JUMA LA KUMI NA TATU

Mungu Anatayarisha Njia

Mwongozo: Ahadi

Kurasa za mwanzo za Kitabu cha Picha cha Yesu (Albamu ya Picha) kinatuonyesha ustahamilivu na uaminifu wa Mungu katika matayarisho ya kumtuma Yesu Kristu kuja kuwa nasi.  Tunaweza kumwona Mungu akiwaita Abrahamu na Sara na kuwaelekeza waihame nchi yao, na kuanza safari mpya ya maisha.  Tunaona pia kuzaliwa kwa Isaka ya Yakobo (Israeli).  Kitabu hiki cha picha kina kurasa nyingi za maisha ya Waisraeli: Utumwani Misri, kuzaliwa na maisha ya Musa, mpango wa Mungu wa ‘Kutoka’ na Ukombozi wa wana wa Israeli kutoka katika mikono ya Farao na Wamisri, miaka arobaini ya Waisraeli jangwani, na miaka ya mwanzo katika Nchi ya Ahadi.

Mungu aliteua watu kuwa waamuzi baina ya watu, na kisha akawateua wafalme kuongoza watu wake, na tena akawatuma manabii kuwakosoa na kuwashauri watu na wafalme wao hasa pale walipopotoka.  Tunakanganywa, tunapigwa na butwaa na hata kupata mshtuko mkubwa tunapoona jinsi watu wateule wa Mungu wanavyokosa uaminifu kwa Mungu, jinsi taifa lao linavyogawanyika, na jinsi haya yanavyowangoza kuangukia katika utumwa kwa Wababeli.  Baada tunawaona wakilijenga tena Hekalu la Mungu, wanapata tena uhuru wao na kuishi kwa amani ya kiasi, chini ya himaya ya Warumi.

Kuna hisia kama za Majilio katika juma hili la mafungo.  Katika kutamani kumjua zaidi, kumpenda zaidi na kuwa karibu zaidi na Yesu, tunarudishwa nyuma kutafakari ile miaka ya matarajio ya ujio wa Kristu.  Kwanza kuna ahadi ya nchi (Nchi ya Ahadi), kisha ahadi ya mfalme na ahadi ya ufalme usio na mwisho.  Manabii wanazungumzia na kutabiri jinsi hali itakavyokua pale “siku ya Bwana” itakapowadia.  Hii yote inatuambia mengi kuhusu kazi maalumu ya Yesu Kristu; na kutusaidia kuelewa hali ya kuchanganyikiwa iliyousibu ujio wake, kukataliwa na wayahudi na hali ya inayoshangaza aliyoitumia kutekeleza ahadi za Mungu kwa watu wake.

Katika juma hili tuipe nafasi akili na mioyo yetu isikilize simulizi ya matayarisho ya njia ya Yesu Kristu kuja katika ulimwengu wetu.  Kama wapenzi wa Kristu, tunataka kujua yote yanayomhusu. Tutaweza kuona na kuthamini zaidi, labda kuliko wakati wowote ule, uaminifu wa Mungu, na kutambua ukubwa na umuhimu wa shughuli ambayo Yesu alikuja kuitekeleza duniani.

Katika juma hili tutafakari kila linalotujia mioyoni mwetu.  Ni kiasi gani tumemjua zaidi Yesu?  Ni jinsi gani upendo wetu kwake unavyoongezeka?  Je, tunavutiwa kusema yapi kwa huyu atuonyeshaye “kitabu chake cha picha”?

Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili

Mojawapo ya mambo ambayo tumekuwa nyeti kwetu katika miongo iliyopita ni umuhimu wa asili yetu, kile kinachotufanya tuwe tulivyo.  Mambo mengi yamehusika katika kutufanya tuwe tulivyo leo hii, ila wahenga—mababu na mabibi wetu—wamechangia kwa kiasi kikubwa katika hili.  Juma hili tujajaribu kuwatazama kwa karibu wahenga wa Yesu Kristu.  Nia yetu katika juma hili ni kumjua Yesu kwa undani zaidi.

Hili si zoezi la kitaaluma au akili.  Si lazima tuwe wasomi wataalamu wa Maandiko Matakatifu ili kufanikiwa kufanya hili zoezi.  Ni jambo jepesi iwapo tunaijua kikamilifu nia yetu: Yesu katuonyesha wazi kuwa anatupenda kupita upeo, na sisi tunataka kumjua zaidi na zaidi.  Tutatumia majuma kadhaa baada ya hili tukipitia Injili ili kujaribu kuwa karibu na Yesu katika simulizi za yale aliyotenda, aliyofundisha na kusema hapa duniani.  Juma hili linatugusia kidogo tu Yesu ni nani na mazingira ya wakati alipotujia.

Katika juma hili tunajaribu kujiweka katika utambuzi kuwa uzao wa Yesu ni wa Kiyahudi.  Basi jinsi alivyofikiria kujihusu yeye mwenyewe, alivyomuwaza Mungu, mtazamo wake kwa vitu vilivyopo na matukio mbalimbali, na utamaduni na jadi yake vilikuwa na asili ya Kiebrania.

Mtazamo wa ulimwengu aliokuwa nao Yesu ulijengwa na utambuzi kwamba Mungu alimwita Abrahamu kutoka katika nchi yake na kumwahidi makazi mapya katika nchi mpya.  Uaminifu wa Yesu Kwa Mungu ulihimiliwa na kumbukumbu kuwa Mungu daima alitimiza ahadi zake zote.  Uzee wa Sara, mkewe Abrahamu haukuwa kizuizi cha Mungu kumpatia Abrahamu mototo aliyemwahidia.  Jeshi la Pharaoh halikuweza kushindana na ahadi ya Mungu kwa watu wake; na japokuwa Hekalu la Yerusalemu liliweza kubomolewa, Mungu aliwezesha lijengwe tena.  Ninapokuwa na nia kamili ya kumjua Yesu, sharti nijue mapokeo ya imani aliyopata kutoka katika jamii yake na kumpa hali ya kujiamini katika kazi yake.

Kuliko kusoma mengi zaidi, ni muhimu kutafakari yale ambayo tayari tunayajua kuhusu utamaduni wa Kiyahudi.  Soma sehemu ya Agano la Kale ya Biblia iwapo hii itasaidia kuhuisha kumbukumbu yako na kukupa habari zaidi.

Labda katika juma hili, ninapotembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine, labda nikiwa nimechanganyikiwa au kukasirika au kujihisi mpweke, naweza kumgeukia Yesu na kumwuliza: “utamaduni na jadi yako ilikutayarishaje kuikabili hali kama ya namna hii?” Jibu lake litakuwa neema hasa tunayoitafuta juma hili.  Mazungumzo haya ya ndani moyoni kati ya jadi ya Yesu Kristu ya jamii yangu itatusaidia kwa kiasi kikubwa kumjua, kumpenda zaidi, na hivyo kuvutiwa kujitoa na kuwa naye katika kazi iliyomleta hapa duniani.

Tumia pia nyenzo nyingine ulizopewa katika juma hili.  Fuata kwa uaminifu mpango wa kutafakari yale uliyopewa katika juma hili, kuanzia mara unapotoka kitandani asubuhi.  Unapoelekea kumaliza siku yako, labda jioni baada ya kazi lakini kabla ya muda wa kupumzika kitandani, jipe muda wa kumpa Mungu shukrani zako. Jaribu kuwashirikisha wenzako mnaofanya nao mafungo haya neema zozote unazopata—waweza kuwashirikisha kwa mazungumzo au kwa kuwaandika au kwa kutumia sehemu ya kuchangia katika mtandao huu.

Kwa Ajili ya Safari: Mwanzo Hisia za Shauku ya Faraja

Misimu hubadilika. Dunia imekua “ikizunguka na kujizungusha, ikijipeleka kule na kujirudisha huku” katika kuhusiana na yule aliye mwanzo wa vyote, vinavyoonekana na visivyoonekana, vilivyo na maisha na visivyo na maisha.

Kama familia ya wanadamu, tumekuwa pia na hali kama hii—wakati mwingine tukimwelekea au kumkimbilia, na wakati mwingine tukimgeuzia kisogo Mungu aliye mwanzo wa mwanga na maisha.  Mara nyingi katika historia yetu wanadamu tumemtaka Mungu awe karibu sana nasi kutulinda, kutulisha au kutusaidia katika mahitaji mbalimbali.  Wakati mwingine tumemdai Mungu atuwache kuwa huru kutoka katika “nguvu zake zinazotuwekea mipaka”—tumetaka kujiamulia njia yetu wenyewe ya kuishi.  Nabii isaya anasali kwa upole, Tumekuwa kama watu usiowamiliki kamwe; kama watu wasioitwa kwa Jina lako.” (Isaya 63:19).

Juma hili tunakaribishwa kupata muonjo wa kuwa katika hali ya shauku au kiu.  Tunajiunga na ulimwengu baridi unaotamani uvuguvugu na mwanga.  Tunajiweka pamoja na Waizraeli wa kale katika kiu na matarajio yao ya upendo wa Mungu, kiu ya kuwa na mwandani wa huruma.  Tuungane na wake kwa waume ambao wameweka juhudi kuwa wema, na kwa moyo mkunjufu wamejisalimisha katika ukweli mtukufu kuwa wao ni wana wa Mungu mmoja, ambaye anaweza kupewa majina mengi na wamwaminio, ila anabaki katika uaminifu wake kwa wote wanaomtafuta.

Juma hili sala yetu inaweza kupata msukumo kutoka katika nafasi zinazotujia na kudai subira zetu—taa za barabarani, foleni mbele ya dirisha la huduma, mlolongo wa kungojea na kuingia katika basi, kumngoja mgeni muhimu anayewasili kwa basi au kwa ndege, nk.  Katika wakati huo tunakuwa na hali ya uwazi, utupu au upweke moyoni.  Tuuchukue uzoefu wa hali hiyo na kuuweka katika hali ya sala au zoezi la sala—kuwa katika hali ya matarajio, hali ya kungojea, hali ya kiu bila kukata tamaa.  Huku ni kudumu katika sala, sala kama hali ya kumngojea Mungu kutujia, kumsubiri kutenda jambo au kumtarajia kutimiza ahadi muhimu, tukiamini kuwa daima yeye ni mwaminifu na mwenye huruma.  Mungu atatujia muda unaofaa, atatupa tunachohitaji, atatuonea huruma na kutupa msamaha tulipomwasi. Hapa tunafanya zoezi la kuwa katika hali ya shauku waliyokuwanayo watu wa Agano la Kale kurudiwa tena na kuwa na makazi pamoja na Muumba wao mpendwa. Juma hili tunasali si kukwepa au kuomba kuondolewa hali ya kiu na shauku ya moyoni, bali kuipokea na kuikubali hali hiyo.  Sharti kuwe na nafasi au chumba ndani yetu na kiu ndani yetu ili kwamba Majilioya Yesu yawe na maana na kuzaa matunda—akija akute anangojewa kwa shauku, na apate mahali pa kukaa nasi mioyoni mwetu, katika maisha yetu. Tunasikiliza vilio vya matarajio vya wahenga wetu katika imani, “Ni hadi lini, Bwana wetu?.” Tunasikiliza pia vilio vya matarajio yetu, “Njoo, Bwana Yesu, njoo.” Kama vile jua linavyosonga mbele na kuiacha dunia nyuma kila siku na kisha tena kuisogelea siku inapoanza, tunaungana na dunia katika kitendawili hiki cha mwanga na giza.

Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...

Yesu Mpendwa,

Hakika juma hili limekuwa tofauti sana na majuma mengine.  Sijawahi kufikiria kuwa Agano la Kale ni simulizi ya historia ya jamii yako—ila nilidhani ni hadithi tu za watu walioishi kabla yako, ambao walikuwa na ushawishi mkubwa kwako.  Nilipoanza mafungo haya, nilikuonyesha albamu ya picha za maisha yangu, zote za wakati mgumu na wakati mwororo, na niliona kuwa daima ulikuwa nami.  Sasa, ninapojihisi karibu zaidi na zaidi nawe, nataka kuona historia yako, simulizi za maisha yako.  Nakupenda sana, na nataka kusikia hadithi za yote yaliyowahi na kukufanya uwe ulivyo.

Nategemea mengi sana kutoka katika hadithi hizi.  Ni kwa namna nyingi sana watu wako wamekuwa wakingojea ujio wako: wengine wakiwa na subira na wengine wakikata tamaa, karne moja baada ya nyingine.  Walikuwa wakitafuta mfalme ambaye atakuja kuwaongoza na kuwakomboa.  Lakini ulikuwa mfalme wa namna tofauti sana!  Walitegemea na kutaka mfalme mwenye fahari na mabavu, lakini uliwajia katika umaskini, unyenyekevu na utumishi.

Uliihisi hali ya kuvunjika  kwa matumaini yao? Hakika ulijua wazi kabisa simulizi na mapokeo waliyokuwa nayo kwa karne nyingi kuhusu mfalme ambaye walimtegemea; na jinsi walivyozitafsiri simulizi hizo.  Ilikuwa vigumu kwako kuwa tofauti na vile walivyodhani? Najua ni asili yetu sisi wanadamu kupenda kuwaridhisha wenzetu. Je, ulikuwa na mahangaiko yoyote yaliyohusu ukweli wa ‘wewe ni nani’, na yale uliyotaka kuwafundisha?

Ee, Yesu, asante sana kwa kutupenda sisi sote kiasi hicho.  Asante kwa kunipenda mimi, kiasi cha kunichagua niwe nawe katika maisha yangu hapa duniani.  Naweza tu kuwaza jinsi ulivyohangaika katika juhudi za kuufikisha ujumbe wako wa mapendo na ukombozi kwa watu ambao tayari walikuwa wamevunjika moyo na kukata tamaa. Uliuishi ufalme wako namna gani ikiwa watu ambao walikuwa wakimngoja mfalme kwa karne nyingi walikuona kinyume kabisa na matarajio yao.  Haukuwa yule walioshawishika kumngoja; lakini wewe hukukata tamaa, ulibaki nao na kuendelea kuwa mwaminifu kwa ujumbe uliowaletea.

Asante sana kwa kunishirikisha hadithi zako na za jamii yako.  Tafadhali kuwa nami katika juma hili ambapo naingia ndani zaidi ya maana ya historia yako, simulizi wazi za kusisimua za Agano la Kale.  Kuwa nami ninapoingia ndani ya Agano la kale na nipojifunza mengi kuhusu wewe kutoka katika historia hiyo ya kweli kuhusiana na kukungoja na kukutarajia, na hatikaye kutimiza kiaminifu kabisa yale uliyoahidi.  Bwana rafiki yangu, asante sana kwa kuwa nami, hata pale ninapokusikitisha—pale ninapoishi kama vile sikuumbwa nawe.  Asante sana kwa kwa uaminifu wako kwangu na kwa kunipeda. Amina.

Maandiko Matakatifu:

Mwanzo          12:1-7

Mwanzo          18:1-15

Mwanzo          37:1-36

Kutoka            2:1-25

Kutoka           15:1-18

Zaburi              81

 

 

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO