JUMA LA KUMI NA SITA
Maisha Nje ya Hadhara kwa Miaka Thelathini
Mwongozo: Mwana wa Seremala
Mojawapo ya ukweli wa kushangaza sana
kumhusu Yesu Kristu ni kuwa tunajua kidogo sana kuhusu maisha yake katika miaka
thelathini ya mwanzo wa maisha yake. Tunajua alipoanza kazi yake hadharani,
wali walimjua yeye na ndugu zake walishangazwa sana. Kwa dharau wengine walitoa mashambulio yao
dhidi yake wakisemezana: “huyu siye yule mwana wa seremala?”
Juma hili la mafungo linatupa muda wa
kumjua Yesu anayekua katika ubinadamu wake (anayeongezeka umri). Kwa kuwa kuna Maandiko machache sana ya
kurejea kuhusu maisha yake kati ya kuzaliwa kwake na kubatizwa kwake, tutatumia
ubunifu wetu kujazia sehemu zile ambazo hatuambiwi mengi na maandiko—ila
tunajua kweli mbalimbali za historia ya wakati huo, kazi ya baba yake, imani na
tamaduni za watu wake, n.k. Zaidi, kama tukiifikiria hali ya utu-uzima ambayo
Yesu alifikia, tunaweza pia kutafakari jinsi utoto wake ulivyokuwa, alikuwa mtoto
wa namna gani, mambo gani alipambana nayo katika maisha na fikara, ni maamuzi
gani hasa alifanya, n.k. Kwa kutumia kile tunachojua kuhusu maendeleo ya watoto
hadi kufikia ujana, halafu kufikia utu uzima, tunaweza kufanya ubunifu mzuri
kuhusu mambo kadhaa ya kibinadamu ambayo sharti Yesu aliyakabili. Tukisali
namna hii tuingie katika zoezi la kumjua kwa undani zaidi, ili kwamba tuweze
kumpenda zaidi na kufikia shauku yetu ya ndani kabisa ya kuwa naye katika utume
wake aliopewa na Mungu Baba.
Tufungue mioyo yetu ili tuonyeshwe jinsi
ilivyokuwa miaka ya utoto wa awali wa Yesu. Tunaweza katika juma hili kuenenda tukitafakari magumu yote ya
kibinadamu yaliousibu utoto wa Yesu? Na tunapofikia miaka yake ya kubalehe na
ujana, tunaweza kumpa nafasi atuambie aliipitia vipi na kuwa mtu tunayemjua
sasa. Tunaweza kutafakari mahangaiko na
harakati alizokuwa nazo? Vipi kuhusu
maswali aliyojiuliza? Yapi yalikuwa
mazito kwake? Wapi alikuwa na nguvu na wapi alikuwa na madhaifu? Tunaweza
kudhani mahusiano yake na watu katika hatua mbalimbali za kukua kwake?
Kama tunaweza kupata mengi kumhusu Yesu
katika miaka yake ambayo haonekani hadharani, tunaweza pia kujifunza mengi
kuhusu jinsi Mariamu na Yusufu walivyomlea. Tunaweza kutafakari jinsi maisha katika mji wa Nazareti yalivyokuwa.
Tunajua kuwa Yesu alijiona na kujijua kama
aliyeitwa kutangaza wokovu kwa wote utumwani na kutangaza Habari Njema kwa
maskini. Tunajua kuwa alitambua kubarikiwa
kwa aliye maskini wa roho. Tunajua kuwa
alijua kuwa utawala wa Mungu ni kama chachu ya kuumulia unga au mbengu ndogo,
na kuwa magugu na ngano sharti vikue pamoja. Tunajua kuwa hakuogopa kula na kunjwa pamoja na wenye dhambi na wale
ambao welikwepwa na kutengwa na viongozi wa dini. Tunajua kuwa alijiona kama
mtumishi, mwoshaji wa miguu ya watu, na mkate ambao utamegwa na kutolewa [kafara]
kwa ajili ya maisha ya ulimwengu. Ilikuwaje mwana wa seremala ayafikie haya yote?
Hakika mtu anayetupenda atatuonyesha yeye
ni nani, atatupa nafasi tumpende zaidi kuliko tunavyoweza kudhani na kutuvutia
kumfuasa kwa karibu zaidi, siku baada ya siku, wiki baada ya wiki.
Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili
Kutafakari maisha ya Yesu yaliyojifichika
kunaweza kuwa na changamoto nyingi mwanzoni. Tunaweza kuogopa kwa sababu ya kutokuwa na simulizi za kutosha za
maandiko matakatifu kuhusu sehemu hii ya maisha ya Yesu, hivyo tafakari yetu
inaonekana tofauti na tuliyozoea ya Neno la Mungu tunalosoma kutoka katika
Biblia. Ila kwa kutumia uwezo wa
udhanifu wetu na uhuru tulionao—na kwa kutumia nguvu tunayopata baada ya
kuguswa na Yesu ndani mioyoni mwetu—juma hili linaweza kuwa na uzuri wa
kustaajabisha. Zaidi, kufanya mazoezi
haya katika mazingira ya maisha na mishughuliko yetu ya kila siku kunaweza kuwa
chanzo cha neema zenye nguvu. Zana za
Kukusaidia katika majuma mawili yaliyopita zilikuwa na ushauri wa msingi kwa
ajili ya kusali kwa kutafakari aya za Maandiko Matakatifu, katika kipindi
maalum cha sala na pia katika hali ya kawaida ya kuendelea na maisha ya kila
siku.
Tunaweza kuanza kwa shughuli ya ndani ya kukusanya habari yakini. Tunajua nini kuhusu jinsi watoto wachanga
wanaendelea kuwa watoto wavulana au wasichana wadogo, na jinsi wavulana watoto
wadogo wanavyokua kufikia muda wa kubalehe, kisha kuwa kufikia ujana na
mwishowe kukomaa katika utu uzima? Tunajua kuwa hatua za kukua zinahusisha changamoto na migogoro
mingi. Tunajua kuwa katika haya yote
wazazi ni wa muhimu sana. Tunajua pia kuwa marafiki wa rika moja ni muhimu
katika kukua. Zaidi, tunajua kuwa uamuzi
wa awali wa mwelekeo wa maisha yetu hutuumbia mazingira ya baadaye ambapo chaguzi
na maamuzi mbalimbali hutendeka. Yesu,
hakika alipitia hatua zote hizi katika kukua kwake. Mwinjili Luka anatuambia, “Mtoto Yesu
alipokuwa akikua, alijawa na busara na baraka ya Mungu ilikuwa naye” (Luka
2:40).
Sasa kuyaweka katika umbo yote tunayokusanya kuhusu miaka ya kukua kwa Yesu Kristu,
tujaribu kuangalia alikuja kuwa mtu wa namna gani. Ukweli ni kwamba zoezi hili huwa tunalifanya
kila mara. Tunamwangali mtu, hasa mtu
tunayemchukia au yule ambaye tunadhani hajakua
mtu mzuri kiasi cha kutupendeza, na tunaanza kufanya dhana au ubunifu wa
jinsi utoto wa mtu huyo ulivyokuwa. Pia
tunaweza kukutana na mwanafunzi mwenzetu chuoni ambaye ana kila tabia tunayodhani
ni nzuri, na kujiambia kuwa wazazi wake sharti walitenda vema katika kumlea.
Injili inatusaidia kujua Yesu ni nani leo
hii. Ni nani huyu anayenipenda mimi leo,
Yesu ninayezungumza naye katika sala na aliye na makovu na matundu katika
viganja vyake? Tunajua hawakwepi
wadhambi na wanawake na wengine ambao jamii ya wakati wetu haiwapi nafasi vya
kutosha. Tunajua kwamba anayajua maisha ya kila siku: kwa mfano alitumia mifano
iliyohusiana na kuoka mikate, ukulima au utunzaji mimea, kualikwa na kwenda
harusini, na kuhusu jinsi watu hutupata mali na kuitunza.
Sasa tupo tayari kuziweka katika uhalisi
tafakari zetu kwa kuunda matukio. Tunaweza kuanza kwa kuitengeneza picha ya
jinsi nyumba ya Mariamu na Yusufu ilivyoweza kuwa. Inasaidia kupata habari nyingi na kwa
kinaganaga iwezekanavyo. Ina vyumba
vingapi? Vyumba vina ukubwa kiasi gani? Ni nini kinachotendeka katika kila chumba? Kuna samani gani katika kila chumba? Ni wapi wanapolala, wanapolia chakula,
wanapopikia, wanapokaribishia wageni? Ni wapi ilipo karakana ya useremala ya
Yusufu? Karakana ya Yusufu ikoje? Kisha tunaweza kuunda picha ya mpangilio wa mji
mdogo Nazareti. Watoto wanacheza
wapi? Kisima cha maji kiko wapi? Sinagogi wanapoenda siku ya Sabato lipo wapi? Soko la mji liko wapi? Na ukumbi wa harusi
upo wapi? Makaburi yao yako wapi?
Sasa tupo tayari kuyatazama matukio ya
kawaida ambayo hakika yalitokea katika maisha ya Yesu. Jinsi tunavyoyadhani na kutafakari uhalisi wa
maisha ya Yesu, tuingie ndani yake hadi kuwa sehemu ya wahusika katika matukio
ya maisha yake, tukiyaishi matukio katika maisha yake na kujifunza mengi kumhusu
Yesu, na kumsikiliza akituambia lolote analotaka kutufunulia. Tunawea kujiundia picha ya mgogoro au tatizo
lolote maishani, kuchanganyikiwa kunakotokea wakati ambapo inabidi tuchague
njia fulani ya maisha ambapo gharama yake ni kuacha au kupoteza chaguo jingine;
au pia tunaweza kuchukua jambo lililowahi kutugusa sana moyoni katika maisha
yetu. Uzuri wa namna hii ya tafakari ni
kuwa siyo kila kipengele chake kinapaswa kuwa na ukweli kamili wa kihistoria. Mada tunayoishughulikia inatupa mazingira na mlango wa kuingia katika sehemu ya
kukutania na kuzungumza au kuwa na Yesu uso kwa uso.
Kuna matukio mengine zaidi ambayo tunaweza
kuyajenga au kuyaendeleza: hapo mwanzo kabisa wa maisha ya mtoto Yesu ambapo
Mariamu na Yusufu walikuwa wakijifunza kumtunza Yesu, kumlisha, kumvika mavazi
ya kitoto; Matukio ya kumfundisha kuzungumza na kutembea; Matendo iliyobidi
wayafanye kumfundisha Yesu, kumsahihisha, kumfunza nidhamu; Matukio ya mezani walipokula chakula,
nyumbani alipocheza na kuigiza watu mbalimbali waliomvutia, muda wa
kusali; Yesu akijifunza kusoma; Wakienda
naye kwa mara ya kwanza katika sherehe ya harusi, wakienda naye kwa mara ya
kwanza katika mazishi; Yesu anapoanza kwa mara ya kwanza kusaidia katika
karakana ya useremala; Yesu anapokuwa kwa mara ya kwanza katika kikundi cha
marafiki wavulana wadogo, migogoro midogo midogo inayotokea katika kikundi chao
cha urafiki; Baada ya kubalehe—Yesu
anapokutana kwa mara ya kwanza na wasichana na mambo aliyoyakabili katika muda
huu wa maisha yake; jinsi familia yake ilivyotatua migogoro ya kawaida kati ya
familia yake na ndugu au majirani; Yesu kama msaidizi wa fundi seremala,
aliposaidia katika kupeleka kazi kamilifu kwa waliagiza au walionunua,
alipojenga nyumba; jinsi familia
ilivyoshughulikia masuala ya kuzeeka, kuumwa na kufariki kwa Yusufu.
Hapo mwanzo ilionekana kuwa hakukuwa na chochote cha kutafakari, kwa
sababu ya ukweli kuwa maisha yake
yalikuwa yamefichika. Sasa tunaona katika muda huu kuna mengi sana
ya kujifunza kumhusu Yesu. Hakuna hata
mmoja kati yetu anaweza kupata muda kwa ajili ya yote haya, hususan juma hili,
ila ni neema kubwa kupata mlango wa kuingia katika maisha ya Yesu na kumpa
nafasi atuambie jambo kujihusu yeye mwenyewe. Hii inawezekana hata katika harakati nyingi za kazi na maisha yetu kila
siku kwa kadiri tunavyoendelea kuvutiwa na Yesu.
Katika juma hili fikara na tafakari zetu
zijazwe na yote tutakayopitia kuhusu maisha ya Yesu na nafsi ambayo maisha yake
yalimjengea. Tunapoliishi juma hili la
mafungo, tutaona kuwa, kuunganisha kwetu sala na yale tunayotenda au kutendewa,
kusema au kuambiwa, n.k. kunaleta mshahibiano na yale tunayowaza kuhusu maisha
ya Yesu kwa kuwa Yesu pia aliishi kama katika maisha yetu kila siku, akitenda
kazi na kushirikiana na wengine, akizungumza na kusikiliza wengine, akiwaza,
akifurahi na kuwa na hisia mbalimbali za kibinadamu. Hii ni kusema juma hili tutakuwa tumezama
hasa katika sala ya tafakari kwa kuwa tutakuwa na Yesu ambaye pia anashughulika
nasi kila siku. Magumu yote ya kawaida
tunayokutana nayo katika maisha yataonyesha maisha ya Yesu kuwa ya kibinadamu
na halisi kwetu, na wala siyo ya dunia nyingine wala simulizi za kutunga
tu. Hii itatusogeza zaidi na zaidi
karibu naye.
Kwa Ajili ya Safari: Kuwa
Karibu Zaidi na Yesu
Tunaanza juma hili kwa
kusikiliza na kutazama matukio katika maisha ya siku za awali ya Yesu. Wachungaji kondoo na mamajusi, maskini na
matajiri, wamefika kumwona yule ambaye amekuja kutusaidia kujiona na kujitambua binafsi. Neno limesemwa katika Mji wa Daudi, na Neno linatayarishwa ili kusikiwa
na wote, Wayahudi na Watu wa Mataifa, karibu na mbali, masikini kwa matajiri.
Yusufu, ambaye alisihiwa na malaika matika
ndoto kumchukua Mariamu awe mke wake, sasa katika ndoto anaambiwa amchukue
Mariamu na mtoto wao waende kwenye nchi ya mbali. Hapa tunashauriwa kutilia maanani imani
aliyokuwa nayo kumwezesha kuzisadiki ndoto hizo na imani aliyokuwa nayo
kuzisichukulia kama ombi au mwaliko na siyo amri au shuruti. Kusafiri, bila kujua kwa uhakika tunakoelekea
na kwa sababu gani hasa kunaelekea kuwa mada
na kiini cha yanayotokea hapa mwanzo katika maisha ya familia
takatifu. Wachungaji kondoo wamerudi
katika shughuli zao wakimtukuza Mungu; wafalme (mamajusi) wamerudi walikotokea
wakitafakari yale waliyoyashuhudia; Mariamu, Yusufu na mzigo wao wa ajabu wanabaki peke yao na kusafiri
kuelekea Misri ambapo wanangojea maelekezo zaidi, ambayo wanaamini watapewa
muda utakapofika.
Tunakaribishwa kutembelea hekalu miaka
kumi na mbili baadaye, katika muda ambao Yusufu, Mariamu na Yesu katika utatu
wao wanasafiri kwenda Yerusalemu. Kinachotokea ni kuwa wanaanza safari ya kurudi nyumbani bila kuwa na
Yesu, na wanashtuka sana na kuogopa kama wazazi wanapogundua hili. Hapa mtakatifu Inyasi anatusihi tusikilize na
kutafakari hisia zao:
Ikawa baada ya siku tatu walimkuta hekaluni akizungumza na walimu wa dini
na sheria: “Na walipomwona walishangaa na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona
umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.
Akawambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwemo katika nyumba ya Baba yangu? Akashuka pamoja nao Nazareti, naye alikuwa
akiwatii, na mamaye aliweka haya yote moyoni (Luka 2:48/49)”
Wanamkuta Yesu, akiwa anaonekana hazijali
hisia zao wazazi wake. Yesu kakamilisha
sheria ya kuwatii wazazi wake na sasa anatekeleza sheria mpya ya kumtii Baba
yake wa mbinguni. Ilimbidi atekeleze utume
wa Baba yake, kazi ambayo inakuwa ya kudumu maisha yake yote: anaishi akisema
na kutenda maneno ya Mungu.
Tunatazama kwa uangalifu kuvurugikiwa kwa
hisia katika mioyo ya Mariamu na Yusufu. Mshangao: “Kwa nini!” anaoutoa Yesu unabadilika
na kuwa swali zuri sana: “Kwa nini?” Mariamu atajiuliza swali hili mara nyingi
katika maisha yake. Tunategemea kwamba
alisali ili kwamba maswali yake yapate majibu au kumezwa na matendo yake ya
imani na matumaini aliyokuwa nayo, kwa mfano pale chini ya msalaba
aliposulibishwa mwanaye. Tukio hili la
kubaki hekaluni linaendelea kidogo baada ya kurudi Nazareti. Kwa miaka kumi na nane ya thamani kuu
inayofuata katika maisha yake, Yesu hakima anatenda jambo muhimu sana: anajifunza
Maandiko Matakatifu ya Mapokeo yake ya Kiyahudi. Je, anamsaidia Yusufu katika karakana yake ya
useremala? Anajifunza na kutenda matendo
ya kibinadamu ya kupenda na kuchukia, ya kusaidia na kutelekeza watu? Hapa tunaalikwa kuwa macho tu tukiangalia na
kutunza mambo moyoni, kama ilivyombidi kukutenda mama yake. Mengi yalikuwa bado mafumbo kwa Mariamu na
Yesu kadhalika. Anajiandaa kwa kuwa
mwaminifu kwa muda, na muda unavyosonga mbele anajifunza kumwamini na
kumtegemea baba yake wa Mbinguni.
Juma hili, tunakubali kushangaa,
kuvurugikiwa na kuulizwa maswali kuwe sehemu tutakaposimama kuyatazama maisha
ya awali ya Yesu Kristu. Tunasali kwa kutumia
hisia zinazoamshwa kwa kuuliza maswali magumu na hata kwa kutilia shaka. Jinsi Yesu anavyokuwa bayana zaidi kwetu,
sisi sura halisi ya nafsi zetu inakuwa bayana katika fumbo la maisha yetu ya
kawaida. Tunaanza kumwacha awe karibu
nasi kila mmoja katika hali yake binafsi, na sote kama jumuiya moja ya
binadamu. Neno limesemwa kwanza katika Mji wa Daudi na sasa kwa ajii ya wote
kila mahali katika dunia ya Mungu.
Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...
Yesu Mpendwa,
Kwa namna fulani nimekuwa nikikuwaza wewe
kama mtu mzima tangu awali yako ya kuwa mtu kama sisi. Sasa naona wazi kuwa ulipitia utoto, ila mara
Injili inakuelezea ukiondoka nyumbani kama mtu mzima. Kulikuwa na nini katika miaka kati ya utoto
wako na utu uzima wako? Kulitokea nini
baada ya wewe kutoka katika banda la ng’ombe ulipozaliwa kule Betlehemu na
wazazi wako kwenda nawe nyumbani?
Ningependa sana kujua zaidi jinsi
ulivyokuwa utotoni. Ulipoanza kutembea,
ulikuwa uliyechekesha watu kwa jinsi ulivyoitumia miguu yako kwa mara ya kwanza
na kupenda kuendelea kujidhatiti kutembea hata ilipoonekana wazi kuwa ulikuwa
umechoka? Sijaona popote palipoandikwa kukuhusu wewe ulipokuwa na umri wa miaka
miwili, ila inanifurahisha ninapokufikiria kama mtoto wa miaka miwili
mchangamfu na mwenye furaha, unayetaka kuchunguza mambo, kutaka kufikia na
kuchukua kila ulichokiona, ukikwea kila ulipoweza hata pale ambapo hukupaswa
kwenda, ukipita kati ya miguu ya Yusufu anapofanya kazi katika karakana yake ya
useremala, ukicheza jikoni Mariamu alipokuwa akipika... Napenda kukuona wewe ukiwa katika namna hiyo,
kwa kuwa hapo utu wako ulio kama wangu unaonekana zaidi; na kuwa ni kwa namna
kama hii sote tulijifunza mengi tulipokuwa tukikua kama watu wenye maswali na
udadisi mwingi kuhusu maisha na watu wengine waliokuwa nasi katika maisha.
Ulijifunza vipi kusoma? Mariamu ndiye aliyeketi nawe na kuanza
kukufundisha Maandiko Matakatifu? Yusufu
ndiye alikuchukua kwenda na wanaume katika sinagogi? Rafiki uliocheza nao
walikuwaje? Ni nini ulichojifunza kuhusu
ulimwengu ulipowatazama wafanyabiashara katika soko, ulipokutana na majirani,
ulipoonana na wateja wa Yusufu, ulipokuwa na ndugu zako?
Bila shaka Yusufu alikuwa na ushawishi
mkubwa sana katika maisha yako, na mara nyingi ulisimama karibu naye alipofanya
biashara na wachuuzi. Alikuwa mtaratibu
na mwaminifu ila mwenye nguvu katika msimamo wake. Mara kadhaa alikwenda sokoni kumsaidia mjane
jirani kwa kuwa wachuuzi daima walijaribu kumlanghai na kumpunja. Ulimtazama Yusufu akizungumza nao,
akisisitizia haki ila kamwe hakuwai kujaribu kupata zaidi ya kile
kilichostahii.
Ninavyoiona nafsi yako ya kuvutia, bila
shaka ulikuwa mmojawapo wa viongozi wa wavulana katika mtaa wako, mkikimbia
huku na kule hapo mjini na kurudi mkicheka na kufanyiana mzaha hadi katika
karakana ya Yusufu. Mara moja ulihadaa
katika mashindano yenu ya kukimbia, na Mariamu alikuona ukifanya hivyo. Alikuita pembeni na kwa taratibu alikusimulia
hadithi ya fumbo yenye kuonyesha ubaya wa kuhadaa, na mara ndani moyoni uliwaka
kwa majuto. Kusahihishwa kwa utaratibu
namna hii ndiko ulikokuhitaji kukusaidia kurudi kwa wenzako ukiwa umesonga
mbele zaidi katika unyofu wa moyo na uwajibikaji kama kiongozi mmojawapo wa
wavulana wenzako.
Ulipokuwa na miaka kumi na miwili, ulikuwa
na safari muhimu na sana kwenda Yerusalemu ukiwa pamoja na kundi kubwa la watu
wa familia yako na marafiki kutoka Nazareti. Ulipofikahapo ulichungulia ndani ya hekalu na kuvutiwa sana na yale
yaliyokuwa yakijadiliwa hapo. Ulitaka
kubaki na kutazama yote, ila marafiki zako walikuvuta, na mara mlianza kukimbia
huku na kule katika mitaa ya Yerusalemu. Najua ulishangazwa na lile soko kubwa sana karibu na hekalu, ambapo pia
bidhaa kutoka nchi mbalimbali ziliuzwa. Uliwaangalia kwa mvuto wa pekee watu wa namna mbalimbali katika jiji
hili—walikuwa tofauti sana na watu kutoka katika mji mdogo ulipoishi.
Lakini kwa ukimya ulijitenga na marafiki
zako, nguvu ya kile ulichokiona hekaluni na Yule aliyekuwa akijadiliwa
ilikuvutia kurudi hekaluni. Lakini, ee
Yesu, haukufikiri chochote kuhusu wazazi wako? Mara nyingine nashangazwa na jinsi ulivyokuwa hekaluni. Cha kwanza, ulikuwa mvulana mdogo wa miaka
kumi na miwili tu—hakudhani ukweli huu ulipaswa uuzingatie? Mariamu na Yusufu waliogopa na kutaabika sana
walipogundua kuwa haukuwa nao katika safari ya kurudi Nazareti. Ila waliliwazwa sana walipokupata. Ninapojaribu kutafakari lililotokea hapo na
baada ya hapo, ee Yesu, nadhani ulipofika nyumbani walikuadhibu kwa kukukataza
kwenda kucheza kwa juma zima.
Lakini ulikuwa mtoto mwema na hali ya
wazazi wako kwako iliyoonyesha kupendelea nidhamu, upendo, imani na haki,
vilisaidia kukulea kuwa ulivyo; vikisaidiana na mafunzo ya Mariamu, na bidii ya
Yusufu katika kazi 1uliyoona na kuitamani kila siku.
Najisikia karibu nawe ninaposali nikikuona
taratibu ukikua kuelekea ukomavu wa mtu mzima. Hata hivyo bado najihisi napenda kukujua zaidi. Ni lini ulipata ufahamu kuwa una mwito wa
pekee kutoka kwa Mungu? Ulianzaje kuwa
mtumishi wa wengine, mwoshaji wa miguu ya watu?
Mpendwa Yesu, nisaidie kukuelewa zaidi ili
niweze kufanana nawe zaidi. Nisaidie
kutafuta namna ambayo naweza kumtumikia Mungu kama ulivyofanya. Natamani kuwa nawe katika ulimwengu huu na kutumikia
kama wewe.
Maandiko Matakatifu
Luka 2:22-38
Luka 2:39-40
Luka 2:41-52
Waebrania 1:1-2