JUMA LA KUMI NA MBILI
Huruma ya Mungu—Mchipuko wa Utume wa Kristu
Mwongozo: Kuwa na Kristu Katika Utume Wake

Tumeuitikia mwaliko wa Yesu mpendwa wetu. Kwa kiwango fulani, tumeashiria utayari wetu wa kushirikiana na Yesu katika kazi aliyotumwa kuifanya na Mungu Baba hapa duniani.  Ni pendo linaloendelea kukua ndani yetu, kati yetu na Yesu, na tunaliacha liendelee kukua—tunaacha uhusiano wa kushirikiana na Kristu uendelee kujengeka.

Tunapozidi kukomaa katika kupenda hasa pale anayehusika ni aliyetutendea mengi mazuri, tunakuwa na shauku kubwa sana ya kuwa na yule tunayempenda, na pia kujua mengi iwezekanavyo kumhusu huyo tumpendaye. La kushangaza sana katika kupenda, ni kuwa kila wakati inaonekana kuwa hatuwezi kujua yote tunayotaka kumhusu tumpendaye. Kiu yetu ya kutaka kumjua tunayempenda haitoshelezwi hadi mwisho.

Katika juma hili na majuma yanayofuata, nia yetu moja ni kujua mengi iwezekanavyo yanayomhusu Yesu Kristu.  Bila shaka tunatambua kujua huku tunakokutafuta si kwa akili zetu tu; bali kwa kiasi kikubwa ni ya utambuzi wa ndani unaozidi kutujengea ukaribu wa pekee na yule tumpendaye.  Ukaribu huu unaendana na shauku ya kutaka kuwa naye wakati wote katika utume wake.  Hivyo basi tunaweza kusema nia yetu ni kumjua Kristu kwa ukamilifu zaidi, ili tuweze kumpenda kwa undani zaidi, na upendo huu wa ndani zaidi utuongezee uwezo wa kumfuasa kwa karibu zaidi.

Katika siku za mwanzo za mafungo haya, tulijaribu kuangalia historia ya maisha yetu kwa njia ya kujitafakari tukitazama kitabu cha picha cha maisha yetu—kitabu chenye picha nyingi, zijulikanazo na wengine na zingine tuzijuazo sisi wenyewe tu, picha zingine tuzioneazo aibu na zingine zitupazo majigambo ya moyoni, zingine zenye kutupa simanzi na nyingine zenye kutukumbusha furaha zilizopita tukiwa na wapendwa wetu...  Sasa tunamwomba Yesu atuonyeshe Kitabu Chake cha Picha (“Photo Album”).  Katika shauku yetu ya kujua mengi yanayomhusu, tunamwomba Yesu Kristu asitufiche chochote—atuambie hadithi au wasifu wote wa maisha yake ili kwamba tuweze kumpenda zaidi, yeye tunayetamani kumjua kwa undani zaidi.  Hakika kuna thamani ya pekee kumjua yule anayetualika kumfuasa katika kutekeleza kazi aliyotumwa na Baba Yake.

Juma hili tunaanzia hapo mwanzoni.  Tunamtafakari Mungu katika umilele wake, yaani hali yake ya kutokuwa na mwanzo wala mwisho.  Tunamtafakari Mungu katika Utatu wake Mtakatifu kama vile akiutazama ulimwengu wetu kutoka juu mbinguni—akitazama matendo na wasifu wa binadamu wote, na kujawa na huruma kiasi cha kumtuma mwanaye Yesu kuja kutukomboa.  Hata sisi tukijaribu kutafakari kitabu cha picha za vita vya dunia na vita vingine vingi, biashara ya utumwa, vifo vitokanavyo na magojwa na njaa, mauaji ya kimbari katika sehemu mbalimbali, athari za UKIMWI, chuki za kidini na kikabila n.k., tunaweza kuona wazi wasifu wa mwanadamu ambao hakika unamgusa sana Mungu atupendaye kiasi cha kutuhurumia sana.   Picha tuliyopewa katika juma hili ni ya Sarayevo, Boznia na Hesgovina ikionyesha uharibifu wa vita kati ya wanadamu.  Tunaweza kuwaza jinsi picha hii inavyomgusa Mungu akiwaona wanadamu aliowaumba kwa sura na mfano wake wakitumia akili, nguvu, uwezo na uhuru wao kumalizana na kulemazana kwa vita.  Tunajua wazi kuwa uamuzi wa Mungu kumtuma Mwanaye ni ukurasa wa utangulizi wa kitabu cha Historia ya Ukombozi Wetu. Na pia unafanya kiini cha sura kadhaa za “kitabu hicho”. Hii ni kwa kuwa uamuzi huu aliuweka katika historia yetu katika hali ambayo hatuwezi kuutenganisha tena na maisha yetu.  Alipanga kutuletea mkombozi, akatuahidi mkombozi, akatuweka katika hali ya kungojea ujio wake, kisha mwanaye Yesu Kristu akazaliwa kati yetu, akaishi nasi, akafa na kufufuka kwa ajili yetu.

Juma hili na tutumie yale tunayopewa kutusaidia kutafakari na kuingia ndani ya fumbo la umwilisho wa Mungu katika Kristu na uamuzi wa Mungu kuukomboa ulimwengu.  Tayari tumekwishaona athari za dhambi na kumuasi Mungu katika maisha yetu—si dhambi na uasi wa wanadamu kwa ujumla wetu tu, bali pia katika uasi na udhambi wetu binafsi.  Sasa tunatafakari mwitikio wa Mungu kwa dhambi ya limwengu—mwitikio huu ni kumtuma kwetu Mwanaye Yesu Kristu.  Sasa na tuanze kwa kuelezea shauku yetu ya kujua atokako ili kwamba tuweze kumpenda kwa undani zaidi, na kuona nafasi yetu katika kazi aliyotumiwa.  Hata hivyo sharti tumwache achague kutualika kujiunga naye.

Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili

Katika maisha ya kila siku, kupata wa kumpenda hakuhitaji msaada wala juhudi nyingi.  Ni kama vile jambo hutokea tu bila juhudi yoyote.  Kwa tafakari ya moja kwa moja, wazungumzao Kiingereza wanasema “kuangukia katika mapenzi”.  Ni kama vile jambo lisilopangwa, ni kwa bahati tu mtu “huanguka”, hivi basi inaonekana kuwa ni jambo lenye urahisi wa kiajali, japokuwa aangukaye aweza kuumia vibaya.  Ni wazi kuwa kuangukia katika mapenzi hakuna kile vipengele muhimu ambavyo kwavyo tunaweza kujifunza lolote la kutusaidia katika kupata kile hasa tunachokitafuta katika majuma yaliyo mbele yetu.  Vilevile, kama sote tujuavyo kutunza uhusiano wa mapendo ya kweli huhusisha kujitolea mhanga ambako hakuwezi kufanyika bila kuwepo kwa uaminifu wa hali ya juu kati ya wapendenao.  Si suala la ajali tu, bali ni suala linalohusisha nia na hisia zetu za ndani sana.

Tujaribu tena kufikiria kuhusu hali ya kuanza kupenda.  Ni nini hasa kinachoanzisha wawili kupendana?  Ni nini tunachokitenda katika hatua za kwanza kabisa tujikutapo tumeanza kumpenda mtu fulani?  Je huanza kwa kile tunachokiita kukutanishwa?  Labda wakati mwingine ni “kukutanishwa” na mtu ambaye ni mgeni kabisa katika maisha yetu.  Kuna kitu fulani ambacho hutokea ndani yetu na tunajikuta katika hali inayogusa na kunyanyua mioyo yetu kumwelekea tuanzaye kumpenda.  Kiini cha hayo yote ni kuvutiwa sana na huyu tuliyekutanishwa naye, na tunagundua hali ya namna fulani ya kutaka kuwa pamoja naye.  Kutokea hapo, kuvutiwa kwetu na yule tunayempenda kunaongezeka na pia hali iliyo ngumu kutawalika ya kutaka kuwa na yule tumpendaye wakati wote huongezeka kwa kiasi kikubwa.  Upendo unaokua hulisha na kukuza shauku ya kukuza muungano—shauku ya kuwa na mpendwa wetu katika hali ya undani wa hali ya juu.  Mwanzoni hili hutokea bila utambuzi wetu, ila kabla muda mrefu sana haujapita, tunapata ufahamu kuwa tupo katika mapendo.  Tunaanza kulifanyia kazi pendo hilo. Tunakuwa na mawazo mengi yanayomhusu tunayempenda, na hata tukiwa tunafanya kazi zetu za kawaida, tunakuwa na ndoto za mchana zinazotuhusu sisi na tumpendaye.  Tunamtembelea au kumpigia simu yule tunayempenda mara nyingi zaidi na kupanga kuwa na muda mwingi zaidi pamoja.  Tunakumbuka mazungumzo yetu yote, na wakati tukiwa hatuko na tunayempenda tunayarudiarudia akilini mwetu—kama vile kucheza tena na tena muziki tunaoupenda.  Mwanzoni tunajikuta tukizungumza na tunayempenda kuhusiana na yote na chochole.  Hakuna lolote linalomhusu tumpendaye linaloweza kuleta mazungumzo yasiyovutia au yenye uchoshi.  Tunapenda kujua yote yanayohusu maisha ya tunayempenda; aliyopitia maishani, jinsi alivyofanya uchaguzi mbalimbali maishani, yale anayopenda na yale asiyopenda na yapi hasa yanamfanya kuwa alivyo.  Tunagundua mengi mapya kumhusu tunayempenda, na katika kila ugunduzi, tunajikuta mwunganiko wetu wa ki-mapendo ukiongezeka.  Tunatafuta njia za kuonyesha mapendo yetu kwa tumpendaye: tunajaribu kutumia maneno mororo, tunatumia matendo yanayojali, na kufanya mengi yanayoonyesha kujitolea ili kumfanya mwenzetu awe mwenye furaha na faraja.  Kila neno tumsemezalo na tendo tumtendealo tunayempenda huchangia katika kukua kwa pendo letu.  Hatusahau daima ishara ya kwanza kabisa aliyotuonyesha kuwa anatupenda.  Kwa kadiri upendo wetu unavyokua, ndivyo hivyo pia kiwango cha wajibu wetu katika pendo hili kinavyoongezeka—najikuta nikitafuta kitu cha kunihakikishia kuwa nimpendaye atukuwa nami katika maisha.  Kwa upande wangu naonyesha kuwa nitawajibika na kujitoea mhanga katika hali yoyote ili pendo letu liendelee.

Kama haya yamepata kukutokea kwa namna yoyote ulipopenda katika maisha yako, au kama yanakumbushia yale yaliyotokea katika kupenda, basi yatakuwa ya msaada mkubwa katika majuma yanayofuata.  Tupo katika mwelekeo wa kuanza kumpenda Yesu.  Tunaweza kujaribu kuhisi hatua ya kwanza ambayo ni kukutanishwa kwetu na Kristu.  Tunaweza kujipa muda wa kushuhudia jinsi shauku yetu ya kuwa na Yesu inavyoongezeka, ikisababisha kujiwa na maswali mengi, ikitufanya tutunge misemo mingi ya kuelezea mapendo yetu kwa Yesu, na kuonyesha dhamira ya kuwa naye pamoja wakati wote.

Huu ni msaada wa kutenda na si wa kufikiri wala si zoezi la kupata elimu ya kutusaidia kuangalia “Kitabu cha Picha cha Yesu”.  Hili ni suala la moyoni.  Kufikia kiwango hiki katika mafungo yetu, tayari tumeunganika na Yesu ndani mioyoni mwetu.  Sasa tuna nia ya kuyapa nafasi mapendo haya yaongezeke kina.

Kurasa za mwanzo za Kitabu cha Picha cha Maisha ya Yesu kinaturudisha “hapo mwanzo”, na kutuweka katika tafakari ya taswira bunifu ya Jumuiya ya Utatu Mtakatifu ikiuangalia ulimwengu wa binadamu kutoka juu mbinguni, na kujawa na huruma moyoni.

Tafakari ya huruma ya Mungu Baba katika kumtuma Yesu Kristu katika ulimwengu wetu na katika maisha yetu inaweza kuwa na mguso wa pekee katika mioyo yetu.  Jinsi tunavyozidi kutafakari, kwa mfano mauaji ya Bosnia au yale ya kimbari ya Rwanda ambayo yanaigusa pia huruma ya Mungu katika Kristu, ndivyo tunavyozidi kumtambua Yesu ni nani.  Ukweli kuwa Yesu yu kwa ajili yetu unashinda upeo wetu wa udhanifu na utambuzi.  Umwilisho wa Yesu hakika washinda elimu yote na uwezo wote wa mwanadamu wa kuelewa.  Yesu Kristu, Mungu kamili anajishusha na kujiweka katika hali duni kiasi hicho!  Hakika hakuna tena sehemu ya maisha yangu ambayo naweza kusema niko peke yangu.

Katika juma hili lote, fanya zoezi la kurudia kusema maneno haya: “Bwana, nisaidie kukujua kikamilifu, ili niweze kukupenda kwa dhati zaidi, ili kwamba niwe nawe kikamilifu zadi.”  Vilevile unaweza kupenda kuimba kila siku wimbo wowote unaotumia maneno haya ya Mt. Inyasi wa Loyola:  “Ee Bwana wangu, mambo matatu nakuomba: kukuona wewe kwa udhahiri zaidi; kukupenda wewe kwa dhati zaidi; na kukufuasa kwa ukaribu zaidi—siku baada ya siku.”

Kabla ya kulala kila siku, naweza kujiwekea muda mfupi wa kujiuliza ni neno gani nadhani linafaa nimwambie Yesu ninayempenda.  Bila shaka muda huu mfupi utakuwa pia muda wa kuburudishwa na furaha na faraja ya ndani inayonijia nilipotambua jinsi pendo langu na kuvutiwa kwangu na Yesu kunavyoongezeka.

Kwa Ajili ya Safari: Ishara za Mungu

Nguvu za kuvutiwa kwa yuke tunayempenda huanza kufanya kazi pale tumpendaye anapotoa ishara kwa maneno au kwa matendo.  Kwa kawaida kila mmoja huvutiwa kutaka kujua maana ya ishara fulani ili aweze kuiitikia inavyostahili.  Watu hutoa ishara mbalimbali kwa kutumia karibu viungo vyote vya miili yao:  mikono, uso, macho, kichwa, miguu na hata mwili mzima wakati mmoja.  Mara nyingi wengi “hujieleza” mengi kuwahusu wao, kile wasichonacho, maisha wanayopendelea, walichonacho, wanachotafuta n.k. kwa kutumia viungo vyao, miondoko na mienendo yao, jinsi wanavyobeba mikoba au vitabu vyao; uchaguzi wao wa mavazi n.k.,--yote haya hutokea bila wao kujua kuwa wanatoa ujumbe fulani kwa ishara zinazoeleweka.  Hivyo basi kwa kadiri tunavyoonekana mbele za watu ndiyo kadiri watu wanavyoweza kutujua.  Kupitia ishara zetu basi tunapata kuvuka kutoka kuwa mgeni na kuwa mwenzetu mbele za watu.  Tunapokaribishwa katika Mazoezi ya Kiroho kutafakari au kutaamuli maisha ya Yesu Kristu, tunasihiwa kumwangalia Mungu akijiingiza katika historia yetu kwa kupitia ishara za Yesu aliye umwilisho-wa-Mungu.

Mungu alifanya majaribio mengi ya kuvutia usikivu na hisia zetu kwa ujumla wake kwa kupitia maagano mbalimbali na wahenga wetu wa Kiyahudi.  Ishara hizi zilianza na kundelea kwa karne nyingi—zikawa kama vile Mungu kuwa katika wakati wa uchumba mrefu jamii ya wanadamu.  Sasa tunashuhudia kilele cha ishara za Mungu kwa mwanadamu katika ujio wa Yesu Kristu.  Hata kama bado tuna mashaka na Mungu aliyetuonyesha ishara nyingi za kutupenda na kutujali katika hali nyingi sana tangu enzi za wahenga wetu, sasa basi tunaye yeye mwenyewe katika hali ya mwili kama wetu, na tumpe basi nafasi atuonyeshe ishara za Mungu katika namna ambayo labda akili zetu zinaweza kujua zaidi na mioyo yetu kuguswa zaidi na uthabiti wa ishara za mapendo ya Mungu.  Tumwache Kristu azungumze na akili zetu na utashi wetu ili kwamba ikibidi tukubali kuwa sehemu ya kundi lake.

Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...

Ee Bwana,

Unajisikiaje ukiuangalia kutoka juu mbinguni ulimwengu uliouumba?  Hakika unaona kupendeza kwake, kupendeza kwa mali asili zake, watu wanaojaliana, watoto wakizaliwa n.k.  Lakini nina hakika kuwa kuna hali nyingine ya ulimwengu unayoiona, hali ya mabaya:  watoto wakishinda njaa na wengine wakifa kwa njaa na magojwa katika mikono ya mama zao; silaha zikipewa uzito kuliko watu ambao zimeundwa kuwalinda; watu wachovu na wapweke wakizurura mitaani, wakiwa hawana kazi, makazi wala kujaliwa na wengine kama binadamu...

Kutoka katika starehe ya nyumba yangu salama, najaribu kuiangalia picha ya juma hili—Picha ya athari za vita.  Naona nyumba zilizopigwa mabomu, moshi ukipanda juu, maua madogo yamesalia katika miti...  Mara inabadika kutoka kama picha ya sehemu iliyo katika vita na kuwa picha ya sehemu ya mtaa wangu.  Kama katika mtaa wangu, watu katika nyumba hizo zilizoteketea walikuwa katika hali yao ya kawaida.  Kutoka katika nyumba hizi watu waliondoka kwenda kazini, wengine kusherehekea matukio ya kifamilia, wakizungumzia mipango ya harusi na kujadiliana kuhusu vitabu na masomo, wakiazima unga kutoka kwa jirani zao, kwa furaha watoto wakicheza na kuimba nyimbo nzuri za kitoto... Sasa yote yamepotea katika magofu yanayoteketea kwa moto.  Mtaa wangu si tofauti, waweza kuwa kama huu wa Sarayevo.

Unauangaliaje ulimwengu kama huo ambapo tunauana na kubomoleana nyumba; ambapo tunatiliana sumu katika maji ya kunywa na tunathamini fedha na mali zaidi kuliko tunavyowathamini wenzetu?  Bila shaka unapata huzuni kubwa sana moyoni.  Viumbe wako wamekusahau, na kusahau uzuri na nia njema uliyowaumbia.

Lakini katika tendo lisiloelezeka wala kufikirika la mapendo, huruma yako inakufanya kujitoa kikamilfu kwa ulimwengu uliouumba.  Kwa njia ya ajabu sana unatuonyesha tena ni kwa kiasi gani unatupenda—unakuja na kuwa mmoja wetu.  Ee Bwana, inawezekanaje kutupenda sisi kiasi hicho, sisi tunaoonyesha chuki kila siku kwa maneno na matendo yetu?  Tena umetenda hili ukijua wazi kuwa hili litahusisha maumivu ya hali ya juu kwako, litakusababishia mahangaiko mengi unapojitahidi kutuonyesha kuwa bado tunapendeka na tunatupendwa na Mungu, na zaidi ukijua kuwa kujitoa kwako kuwa mwanadamu kunahusisha kifo?

Ee Bwana, nifundishe kupenda zaidi.  Nakuomba, tafadhali nipe nafasi nione na kuhisi jinsi gani uliishi maisha yako hapa duniani.  Natamani kukujua zaidi na nataka kuwa nawe hapa duniani.  Natamani kukubali mwaliko wako: kukupa NDIYO yangu.  Nikubali niwe rafiki wako unapotembea hapa duniani.  Niruhusu nijifuze kutoka kwako jinsi ya kuwa vile Mungu alivyoniumba niwe; zungumza na unieleze jinsi ya kuwa mwanadamu mwenye utu ulioniumbia, utu nilioupoteza kwa kutenda maovu, lakini unanirudishia, iwapo nipo tayari kuupokea kwa njia ya umwilisho wako.  Nipe uwezo wa kuyapanga maisha yangu yashabihiane na yako.

Tazama nayastahi sana mapendo yako kwa wanadamu—mapendo yako kwangu.  Kwa kiasi fulani yananipa hisia ya ajabu moyoni—yananitisha kwa kuwa siyastahili; ila sijisikii kukimbia bali kuyajia na kuyakumbatia, kwa kuwa wewe mwenyewe unanistahilisha.  Mapendo yako yananivutia—nipe neema yako ili mapendo yako yaniumbie moyo unaofanana na wako Mtakatifu.  Naishiwa maneno ya kukwambia—niseme nini zaidi mbele ya mapendo haya?  Ee Yesu nasema “asante sana” japokuwa najua asante yangu haielezei kikamilifu shukrani niliyonayo.  Nishike mkono Bwana.  Zungumza nami.  Nionyeshe tena kitabu cha picha za maisha yako.  Nisaidie kukwambia “ndiyo” kila siku.

Maandiko Matakatifu

Waefesi 1:3-14

Wakolosai 1:9-22

Yohana 1:1-18

 

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO