JUMA LA MARUDIO
Kutua kwa Muda Ili Kukagua Neema
Tulizopokea
Mwongozo: Kufanya Tathmini
Katika Mazoezi ya Kiroho, Mt. Inyasi
anawasisitizia waongozi wa wale wanaofanya Mazoezi kuwakumbusha wanaofanya
Mazoezi kuwa ni vema “kubaki” pale “wanapopata matunda.” Majuma yaliyopita ya mafungo haya yamekuwa
chanzo cha neema zenye nguvu. Juma hili
la marudio halianzi mada mpya. Mada ya
juma hili ni tafakari ya neema tulizopokea katika majuma kadhaa yaliyopita.
Baada ya kujijua kuwa sisi ni wadhambi tunaopendwa na Mungu, tulipata neema ya kualikwa kumfuasa
Yesu. Tunakumbuka miitikio yetu binafsi
ya kumfuata, na kuongezeka kwa shauku ya kumjua na kuwa na Yeye aliyetupenda
kiasi kikubwa sana. Tumeanza kumpa
nafasi atuelezee mpango wa Mungu na maisha yake. Tulishatafakari mwito wake na
jinsi Mungu alivyotayarisha ujio wake kuanzia enzi za Agano katika Maandiko ya
Wayahudi. Kisha tuliingia katika
simulizi za wazazi wake, na wale waliowazunguka katika maisha, wakati
alipotujia kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mwishowe tumejikuta tukiwa ndani ya banda la wanyama, pale anapozaliwa
kwa ajili yetu.
Juma hili la mafungo tunakaribishwa kubaki hapo
kwa muda kiasi. Labda tumekuwa katika
harakati nyingi sana kiasi cha kushindwa kukamata yote yaliyofunuliwa kwetu. Yawezekana
pia tunashindwa kuona kufanana kwa kuzaliwa kwake katika hali duni ya zizi la
ng’ombe na kutujia katika umaskini wa
maisha yetu.
Tunapoamka killa asubuhi juma hili, tutapitia tena
neema fulani ambayo kwayo tunamshukuru Mungu. Yaweze kuwa neema moja juma zima. Yaweza kuwa kufanya jambo lisilo na vipengele
vingi kama vile kufanya makazi yetu
katika zizi lile la ng’ombe ili kuwa na Yesu mahali hapo.
Neema tunayotamani juma hili ni kuingizwa ndani zaidi katika nafsi ya Yesu
Kristu. Juma hili tutapata misaada ya kuanza, ya kuingia ndani zaidi, na ya
kutusaidia kupata maneno kwa ajili ya sala.
Tafakari zetu zitakuwa sehemu-fiche, lakini hai,
katika kila linaloendelea katika maisha yetu kila siku juma hili. Lolote tunalokabili kila siku katika wiki hii
linaweza kuwa sehemu ya mafumbo ambayo tumekuwa tukitafakari, iwapo
tutaliruhusu liwe. Tukio lolote katika
maisha ya mtu ni tukio ambalo Yesu Kristu amekuja kuwa sehemu yake. Juma hili tunashuhudia upendo wa Mungu
ukiingia ndani kabisa ya nyoyo na maisha yetu.
Mwishowe, kila jioni katika juma hili, tunatoa
shukrani zetu kwa ajili ya neema mpya tunazopokea. Kwa ingalao muda mfupi kila siku, labda
tunapobadili mavazi ya kazi ili kupumzika kitandani, tunaweza kuinyanyua mioyo
yetu kwa shukrani kwa Mungu kwa ajili ya misukumo ya kiroho siku hiyo—misukumo
ambayo inayotuunganisha na Yesu ambaye amekuja katika ulimwengu wetu kuwa mmoja
wetu katika ubinadamu, na kutukaribisha kujiunga na utume wake.
Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili
Kulianza juma hili sharti kwanza tujue wazi tofauti
kati ya juma hili na majuma mengine yaliyotangulia. Juma hili ni la kufanya marudio, kusita
kidogo tulipofikia ili kupata muonjo kamili wa neema tulizopewa, au kuzipa
nafasi zaidi zipenyeze katika sehemu zote za maisha yetu. Hatufanyi mazoezi yote ya majuma yaliyopita,
bali kuhakikisha tumepokea kwa ukamilifu zaidi neema za Mungu katika majuma
yaliyopita kwa kuziona, kuzitambua, kuzipa
majina na kuzipokea ziwe zetu zaidi au ziwe sehemu ya maisha yetu, kama
Mungu anavyotaka. Hivyo basi ni wazi kuwa
hatufanyi marudio haya kwa kuwa hatutaki kuendelea mbele, na mtazamo wetu upo
zaidi katika neema tulizopokea kuliko katika mazoezi tuliyopitia kuzipata neema
hizo. Hivyo basi, mfano mzuri tunaoweza
kuutumia hapa sio wa kusoma kitabu kizuri, kisha kurudia kukisoma chote mara
nyingine. Mfano mzuri wa tunayofanya
juma hili ni kama hivi: Rafiki yangu ananionyesha albamu ya picha za familia
yake, na ananionyesha kwa kasi hasa kurasa za awali. Namwambia rafiki yangu apunguze kasi ya
kunionyesha picha na kumwambia: “Hakika picha hizi ni za kufurahisha. Hebu tuuangalie tena ukurasa huu. Nafurahia hasa kuziangalia picha hizi hapa
kwa umakini zaidi. Tazama jinsi baba na
mama yako walivyokuwa vijana! Na hii ni
nyumba ambapo uliishi utotoni? Tazama
jinsi macho ya baba yako yalivyokuwa makali, labda hata sasa ni miwani yake tu
inayaficha! Na picha hii inaonyesha wazi
jinsi ulivyo, japokuwa hapa ulikuwa bado kitoto kichanga.”
Kama tulivyoelezewa maana hasa ya marudio katika
mafungo hapo juu, ni wazi kuwa njia nyingine ya kuelezea tunachofanya juma hili
ni kwa upande wa sala za juma hili. Kama majuma mengine katika mafungo haya,
juma hili tunasali, lakini siyo kwa kuchukua mada mpya za kusalia, bali kwa
kutumia neema tulizopokea katika majuma yaliyopita. Napokea neema niliyozawadiwa au nachukua
neema niyokwishapokea na kuipenyeza kwa undani zaidi, kisha natulia ndani ya
neema hiyo nikifaidi utamu wake. Tunafanya hivi kwa kuwa tunajua kuwa daima
kuna zawadi nyingine ndani ya zawadi tulizopokea. Basi juma hili tutaziweka mbele yetu zawadi
(neema) tulizopokea, na tutazifungua ili kugundua zawadi nyingine ndani ya
hizi, ambazo pia tunakaribishwa tuzipokee ziwe zetu.
Hivi basi ni hatua muhimu ya kuonyesha moyo wa
shukrani zaidi kwa zawadi tulizopokea—kujua hasa ni nyingi kiasi gani, thamani
au umuhimu wake kwetu, na maana yake katika maisha yetu. Shukrani yetu haiwezi
kuwa kamilifu ikiwa hatujui hasa ni nini tulichozawadiwa. Hili ni zoezi muhimu sana kwa kuwa tunafanya
mafungo haya katika hali ya kuendelea na shughuli zetu za kila siku, zenye
changamoto zinazoweza kutufanya tusione na kupokea yote tunayopewa. Iwapo neema za majuma yaliyopita, kwa mfano:
mwito na mwitikio, ufahamu wa Mpango wa Mungu katika maisha yangu, utambuzi wa
umwilisho wa Mungu kwa ajili yangu—zimekuwa zawadi katika maisha yangu halisi,
basi zitakuwa na maana katika maisha yangu halisi:
Kila siku ya juma hili, naweza kuchukua nyia
tofauti ya kufanya marudio: kubaki katika sehemu fulani yenye zawadi zaidi,
kuingia ndani ya neema fulani ili kupata muonjo wa zawadi ya Mungu kwa
ukamilifu zaidi katika safari hii maalum ya kumwona Yesu kwa udhahiri zaidi,
kumpenda kwa undani zaidi na kumfuasa kwa ukaribu zaidi, siku baada ya siku.
Kwa Ajili ya Safari: Usiharakishe Kuondoka
Mtakatifu Inyasi angependelea tutue na kukaa kwa
muda katika ufukara na unyenyekevu wa zizi la ng’ombe alimozaliwa Yesu. Mtoto Yesu anaanza kutoa maelezo yahusuyo
utambulisho wake—maelezo yatuambiayo yeye ni nani. Matukio ya humu zizini na hali inayotuzunguka
ni maneno muhimu ya sentensi yake ndefu ya mapendo.
Tunapokaa humo tukiangalia yote, tunaweza kupitia dukuduku
lolote tulilonalo kuhusu uwepo wetu humo ndani ya zizi. Uwepo wetu karibu naye
haukwepeki iwapo kweli tunataka kuzijua njia zake. Tuna haraka gani? Tunamwangalia na kusikiliza. Katika fikra zetu, tujiundie picha za rafiki
zetu wakija kututembelea hapo zizini ambapo tumechagua kubaki kwa muda na
mtoto. Tutawaeleza yapi kuhusu yale
tuliyoshuhudia kwa macho, masikio na uwepo wetu humo zizini? Labda katika sala tunaweza kujisikia kutaka
rafiki zetu wa zamani wakutane na hawa rafiki zetu wapya. Tunahisi furaha na faraja moyoni tunaposogea
karibu na pale Mariamu alipo kampakata mtoto? Tunajihisi kuwa na heshima kiasi gani kwa Yusufu baada ya kushuhudia
jinsi alivyoshughulikia tukio lote la uzazi wa mtoto—heshima hii inanifanya
nihisi nini moyoni pale tunapoketi na Yusufu kuzungumza na wageni?
Kuna njia za kupata ukweli na njia tofoauti ya
kukua katika kujua watu. Yesu, Mariamu
na Yusufu ni watu na Mt. Inyasi anatutaka tujitambue pia kuwa watu, na kama
watu kuwa na uhusiano wa nafsi kwa nafsi na hawa tunaokutana nao hapa katika
banda la wanyama, na wote tutakaokutana nao katika majuma yajayo. Kuwa na uhusiano binafsi ni kujuana nao si
kwa kutegemea kila kilichoandikwa au kusimuliwa na wengine, bali katika
kuwaangalia, kuwasikiliza na kuwa karibu nao au kwa kifupi kujenga urafiki nao.
Hata hivyo hili halitokei mara. Katika
njia ya kuwa marafiki, tunapitia hatua mbalimbali. Yote huanza kwa kuangalia na kusikiliza na
kupokea yoyote tunayopewa. Tonaingia
katika hatua ya kuwa watu wanaoelewana,
halafu tunakuwa marafiki na kisha tunakuwa karibu zaidi kuliko marafiki,
tunakuwa wenzi (waandani) au
washirika. Siku hizi tunajiweka wazi
kuguswa moyoni na yale tunayoyaona na kuyasikia.
Ni muhimu kwetu kujikawiza kwenda mbele kwa kuwa
ndani ya banda hili la wanyama, na kuanza kusogea taratibu kuelekea siyo tu
lilipo hori la kulishia ng’ombe na alimo mtoto, ila pia ulipo ukweli wa tukio
ambalo linaamua hatima ya ulimwengu mzima. Ni kipi cha maajabu ya Mungu wetu
kinadhihirishwa kwetu katika hali hii ya kimaskini? Mungu mwenye upendo mkuu anaukumbatia ulimwengu kutokea hapa
katika zizi dogo la ng’ombe na kuifikia hata sayari iliyo kubwa kuliko
zote. Mungu huyu anakuja katika zizi la ng’ombe la kila mmoja wetu kama
kuna nafasi ambamo anaweza kumkaribisha. Hajali hata kidogo uchafu na harufu ya zizi hilo. Hii ni kusema, baada ya Betlehemu, hakuna
jipya tena la kuonekana bali kueleweka. Uamuzi wa Mungu siyo uamuzi wetu. Njia ya Mungu daima iko juu zaidi na kwa
uamuzi wake, yaliyo muhimu ni yale yaliyo duni zaidi, na ni katika hali na
sehemu duni ndipo ambapo wale tu walio wanyenyekevu wanaweza kuona na kuamini.
Hivyo tunaketi kwa muda kidogo katika rundo la
nyasi za kulisha ng’ombe, na kuanza kukubali. Kwanza tunaanza kumkubali yeye, na kumkubali kwetu kunaongezeka kila
siku katika mazizi yetu. Tunalikubali fumbo la ujio wake na ukweli
kuwa haikuwa jinsi tulivyotarajia, kupanga wala kuamua—ni uamuzi wake. Tunakubali kuwa tunapendwa na Mungu kwa namna
ya ajabu. Tunaanza kukubali kuwa njia za
Mungu zinaanza kutuvutia. Tunakubali kuwa
tunahitaji kuongeza kidogo muda wa kuwa hapa ili kuangalia jinsi roho zetu
zilivyoguswa na kunyanyuliwa na ujio wake katika namna tunayoshuhudia.
Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...
Yesu Mpendwa,
Nipo nyumbani. Nimetulia humu zizini nikiwa nawe
na Mariamu na Yusufu. Kuna baridi na
harufu mbaya na nimesimama penye kinyesi cha ng’ombe, yawezekana pia nilikalia
kinyesi cha ng’ombe bila kujitambua. Hata hivyo nina furaha kubwa isiyo kifani.
Ni kama vile mara nyingi sipo tayari kukukaribisha
kwangu. Nahisi kuna wakati nimekuacha
ukingoja nje kabla ya kukuruhusu uingie ndani; nimekuacha nje hadi nilifagie banda langu, nipate nyasi safi na
kavu, nisafishe soli za viatu vyangu na kuweka tayari nguo za joto kwa ajili
yetu sote.
Ningependa kuwa mwema zaidi. Hilo ndilo ninaloona
katika giza la banda hili, giza la moyoni mwangu. Sizungumzii mazingira ya hapa nilipo, ee
Yesu, najizungumzia mimi na nafsi yangu. Nina wema wa kutosha kuwa mahali hapa
nawe? Ni sasa tu ninapokuangalia wewe na wazazi wako ndiyo nahisi mapendo
makubwa kwako—katika baridi na giza la humu kwenye zizi la ng’ombe. Mikono yako midogo bado imekunya ngumi ya
mtoto mchanga, na nipokusogezea kidole changu, unakikamata kwa nguvu: Bwana na
Mwokozi wangu anaushika mkono wangu! Najawa na furaha moyoni hadi machozi ya
furaha yananibubujika muda huu ninapojihisi kuwa rafiki wako wa ndani moyoni.
Mpendwa mtoto Yesu, kutoka mwanga hafifu wa humu
kwenye zizi la ng’ombe nisaidie kuchungulia na kuona ndani ya giza la moyoni
mwangu. Nijalia kujihisi kwa undani
zaidi kuwa hapa nipo nyumbani. Hapa mafanikio yangu makubwa kuliko yote ni
kukupa kidole changu ukishikilie na kuking’ang’ania kitoto. Nisaidie nielewe
kuwa hukuja kuwa nami katika hali iliyo na ukamilifu bandia, bali kuwa nami
kama nilivyo sasa hivi: nyayo zikiwa zimezama katika mbolea ya ng’ombe, machozi
yakibubujikia uso wangu wenye mavumbi, na kwa furaha natabasamia wazazi wako
wanaosinzia karibu na ng’ombe mmoja na fahali wawili!
Yote haya hayaelekei kuendana na maisha yangu
yaliyo katika mpangilio, hata hivyo nipo hapa katika hali isiyo kamilifu yenye
kile kinachoonekana kuwa furaha kamilifu. Moyo wangu umejawa shukrani nyingi kwa ajili yako, na kwa mapendo
nainama kukutazama usoni. Asante kwa
kuwa wa maana kubwa sana maishani mwangu. Asante kwa kunijia, na kutujia sote tukiwa katika mazizi yetu ya
wanyama, tukiwa tumesimama gizani, tukiwa hatujui hasa nini cha kufanya.
|
MAFUNGO YA KIROHO KUPITIA MTANDAO