JUMA LA KUMI NA TANO
Kazaliwa Kwetu, Kwa Ajili Yetu
Mwongozo: Neema ya Kuzaliwa Kwake
Uchu wetu unaendelea. Ni lazima kwetu kuiamsha upya kiu hii ndani
yetu katika juma hili, (iwapo imefifia)—kiu au uchu wa kumjua Yesu kwa undani
zaidi. Kwa kumwangalia na kumwelewa,
tunategemea upendo wetu kwake kuwa mkamilifu zaidi. Upendo wetu kwake unavyoongezeka katika
ukamilifu, tunapata uhiari mkubwa zaidi wa kuwa naye katika utume wake.
Kwa hiyo, tutakachozingatia akilini mwetu na
katika yote tuyatendayo katika juma hili la mafungo ni pote, yote, wote na
vyote, vilivyokuwepo na kutokea katika kuzaliwa kwa Yesu. Hii itatuelimisha Yesu ni nani. Hata hivyo, kama tulivyoshuhudia hapo awali, kujua
huku hatukupati kwa zoezi la kitaaluma, bali zoezi la kushiriki, hivyo basi
kuwa mtendaji au mshiriki katika tukio lenyewe. Tunahitaji kupitia matukio
yaliyojiri ili kuona wasiwasi uliochanganyika na hamasa waliyokuwa nayo wazazi
wake, hali ya ufukara waliyokuwa nayo; na kwa upande mwingine amani na
kuridhika kwao kuwa katika hali hii ambapo ajabu ya kuzaliwa kwa Yesu kama
mwanadamu kamili inawaletea furaha; Tunaona pia ajabu ya kutembelewa na
wachungaji, na mambo ya hatari ambayo yanaanza kujitokeza kuhatarisha maisha
yake.
Je, wiki hii naweza kuupa nafasi kila wasiwasi
ninaouhisi uunganike na wasiwasi wa Mariamu na Yusufu? Ninaweza kushirikishwa katika uchungu wa
uzazi aliokuwa nao Mariamu katika kujidhatiti kuwa mkarimu kujitolea kusaidia
wengine ili waishi? Naweza kutambua vitanda vya ambapo ninasihiwa
kujilaza kwa furaha? Na naweza kuona vitanda hivi vikibadilika ninapomwangalia
Mtoto Yesu akiwa amelazwa katika kitanda cha yasi horini? Wapo watu maskini au walemavu au wowote
wanaotaabika ninaokuwa nao au kukutana nao maishani ambao wananikumbusha jinsi
gani wachungaji walikuwa na furaha sana walipokaribishwa kushuhudia ukweli wa
kuzaliwa kwa Yesu?
Katika juma hili itahidi kuwa mshiriki katika
matukio yanayosimuliwa uyaelewe kwa kutumia hisia zako hai. Jaribu kuwashirikiwa wengine neema unazopokea
katika ukurasa: Sehemu ya Kuchangia na
Kushirikishana katika mtandao huu.
Yesu Kristu aliyeingia katika maisha yetu katika
ukamilifu wa hali yetu ya kibinadamu na azidi kutusaidia kukua katika kumjua na
kumpenda wakati huu.
Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili
Kutafakari kuzaliwa kwa Yesu kunaweza kuwa tendo
la kufurahisha sana. Zaidi ya hayo,
kufanya tafakari hii katika mazingira ya maisha yetu ya kawaida kunaweza kuwa
chanzo cha nguvu ya kipekee. Katika
usaidizi wa sala juma lililopita tulipata maelekezo ya msingi katika kutafakari
Maandiko matakatifu wakati wa sala, katika hali maalum ya mafungo haya.
Tumezoea sana kusikia simulizi za Krisimasi
(Noeli), na kichwani tuna picha nyingi za siku hiyo ya kuzaliwa kwa Yesu
Kristu. Juma hili na tupenye ndani zaidi ya simulizi ya Noeli kwa kuwa ndani
kabisa ya yale yaliyotokea siku hiyo; tuingie si katika simulizi tu, bali
katika ukweli wa kuzaliwa kwa Kristu, na jinsi ukweli huu unavyotuambia Yesu ni
nani.
Kila asubuhi niamkapo, nitawaza ni kipi napendelea
kiwe katika mawazo na kumbukumbu zangu
siku nzima. Katika siku za kwanza za
juma, naweza kufanya matayarisho ya jukwaa.
Katikati ya juma, naweza kushuhudia kuzaliwa kwa Yesu. Baadaye katika juma, naweza kutenga muda wa
kuwa na Mariamu, Yusufu, Mtoto Yesu na wachungaji wa kondoo. Naweza kufunga wiki kwa kuipitia upya
simulizi ya kuzaliwa kwa Yesu kama ilivyoandikwa katika Injili ya Matayo,
uhasama wa Herodi, wahujaji kutoka Mashariki na familia takatifu kukimbilia
Misri ili kuokoa maisha ya mtoto.
Kama tukipanga vipindi vya sala katika juma hili
na kuvifuata ipasavyo, itakuwa rahisi kuingia katika matukio husika na
kuyatafakari ipasavyo.
Naweza, kwa mfano, kujitafakari kama rafiki wa
Mariamu na Yusufu. Naweza kuwatembelea mara
nyingi wakati Mariamu akiwa mjamzito, na kufurahia kumwona Mariamu akimwimbia
Zuburi mtoto wake, ambaye anasikiliza angali tumboni. Nasikiliza mazungumzo kati ya Yusufu na
Mariamu—mazungumzo yenye ujazo mkuu wa imani kwa Mungu. Namwona Mariamu akipapasa
tumbo lake, kama vile kumtuliza mtoto tumboni mwake kwa imani yeke. Nahisi furaha kubwa pale Mariamu anaposhika
mkono wangu na kuugusisha katika tumbo lake, na nahijisi kuwa karibu sana na
mtoto anayekua tumboni mwa Mariamu. Naweza kuwashukuru Mariamu na Yusufu kwa uwazi wao na “ndiyo” yao kwa
Mungu. Naweza kutoa shukrani zangu kwa
ajili ya kunishirikisha imani yao na furaha waliyonayo kwa ajili ya mtoto wao,
na pia kwa kunipa nafasi ya upendeleo kushuhudia na kuwa mwandani wa familia
hii katika hali hii ya mwanzo. Naweza
kuwaambia lolote ninalotaka kuhusu maisha yangu na yale yanayonikabili leo
hii. Katika sehemu hii niliyofikia
katika mafungo haya, Mariamu na Yusufu wanaweza kuwa marafiki wangu wakubwa
katika safari ya maisha yangu. Labda
nitakuwa nao hapo habari kuhusu sensa inapowafikia. Wanaukabili vipi wasiwasi wao? Naweza
kukumbuka maneno halisi waliyosemezana?
Ninapowasindikiza katika safari yao kwenda
Betlehemu kuhesabiwa, ninaionaje safari hii? Barabara, uchovu, woga, mazungumzo yao: yote nayashuhudia na kuwa sehemu
yake kwa kiasi fulani. Je wanalichukulia
jambo hili tofauti na jinsi nilivyokabili changamoto kama hii katika maisha
yangu? Ni maneno gani ya kiimani mtoto
Yesu anayasikia kutoka tumboni mwa mamaye katika safari hii?
Unaionaje hali yao wanapokosa nyumba ya kulala
ugenini Betlehemu? Mtoto anashuhudia
nini katika maneno “Hapana, hakuna nafasi kwa ajili yako hapa,” “Hapana,
haukaribishwi hapa”, na “Nyumba imejaa”? Naweza kukumbuka maneno yao hasa waliyoambiana wakitoka sehemu moja
kwenda nyingine? Ilikuwaje pale
ilipobidi wajipatie pa kulala katika nyumba ya wanyama? Tumia uwezo wako wa kufikiri na kutafakari,
ukitumia milango yote ya fahamu. Waliona
uzuri wa mahali hapo? Walijua kuwa zizi la ng’ombe lilitosheleza nia yao, tena
kwa ukamilifu?
Naweza kwenda karibu kiasi gani na pale
anapozaliwa Yesu? Naweza kwenda karibu kiasi
ninavyotaka. Kama nimewahi kuwa na mtoto au kuona mtoto akizaliwa, naweza
kutafakari jinsi Mariamu anavyoukaribisha uwepo wangu. Ni maneno gani namwambia? Mariamu anapoingia
katika uchungu wa uzazi, yeye na Yusufu wanaambiana nini? Wanazungumza na mtoto
tumboni mwa mamaye? Naweza kusogea
karibu kiasi cha kuwa mshiriki katika tukio hili na kutambua maana yake? Naweza kumpokea mtoto mchanga anapozaliwa mikononi
mwangu? Mwili wake vuguvugu akiwa na
damu mwili mzima, anavuta pumzi na kutoa kilio huku akiyoosha mikono yake kulia
na kushoto, kama vile kuukuumbatia ulimwengu. Naweza kumfunika asihisi baridi na kumlaza manyasini katika hori la
kulishia ng’ombe? Ndani moyoni, nahisi kuwa yote haya ni yangu; yote haya ni kwa ajili yangu?
Katika siku zinazofuata, tunaambiana nini? Ninapotafakari kuwasili kwa wachungaji pale
alipozaliwa mtoto Yesu wanapata mandhari ya namna gani? Wanapoondoka, naweza kutafakari maneno ambayo
Mariamu na Yusufu wanamwambia mtoto wao kuwa siku moja atajitolea maisha yake
kuleta habari njema kwa maskini?
Kama tukifanya juhudi kupenyeza katika matukio
haya kwa kutumia uwezo wetu wa tafakari
hai, itakuwa rahisi kwetu kuendelea na shughuli na kazi zetu za kila siku
tukiwa na picha hai za matukio haya
mioyoni na akilini mwetu. Matukio ya
kila siku yatakuwa yakishabihiana na yale katika ya uzazi wa Yesu: woga na
wasiwasi, imani, matarajio, safari, matatizo, vizingiti visivyotarajiwa, kukataliwa,
kutokukaribishwa, kufanya mipango mbadala, umaskini, kitanda cha nyasi na
kupokelewa kirahisi. Siku nzima, naweza
kuwa naona na kutambua na kufananisha mambo; huku nikiendelea na mazungumzo,
kumbukumbu ya maneno na utambuzi wa hisia zangu.
Nipokwenda kupumzika kitandani mwisho wa siku,
naweza kutoa shukrani zangu kwa yote niliyopata siku ya leo. Naweza kumwambia Yesu ni kiasi gani ninatamani
kuwa naye katika utume wake, kwa kuwa mapendo yangu kwake yanakuwa dhahiri
zaidi anaponipa nafasi ya kumjua zaidi.
Kwa Ajili ya Safari: Unaona Nini?
Juma hili tunaangalia na kusikiliza simulizi zaidi
ya Mungu mwenyezi kuwa kitoto kichanga. Yote si tulivu na angavu pale Yusufu na
Mariamu wanapoanza safari kwenda Betlehemu. Kuna mwanga wa kutosha, ila hakuna utulivu katika nyumba ya wageni
ambapo wanakosa nafasi. Yote si angavu
katika banda la wanyama ambapo wanapata nafasi, ila wanapata utulivu baada ya
safari ndefu.
Tupo na Yusufu, mume ambaye hawezi kufanya yote
anayohitaji mkewe wakati huu. Tunamwona
akihangaika kutenda hili na lile—akiwasha moto ingalao mtoto na mzazi wasipate
baridi sana, na pia tunamwona akijitahidi kulisafisha zizi la ngombe ili lifae
zaidi kuwa pango kwa familia yake hii changa. Tunauhisi ukimya wa usiku, ukimya wa muda kama vile saa haisongi
mbele. Ukimya huu ni sauti ya yule Asiye
na Kikomo cha Muda, ambaye ameingia katika ulimwengu wetu sisi tulio na kikomo
cha muda.
Umeketi au umesimama wapi? Unamwangalia nani kwa ukaribu? Unavutiwa na hawa wanadamu wawili
wakimstaajabia mwanadamu wa tatu ambaye sasa ametulia katika hori la kulishia
Ng’ombe? Unavutiwa kusogea karibu na walipo au unasukumwa kutoka nje? Mariamu anakwambia chochote kwa
maneno au kwa ishara?
Na sasa ukimya unaisha kwa kuwasili kwa wachungaji
wa kondoo. Wameuona mwanga, na
kugutushwa na malaika waliokuwa wakiimba wimbo wa amani duniani. Unavutiwa kuwaambia chochote kuhusu uliyojionea? Je, hapo pamekuwa mahali pa kushangaza na
penye mengi ya kutafakari? Mariamu ameketi hapo akishuhudia yote na
kuyachanganua na kuyatunza moyoni. Alikuwa kalisemea ndiyo fumbo
hili alipoamini ahadi ya Mungu. Tayari
kashuhudia sehemu kubwa ya fumbo hilo usiku huu. Maswali yote ya “Ni ni hiki hasa?”,
“Kulikoni?” na “Itawezekanaje?” yanasukumana rohoni mwake; ukipenda unaweza
kuketi karibu naye ukiwa na “ndiyo” yako uliyoitoa pamoja na “Nitendewe
anavyotaka Mungu.”
Mtakatifu Inyasi anatusishi tuwe wawazi mbele ya
Mungu, ili kwamba tuweze kupata neema ya kumshuhudia Mungu kwa uwazi anaopenda
kutufunulia anapotuita. Tunajua vema
historia ya ukombozi wetu, ila kila tunaposali inakuwa zaidi na zaidi mali yetu
na sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Hivi ndivyo Mungu anavyotueleza sisi ni nani na jinsi gani tupo katika
mawazo yake na mpango wake. Sehemu ngumu
ya tafakari hii ni kuizoea. Kwa kuwa
watulivu, katika ukimya wa usiku huu, sala zetu zinaturudishia katika hali mpya
ule mwangaza ambao wachungaji waliusikia:
Leo hii, mtoto amezaliwa ambaye anatuletea amani ulimwenguni; Amani kwa wote
wanaobarikiwa na Mungu; Amani kwa wote wenye mapenzi mema. Amani, kwa Mtakatifu Inyasi, ni kwa wote
ambao wanafurahia na kuburudishwa moyoni au kupata faraja kama matokeo ya
tafakari zao za mafumbo matakatifu ya Mungu katika Neno lake, viumbe vyake au
matendo yake tunayoyashuhudia kila siku katika maisha.
Tunamjia tena huyu mama mjamzito na mtoto wake
atakayejifungua. Tunasogea karibu naye
au tunakaa kwa umbali kidogo kwa kadiri tunavyotaka. Tunasali tukiwa katika hali ya uwazi kama
vile mabanda tupu ya wanyama yanayongojea ukimya na mwangaza mpya uyajie na
kuyabariki.
Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...
Yesu Mpendwa,
Nadhani ni harufu mbaya muozo wa nyasi za kulishia
ng’ombe ndio unaonifika kwa uzito zaidi. Najikuta nimesimama kwenye baridi nje ya zizi la ng’ombe, nikichungulia
ndani kupitia ufa mkubwa katika zizi hilo. Kuna mwanga hafifu ndani, ila unanitosha kuona yote yanayotokea ndani ya
zizi.
Sala hii imekuwa safari ya kufurahisha na
kusisimua. Safari hii imekuwa sala ya
kufurahisha na kusisimua. Niliwatazama Yusufu na Mariamu wakisafiri kwenda
Betlehemu. Mariamu alikuwa
amekwishasaidia wengi waliozalia majumbani, lakini kwa sasa wakati wake
unapokaribia hakuna mwanamke yeyote aliyenaye na anakuwa na woga kiasi. Hakuwa amepata muda wa kumjua Yusufu kwa
undani, ila alimpenda na kumwamini. Kwa miezi kadhaa, walikuwa wameshirikishana
yaliyokuwa katika mioyo yao hasa walipozungumza kuhusu ujauzito wake, wasiwasi
wa Yusufu, imani yao kwa Mungu isiyotetereka, na uamuzi wa Yusufu kuwa na
Mariamu kuendelea na Mariamu katika ndoa na kuwa naye katika yote. Yote hayo yalifanya kukomaa kwa muungano wao
na kuwa na nguvu zaidi kuliko uletwao na mapenzi ya wawili walioana hivi
karibuni.
Sasa ninaposali nikitafakari tukio la uzazi wa
Yesu, nakutana nao katika zizi la ng’ombe na harufu isiyo nzuri ya nyasi za
kulisha ng’ombe zilizooza ya kinyesi cha ng’ombe. Inawezekanaje uzae mtoto hapa, katika nyasi za kulishia ng’ombe zenye uvundo uletao harufu
mbaya? Inawezekanaje mwana huyu mtukufu azaliwe hapa katika zizi la ng’ombe ambapo kinyesi cha wanyama hawa
kimetapakaa kila mahali?
Ninachotaka hasa ni kwenda katika lile zizi na
kuwasaidia. Nitaweza kweli? Ee Yesu, naweza kusali kwa kutafakari na kuwa
na hali ya kutojijali hata kuweza kuingia huko zizini? Naingia na wote wawili wanaelekea kufurahia
kuniona. Mariamu ananikaribisha na
kunishukuru kuwa nao hapo. Yusufu
amekuwa akishughulika kusafisha sehemu ambapo Mariamu angeweza ingalao kujilaza. Anapoanza kupata uchungu mkubwa wa uzazi,
namshika mkono kwa nguvu kumwashiria nipo hapo, nipo pamoja naye. Lakini humu ndani kunanuka sana! Ee Yesu, uliwezaje kuzaliwa sehemu panaponuka
namna hiyo! Nilianza kujaribu kuleta
nyasi kavu ili kuzisambaza zifanye kirago kwa Mariamu, ila mara alianza kujifungua na ni mimi tu niliyeonekana kujali
kuhusu nyasi kavu.
Ndipo ulipozaliwa katika nyasi tepetepe
zilizonuka, na kupokelewa na mikono yenye nguvu ya Yusufu. Alikupangusa uso na kusafisha pua yako na
nacho na mara ulipotoa kilio kikali, wote walicheka. Nami nilicheka pia kwa sauti ya chini, ila
sikutaka kuwaingilia katika hali yao wakati huu walipoonekana wazi jisi walivyohusudiana, hivyo nilijiweka
pembeni kidogo. Ee Yesu, tazama moyo
wangu unajazwa na uwepo wako! Kuzaliwa
kwa mtoto yeyote katika mahali kama hapa kunashangaza, sembuse wewe Muumba wa kila kitu. Pana baridi
kali hapa, pananuka na hata hakuna kitanda wala blanketi kwa ajili yako
kitoto? Yusufu kakufunika kwa joho lake,
ila naona unahitaji kufunikwa zaidi.
Sasa natambua uchovu mkubwa wa Mariamu na Yusufu
baada ya safari ndefu, ila pia naona waziwazi jinsi wanafurahia sana kuzaliwa
kwako usiku huu. Mariamu anaposinzia
akiwa kakubeba, anafumbua macho yake mara. Naweza kukupakata wakati Mariamu na Yosefu wakiwa wamelala? Ni ajabu sana kuaminika kiasi hiki! Naketi taratibu katika nyasi ambapo sitakuwa
nikiwasumbua, na nakupakata ukiwa umefunikwa joho la Yusufu. Nakuangalia, nanusa shingo yako ya kitoto,
nakupapasa mashavuni kama nilivyozoea kuwafanyia watoto wangu binafsi. Nahisi upendo mwingi kwako na kwa yote ambayo
umefanya. Unakuja ulimwnguni katika hali
kama hii—katika hali hii duni ndani ya zizi la ng’ombe linalonuka. Unafanya haya yote ili kuwa nasi katika sehemu
ya maisha yetu iliyo duni na yenye kunuka.
Yesu mpendwa, nijengee moyo wa unyenyekevu kama
wako katika majuma ya mafungo yanayofuata. Nipe uwezo wa kuhisi unyonge wako na kutambua unyonge wangu na
kujisalimisha katika unyonge huo kama ulivyofanya. Nisaidie niwe mdogo katika ulimwengu huu na kuwa hapa kwa ajili yako, japokuwa
hii inashangaza kwa kuwa ni wewe uliye hapa kunisaidia. Amina.
Maandiko Matakatifu:
Matayo 1:18-24
Luka 2:1-21
Matayo 2:1-12
Matayo 2:13-23
Zaburi 98
|
MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO