Injili tunamwona Petro akimsihi Yesu asiende Yerusalemu kwani kulikuwa mahali pa hatari wakati huo, akitoa ahadi ya kutokumkimbia Yesu lakini akimkimbia alipowekwa nguvuni, akimkana mara tatu katika njia ya msalaba, na akiwashauri wenzake kwenda kuvua samaki, baada ya ufufuko wa Kristu nk. Ni kweli bado alimpenda Yesu, na hatusiti kusema kuwa alipenda kutoa maisha yake yote kuitikia mwito wa Yesu, lakini bado alijikuta na udhaifu wa kibinadamu, udhaifu ambao ni pengo linaloweza kujazwa na Mungu pekee. Kila mmoja wetu ana wakati ambao anatamani kuyaweka mikononi mwa Kristu maisha yake na yote aliyonayo. Tusisite, na wala tusione ni kidogo kile tunachomtolea—tujue kuwa yeye atapokea sehemu yoyote ya mioyo yetu, talanta zetu, na maisha yetu ambayo tunaweza na tuko tayari kumtolea.
Bwana Mpendwa,
Nahisi mwaliko wako ndani
kabisa ya roho yangu. Katika ukimya,
natulia nikijawa na shauku kuu ya kuitikia mwito ambao haujajibiwa maishani
mwangu, na naona waziwazi kuwa kwenye mwaliko wako unaoutoa kwa kwa moyo mnyenyekevu
ndipo pekee penye jibu.
Nakuhisi ukiniita na
kunialika—ukijitolea kujaza sehemu tupu ndani yangu inaosababishwa na kuipuuza shauku
ya kuitikia mwito wako. Utupu huu
umejificha ndani yangu, mahali ambapo ni wewe tu, Mungu wangu, ndiye unayeweza
kupafikia na kustahili kufanya makao yako, mahali pa kuwa nami mpendwa
wako. Inakuwa vipi kwamba mwaliko huu
unauelekeza kwa nafsi yangu kiasi hicho, hata ukinitaja mimi kwa jina na
kunijia katika hali isiyopingana na yote yangu yaliyo mazuri—elimu yangu, umri
wangu, uwezo wangu, ujuzi wangu, mahali ninapoishi...? Tazama sina jibu jingine kwako ila
“ndiyo”. Nawezaje kuwa na jibu tofauti
na hilo, baada ya kushuhudia ukarimu wako, uaminifu wako kwangu na upendo
mkubwa ulionionyesha katika maisha yangu?
Sijui ndiyo yangu itanipeleka wapi. Mwaliko wako hauna shuruti wala vitisho vyovyote, na sina woga
wowote. Unanisihi, kwa kiasi fulani,
kubadili mtazamo wa maisha yangu ili kwamba niwe kwa kiasi kikubwa kama
ulivyoniumba, na siyo mimi ninayeiga hali za wengine nikionea aibu fulani
uumbaji wako. Mimi ni mwema nilivyo na unanipenda katika hali njema uliyoniumbia. Kwa kiasi fulani, nakiri kuwa na woga
ninapoanza kuwaza wapi hasa haya yote yananiongoza na ni kwa kiasi gani
yanaweza kubadili maisha yangu. Hata hivyo,
kwa namna fulani, najua kama nikiitikia mwito wako nitakuwa jinsi ulivyotaka
mimi niwe wakati uliponiumba. Nitakuwa
mimi hasa, nafsi yangu ikinionyesha mimi
halisi bila ubandia wowote.
Naanza kuelewa, Bwana Wangu,
kubwa si matokeo ya ndiyo yangu tu ambayo
ni muhimu. Muhimu zaidi ni ndiyo yangu. Ni kiu au shauku ya kuwa nawe ndani yangu ili
kukidhi hamu ya kutaka kukufuasa, kutuliza njaa ya kukutumikia wewe katika hali
yoyote utakayonionyesha.
Nitamani kuwa na shauku ya
kweli ya kujisalimisha kwako mimi mzima na yote yaliyo yangu. Nisadie Bwana Wangu, kutokurudi nyuma katika ndiyo yangu. Nipe nafasi niung’ang’anie mkono wako, na
kusonga mbele nawe bila woga.
Nasema asante kwa yote
uliyonijalia. Nasema ndiyo kwa yote
utakayonijalia.
Ndiyo, Bwana wangu. Niite, mwitikio wangu ni ndiyo Bwana, mimi hapa niko tayari...
Ndiyo, NDIYO! Milele Ndiyo!
Amina.
Maandiko Matakatifu
Isaya 6:1-8
Zaburi 116
Luka 10:1-9; 17-21
Yohana 21:15-19
|
MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO