JUMA LA KUMI NA NNE

Mungu Anatangaza Njia; Watumishi Wako Tayari

Mwongozo: Imani ya Watu Alimozaliwa Yesu

Tunapoangalia albamu ya picha ya rafiki yetu, baadhi ya picha zinazotuvutia zaidi ni zile za wazazi na za bibi na babu zake.  Tunajaribu kuziangalia picha hizo kwa ukaribu na umakini zaidi ili kuona jinsi ambavyo rafiki yetu anaweza kuwa amefanana na mama, baba, bibi au babu wake.  Tunajaribu pia kuchunguza iwapo kuna ushabihiano wowote wa tabia, sifa na mienendo ya nafsi, kati ya rafiki yetu na wahenga wake—jinsi walivyosimama kupiga picha, mavazi waliyonayo, shughuli waliyokuwa wakifanya pichani, ishara za usoni, nk.

Katika juma hili tutatumia sura za kwanza ya Injili ya Matayo na ya Luka katika kufuatilia matamanio yetu yanaoongezeka daima ya kumjua Yesu kwa ukamilifu zaidi, ili kwamba tuweze kumpenda kwa undani zaidi, kwa sababu tunataka kumfuasa kwa uhuru zaidi.

Mbinu au utaratibu wetu juma hili utakuwa “kukodolea macho” nyuso za Zakaria na Elizabeti, Yosefu na Maria (Mariamu), ili kuona ni nini wanatuambia kuhusu mpendwa wetu Yesu.  Tutajaribu kujipenyeza katika matukio kadhaa ya Biblia huku tukiendelea na shughuli zetu za maisha na kazi za kila siku.  Tutajaribu kujua zaidi kuhusu tabia na sifa za nafsi ya Yesu.  Hii tutafanya kwa kupitia njia ya kujielewesha kwanza imani ya jamii alimokulia ambayo ilikuwa na ushawishi mkubwa katika kumjengea tabia na utu wake kwa ujumla.

Mtindo huu wa kusali unahitaji mazoezi, ila mtu yeyote anaweza kuyafanya, kwa sababu ni jambo ambalo tunalifanya bila kukusudia kila tunapokutana na wazazi wa tumpendaye. Na tujapojua jambo fulani kuhusu familia ya rafiki yetu, inakuwa ni kama kujua jambo kujifunza jambo moja zaidi kumhusu rafiki yetu.  Kwa msaada zaidi kuhusu namna hii ya kusali hakikisha umesoma na kuelewa zana za kukusaidia kusali unazopewa.

Zakaria hakuweza kuwaza ni jinsi gani Mungu angeweza kupata ushindi mbele ya uzee wa mkewe Elizabeti—wangewezaje kupata motto katika uzee huo?  Hakuweza kuzungumza lolote hadi ilipofikia wakati wa kutamka jina la mtoto wao wa kiume, “Mungu ni Mwaminifu”.  Malaika alimwarifu Maria kuwa “...kwa Mungu hakuna lisilo wezekana.’’ Elizabeti anasema, “Wewe umebarikiwa kwa kuwa uliamini kwamba Bwana atatimiza yale aliyokuambia.  Nafsi yote ya Maria inatangaza ukuu wa Mungu, na maneno na mwenendo wake vinatamka wazi imani ya wahenga wake.

Tunapoendelea na shughuli zetu za maisha kila siku, hadithi hizi zenye maajabu ya kupendeza zitalipa juma letu sura maalum.  Atakuwepo Zakaria wakati tunapokuwa na mashaka, pale ambapo tunapotilia mashaka hata uwepo wa Mungu.  Muda mwingine wa mashaka-ya-Zakaria pale tunapoweza hatimaye kusema, “Mungu ni Mwaminifu”.  Kutakuwa na muda ambapo picha ya wiki hii katika kompyuta yetu itatukumbusha hisia za nzito na kusema, “Hii itawezekanaje?” Na utafika muda ambapo picha hiyo itakukumbusha maneno ya Maria, “Mini ni Mtumishi wa Bwana, nitendewe ulivyosema.”

Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili

Alipokuwa akimwongoza kiroho mtu mwenye tamaa yake ya kumjua, kumpenda na kumfuasa Yesu, Mt. Inyasi wa Loyola aliwamfundisha kutafakari matukio mbalimbali katika Injili, akitilia mkazo zaidi suala ya kuwekwa huru.  Katika juma hili na majuma mengine yanayofuata, tutajifunza kufanya hivi katika namna inayoendana vema zaidi na maisha yetu ya shughuli kila siku.

Baada ya kusoma simulizi fulani ya tukio katika Injili, tunaweza kuliwaza na kuwa na picha ya wazi kabisa ya yale yaliyotokea.  Lakini hii si toauti sana na mtu kutusimulia kwa uwazi tukio katika maisha yake.  Ni kweli kuwa kuna thamani katika simulizi hizi, lakini kuna mbinu nyingine yenye kuingia ndani kabisa ya tukio, na inawezekana kwa kuwa Maandiko Matakatifu ni Neno la Mungu.  Hadithi au simulizi hizi ni ufunuo wa Mungu ulio hai na ufanyao kazi.  Hivyo basi, tunaposoma Injili, kuna jambo linalotokea ndani ya mioyo yetu.  Ufunuo wa Mungu unakwenda mbele zaidi na hata kupita mahali andiko tulilosoma lilipoishia.

Mtakatifu Inyasi anatuhamasisha kuingia ndani au kupenya ndani ya simulizi ya tukio.  Hataki tusikilize tu, na kupata ukweli wa lile lililotokea.  Ananitaka mimi nilipenye tukio hilo, liwe na maana katika maisha yangu na kunipa ufunuo wa Mungu—zoezi hili hufanyika zaidi ndani moyoni na si akilini tu.  Namna hii ya kutafakari hunipeleka ndani zaidi ya Neno la Mungu kuliko simulizi tu ya Neno hilo, ambayo inaweza kusomwa na yeyote ajuaye kusoma au kusikiliza, na kuwaza kwa akili yake.  Nikisoma Neno la Mungu kwa moyo namna hiyo, Neno hilo linakuwa hai ndani yangu na Yesu huzungumza nami ndani moyoni, na nakuwa mshiriki hai katika tukio husika.  Hebu tujaribu kuchukua mifano miwili.

Kipindi cha Sala ya Kutafakari Tukio Katika Injili

Kama nina muda, kati ya dakika thelathini hadi arobaini na tano, naweza kupata mengi sana kutoka katika tukio lolote katika Injili.  Nitaanza kwa kujiweka binafsi mbele ya Mungu. Kisha, rasmi nitamweleza Mungu ni neema ipi hasa ninayohitaji kutoka kwake katika muda wa sala.  Kwa mfano nia yangu yaweza kuwa ‘kuelewa kwa undani zaidi Yesu ni nani, ili kwamba mapenzi yangu kwake yaongezeke, na nitamani zaidi kuwa naye.’

Kisha nitasoma kutoka katika Injili, simulizi ya tukio husika na kuiweka Biblia pembeni.  Taratibu nitaanza kufanya taswira au picha ya lile lililotokea kwa ukamilifu niwezavyo.  Tukio linatokea wapi?  Tambua na tilia maanani vyote vilivyopo katika tukio na vinavyolizunguka tukio.  Ni nani yuko hapo?  Waaliopo wamevaa mavazi gani? Hali ya hewa, ni joto au baridi kiasi gani?  Harufu gani naweza kunusa?  Napenyeza katika tukio ndani zaidi kwa kuwa mmojawapo katika tukio.  Naweza kuwa mmojawapo katika kundi kubwa la watu, au naweza kuwa mmojawapo wa watu wanaotajwa kwa majina katika tukio.  Ninapofikia hapo naliwacha tukio liendelee kutendeka, na kwenda popote linaponipeleka.  Nikiwa nimelipenyeza tukio na kuwa sehemu yake, maneno na matendo ni zaidi ya mfano mkanda wa video wa tukio unaochezwa tena.  Kutoka ndani ya tukio, naweza kurudi nyuma na kulipa tukio mtazamo mpya.  Kwa mfano, naweza kutoa nafasi yale niliyofunuliwa yafanywe katika maneno, matendo na ishara za wale wanaohusika katika tukio, au naweza kutulia na kutilia maanani yale yanayotokea moyoni mwangu.  Maelezo ya tukio yanapungua umuhimu kwa kuwa tukio lenyewe limeingia moyoni mwangu—si jambo lililo nje bali ni jambo lililo sasa sehemu ya matukio katika maisha yangu.  Mwishowe namaliza kwa sala, nikizungumza na Mungu wangu ndani moyoni, yeye kama rafiki ninayempenda sana wala sio Bwana ninayemwogopa—nitamweleza lolote linalonijia moyoni, nikimpa shukrani kwa neema nilizopokea muda mfupi uliopita.

Kutafakari Tukio la  Katika Maisha ya Kila Siku

Kuna mambo mengi ambayo hutufanya tusiwe huru hapa duniani—mengine yamesababishwa na jamii na tamaduni zetu, udhaifu wa kibinadamu unaohitaji msaada wa Mungu, na kikubwa zaidi udhambi wetu binafsi au udhambi wa jamii.

Tukiwa na mtazamo wa uhuru, yawezekana kutumia simulizi ya Neno la Mungu kuzaa matunda hata tukiwa katika harakati za maisha yetu ya kila siku.  Katika juma hii, kwa mfano, nitaamka asubuhi, na wakati nikijiweka tayari kuanza siku yangu (nikinawa au kuoga, nikichana nywele, kuvaa nguo nk.), nitakuwa nikifikiria juu ya matukio katika Biblia ambayo tutatafakari juma hili.  Juma hili litakuwa juu ya Yosefu, Zakaria, Elizabeti na Mariamu.  Kisha nitajaribu kujikumbusha kwa kifupi habari zilizopo katika masomo yanayowahusu hao (kumbuka tunatumia Sura za kwanza za Injili ya Luka na ya Matayo).  Hapa yaweza kuwa kama hivi: jitihada ya kuamini kuwa hakuna lishindikanalo kwa Mungu, kujikakamua katika kuipokea hali ya kulazimika kumtegemea Mungu na kuishi katika imani, kujiweka wazi kufunuliwa ukweli wa uaminifu wa Mungu.  Kisha nitaipitia akilini siku iliyo mbele yangu.  Nikiwa katika hali ya moyo wazi, kunaweza kutokea mashahibiano, mlingano au muungano katika ya Neno ninalotafakari na matukio katika siku yangu, au kumbukumbu ya maisha yangu inayonijia.

Yaweza kuwa kuna mivutano katika ndoa yangu na ni vigumu kwangu kuamini kuwa uaminifu wa Mungu kwetu una nguvu kuliko ukaidi wetu.  Katika mfano huu, ninapokuwa na mwenzangu wa ndoa, naweza kuona jinsi hali yangu inavyoweza kuwa na ushahibiano wake na simulizi za Injili zinazomhusu Zakaria na Maria—wakati mmoja nikijikuta siwezi kusema lolote hadi ninapoweza kutamka, “Mungu ni Mwaminifu,” au wakati mwingine kujisalimisha kwa Mungu “Mimi ni Mtumishi wako Bwana.”  Au nikimsikia Elizabeti akisema, “Mwenyezi Mungu amekubariki, kwa sababu uliamini kuwa atatimiza ahadi zake.”

Labda yote ninayotarajia ni mzunguko wa kawaida wa shughuli nyingi za kazi za kila siku, zilizojaa harakati na shinikizo nyingi ambazo nazitekeleza katika hali ya kawaida. Katika majuma yaliyopita ya mafungo haya, niligundua kuwa shughuli na mahangaiko yangu ya kila siku yaweza kuwa sehemu ya hali ya udhaifu na udhambi wangu, na pia sehemu ya upendo mkuu wa Mungu unaoshinda udhaifu na udhambi wangu kabisa.  Juma hili laweza kuwa na mazao mengi sana ya kiroho iwapo nitapitia maisha yangu kama vile mtu anayekagua shamba kake, nitatazama kwa makini matukio mbalimbali katika maisha yangu, kama vile Elizabeti.  Jaribu kuwa na maswali kama haya daima moyoni unapoyapitia maisha yako: “imekuwa kama hivi kwa muda mrefu kiasi kwamba sitegemei badiliko lolote?”; “Mimi ni nani hadi kudhani nitawahi kuzaa matunda kuliko niwezavyo?”, “Katika uzee huu, hali hii ya ukimya wa tumbo langu la uzazi kuwa kama aliyelaaniwa, yawezekana mimi kudhani naweza kuzaa sauti iitayo jangwani, ‘Tayarisheni njia ya Bwana’?”

Labda kuingia katika uwanja wa matukio ya maisha yangu ya kila siku ni kukariri mstari mmoja kutoka katika simulizi ya Injili na kuuacha upenye moyo wangu ninapousema nikiwa hata na pumziko fupi kama vile kungojea usafiri, kuwa katika foleni katika dirisha la huduma nk.—nitaurudia mara nyingi iwezekanavyo, huku nikiwa natambua ninachofanya na kutokusahau kuwa ninasema Neno la Mungu.  Mfano mzuri juma hili ni kurudia maneno ya Mariamu, “Moyo wangu wote wamtukuza Bwana” au “Mwenyezi Mungu amenitazama mtumishi wake mnyonge.”

Mwishowe, itakuwa vema kama utajaribu kuwashirikisha wengine tafakari hizi, mbinu ulizotumia na neema ulizopokea.  Unaweza kufanya hivi kwa kutembelea katika mtandao huu Sehemu ya Kushirikishana iliyo katika Ukurasa wa Mwongozo.

Kwa Ajili ya Safari: Kutumia Udhanifu Katika Sala

“Dunia imejawa na nishati tukufu ya Mungu.” Padre Mjezuiti na mshairi Gerard Manley Hopins anapiga mbiu hii yenye maana mbili katika mstari wa kwanza wa shairi lake mashuhuri kuhusu ulimwengu wetu unaopendwa na Mungu

Ulimwengu una msukumo unaoendeshwa kama vile kwa nishati kubwa ya umeme ili kudhihirisha utukufu wa Mungu.  Ulimwengu pia una nishati kama ya umeme inayosukuma kutenda jambo fulani lililo muhimu sana.  Maana zote mbili zimezingatiwa katika juma hili. Kwa mfano, tukiangalia kile kilichokuwa kinawasukuma kwa ndani Elizabeti, Mariamu na mwanamume aitwaye Yosefu ni nishati ishindayo uwezo wao wa kibinadamu.

Inahitaji aina fulani ya unyeyekevu ili kushangaa—unyenyekevu unaotoa nafasi kutendeka lisilotarajiwa, lisilo la kawawaida au hata linalotisha.  Aina hii ya unyenyekevu tunaweza pia kuiita “uwazi”. Ni hali ya msimamo  au silika ya ndani moyoni inayompa mtu hali ya kuwa tayari kutokupinga au kupokea lolote linaloweza kusemwa au kupewa.  Si hali ambayo mtu anakuwa nayo sasa na kuipoteza baada ya muda mfupi, au inabagua lini kuwa wazi na lini kutokuwa wazi. Ni hali ya moyo inayodumu hivyo basi kumpa mtu mtazamo usiotetereka, na kuwa na hali ya kuguswa na yanayotokea au kuwa na hisia hai isiyosinzia-sinzia kuelekea matukio mbalimbali, huku na kule.

Tunasali tukiwa na neema hii ya unyenyekevu na tukiomba kupewa neema hii zaidi juma hili tunapowatazama Elizabeti, Mariamu na Yosefu wakitekeleza nafasi zao katika mpango wa wokovu wetu.  Ni kama tupo katika aya za awali za sura ya mwisho ya Historia ya Wokovu Wetu.  Hapa tutaanza kumjua Yesu na namna yake ya kuishi na kuwaza.  Kama ni igizo jukwani, basi Yesu ni anaonekana hapa kama “mwigizaji mkuu” na wengine kama waigizaji wanaotekeleza nafasi zao ambazo ni za kumleta “mwigizaji mkuu” jukwaani.

Mtakatifu Inyasi anasisitiza wale wanaofanya Mazoezi ya Kiroho kujaribu kupenyeza tukio au simulizi husika kwa kutumia uwezo wao wa kutafakari.   Mara nyingi tunatumia kumbumbu na uwezo wetu wa kufikiri na kusahau zawadi kubwa tuliyopewa kwa asili, uwezo wa kutafakari.  Tumeshawishika tunaweza kuufikia ukweli kwa urahisi zaidi kwa kupitia mantiki, utumiaji wa takwimu na kumbukumbu, hivyo basi kuzarau umuhimu wa kutafakari—tunasema kutafakari kunazaa ‘ndoto za mchana’ zisizo na umuhimu wowote maishani.

Saikolojia (Elimu Nafsia) inatumia mlango wa fahamu wa kutazama ili kuanzisha tafakari ambayo tunaijua kama vile ‘vipimo vya upachikaji’ (projective tests).  Labda umewahi kutumia kipimo cha Rorscharch;  Katika kipimo hicho unaonyeshwa michoro na madoa anuwai ya wino, na kwa kutumia yale utakayosema baada ya kuyaangalia madoa hayo, mambo kadhaa ya kweli kukuhusu yanakuwa wazi kwa yule anayekupa kipimo hicho.  Mpimaji kapata ukweli kwa kutumia tafakari.  Tafakari ina uwezo na nguvu kubwa kuliko wengi tunavyoamini.  Mtakatifu Inyasi aliamini kuwa zawadi zote alizopewa mtu: kusikia, kusema, kuelewa, kujieleza, kukumbuka, kuona, kuhisi, kufikiri, kuwaza, kutafakari, kutaamuli nk., zinaweza kutumiwa na Mungu kutujia au kuwasiliana nasi.

Juma hili basi na tutumie zawadi hii ya kutafakari ili tuwe tayari kupokea neema ya uwazi, unyenyekevu na matumaini.  Jitahidi kuwa macho kujua umesimama wapi wakati Mariamu anapotokewa na malaika.  Usisahau kile unachodhani malaika anamwambia Mariamu na ni kipi Mariamu anawaza..unasema nini na unafanya nini unampomfuatilia Mariamu kwenda nyumbani kwa Elizabeti?  Ni kipi Yosefu anafanya anapoamka baada ya ndoto ambapo anatambua inampasa kumuoa Mariamu mchumba wake japokuwa ana ujauzito usio wake?

Baada ya hapo Mtakatifu Inyasi anasihi kufanya tafakari kutuhusu sisi ili tuweze kupata mang’amuzi na neema kutoka katika zoezi hili.  Labda tunaweza kumtazama Mariamu kwa umbali, hivyo ni vema.  Sasa na tusali tukiwa na hizo hisia za kuwa mbali naye.  Pengine umbali umekuja kutokana ja kutotaka kuwa na lolote linalohusu sehemu hiyo, na hapa basi tunapata mwito wa kuomba imani zaidi.  Sasa tupo hapa, tumeuweka ukweli katika sala, ukweli ambao uhalisi wake umefumbuliwa katika hali mpya na ya kushangaza.  Kwa Mt. Inyasi, kuwa karibu na Yesu na rafiki zake wa karibu ni kuwa karibu na sisi wenyewe, kuwa karibu na nafsi zetu.  Hili si suala la kujipenda kibinafsi au kujitenga kichoyo.  Hili linasababishwa na ukweli kuwa kwa kadiri ninavyokuwa karibu na nafsi yangu na karibu na ukweli halisi kunihusu, ndivyo naweza kutambua ukaribu wa kimapendo kwangu ambao Yesu anao.  Umwilisho wa Ukweli wa Mungu unaingia katika maisha ya hawa watu watatu kwa ‘kuwa-nishati-sha’ kwa imani na kuwapa neema ya uwazi na unyenyekevu wa kupokea vema ajabu na mshangao huo wa ujio wa Yesu. Juma hili linatisha, ila pia linatuliwaza hasa pale tunapojionea jitihada za mwanadamu kutoa nafasi kwa Mungu katika sehemu ambayo amekuwa akiamini kwa muda mrefu ni yake binafsi, nafasi ya faragha.  Tunasali kwamba nasi tupokee nishati ya uwepo mtukufu wa Mungu.

Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...

Yesu Mpendwa,

Asante kwa kunionyesha tena albabu ya picha za jamaa yako yako.  Kuna utofauti kidogo kusali kwa namna hii, na naweza kujihisi nikiwa na utambuzi zaidi wa nafsi yangu.  Kuwa nami katika hili.  Ipe nafasi hali hii inilete karibu zaidi nawe.

Namtazama Elizabeti na Zakria wakifanya juhudi za kila namna ili kupata uzao, na kisha wanakata tamaa.  Hakika lilikuwa jambo zito zana! Je, walikaa pamoja wakaikumbatika pamoja hii ‘bahati mbaya’?  Waliweza kuibeba vipi hali yao hii katika maisha yao ya ndoa?  Halafu, miaka mingi imepita, wakati Elizabeti anakuwa mkongwe, malaika anawatokea na kuwaeleza kuwa watapata mtoto wa kiume.

Kisha nawatazama Mariamu na Yosefu—Mariamu akiwa bado mwanamwali.  Namwona akicheka jikoni, huku akitayarisha supu katika jiko, akiwafurahisha rafiki zake kwa hadithi za kuchekesha.  Bwana Yesu, ni kutoka kwake huyu atakayekuwa mama yako ndiyo ulijifunza kusimulia hadithi?  Kisha namuona mwanamwali huyu mchangamfu mwenye kicheko kinachovutia, kasimama jikoni akiwa pekee wakati malaika anapomtokea. “Atakuwa Mama wa Mungu?”  Natazama kwa mshangao anapokakamkia habari hii.  Anajua wazi habari hii itayageuza maisha yake kabisa—mambo hayatakuwa tena kama alivyotarajia!  Je, yupo radhi kuacha maisha yake kuchangamanishwa namna hii?  Alitaka na kutegemea maisha ya kawaida tu: kuwapikia rafiki zake, kufunga ndoa na Yusufu, na kwenda katika Sinagogi kusali kila wiki.  Ni kweli kuwa alitaka kuishi maisha yake yote akikuamini na kukutumainia Mungu wake, lakini ilikuwa sharti iwe katika hali ngumu namna hii?

Sikutegemea Mariamu angekusumbua moyoni.  Nilifikiria kuwa ulitabasamu tu kitakatiffu na uamuzi ulikamilika.  Lakini sasa namwona akikakamkia woga wake na kusali akimwomba Mungu kama ilivyokuwa kawaida yake alipoogopa jambo fulani.  Woga wake unayeyuka.  Kama hivi ndivyo Mungu atakavyo maisha yake yawe, yupo tayari kuyaishi. Namwona tena, bado kasimama jikoni, supu bado inachemka katika jiko.  Anageuka na kwa taaratibu anamtazama  malaika usoni na kusema, “Ndiyo.”

Nguvu ya sala hii mbele zako inanishangaza, ee Yesu.  Namwangalia mama yako na namwona akiwa mtu wa kawaida mbele yangu.  Namwona akisema “Ndiyo” yake.  Napata tena kujikumbusha kuwa nipo katika sala halisi na si katika ndoto.  Labda uwezo wangu wa kutafakari unanyong’onyea.  Nafanya kile alichofanya Mariamu.  Nipo katika hali ya kuogopa, hivyo namsalia Mungu.  Taratibu woga unapungua.

Sikumbuki kama nimewahi kumwona Mama yako katika hali ya uhalisi wa kibinadamu namna hii—akiwa hai machoni pangu, mtu wa kawaida mwenye kufurahi, anayepata mashaka na anayesali kama yeyote anayemwamini Mungu.  Namwona akisema ‘ndiyo’ yake, na hii inanikumbusha ‘ndiyo’ yangu katika maisha yangu.  Nataka kukujua zaidi na kufanya maisha yangu yafanane zaidi na ya kwako.  Nataka kuwa wazi kupokea ujumbe wowote unaonitumia, japokuwa najua wajumbe wako hawatanijia katika umbo la malaika wenye mbawa.  Najua ujumbe wako utanifikia kwa kupitia watu ninaowaona na kuwa nao kila siku katika maisha yangu.  Yesu wangu, nisaidie kumtambua yule umtumaye kuniletea ujumbe.  Nisaidie kuusikiliza na kuuelewa ujumbe; na zaidi ya yote, nipe moyo niweze kusema “Ndiyo”.

Maandiko Matakatifu:

Luka           1:5-25, 57-66

Luka           1:26-38

Luka           1:39-56

Luka           1:67-79

Matayo       1: 18-24

 

 

 

MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO