JUMA LA KUMI NA SABA
Namna Mbili za Kuwa na Shauku
Mwongozo: Tunataka Nini?
Tumeanza kutafakari maisha
ya Yesu. Tumeona jinsi, tangu hapo
katika awali utoto wake, maisha yake yalijengeka katika kumtumainia Mungu,
kujisalimisha katika mpango wa Mungu, na kukubali hali ya umaskini na
kukataliwa. Tumekuwa tukisali ili kumjua, kumpenda na kuwa naye kwa undani
zaidi. Kabla hatujaendelea mbele
kutafakari jinsi alivyotekeleza mwito wake mbele za watu, tunatenga majuma
machache kujiweka katika hali ambayo mafungo haya yatakuwa na nguvu ya kuyagusa kwa ndani kabisa maisha yetu na kuyaekeza maamuzi tutakayokuwa
tukifanya tutakapokuwa tunamkaribia zaidi Yesu.
Ni shauku ambayo hutuongoza
katika kuchagua au kuamua. Kuelewa
maamuzi na chaguzi tunazofanya, na kujitayarisha kufanya maamuzi mapya, sharti
tuzielewe shauku zetu na kuwa tayari kuzirekebisha ikibidi.
Juma lote hili, katika muda
unaopata baada ya kumaliza shughuli fulani na kabla hujaanza nyingine, au uwapo
katika kwenda sehemu ya shughuli inayofuata, au ukiwa katika mapumziko mafupi katika
siku ambapo umebanwa sana na shughuli jaribu kuelewa jinsi ya kuwa na shauku au
kiu inayotuweka pamoja na Yesu. Huku
tukijifunza kuikubali njia ya Yesu kwa uhuru, tutajaribu kuelewa nini hasa ni
kinyume cha kuwa na shauku, njia ambayo tunaweza kusema inazinga tamaduni zetu mamboleo.
Ujumbe tunaopata kutoka katika mazingira
ya jumuiya zetu siku hizi, na maadili ambayo yanatawala vyombo vya utangazaji
ni wa kutushawishi kuwa tutakuwa na furaha
zaidi tukiwa na mali zaidi. Mara nyingine
ni shida kuuona wazi ujumbe huu kwa kuwa huweza kujificha sana katika yale
yanayoonekana ya kawaida na ya kiasili; lakini msisitizo na ujumbe wake
haubadiliki, ukitumia mantiki zenye kuvutia akili za wale wanaofikiri sana na
pia vionjo vya wale wanaovutiwa na urembo wa nje. Kwa mfano, matangazo mengi ya bidhaa yana
ujumbe uliojificha kuwa ikiwa kiasi
kidogo ni kizuri, basi kiasi kikubwa
ni kizuri zaidi. Inaonekana kuwa kawaida
kufanya kazi zaidi ili kuwa na mapato zaidi kwa ajili ya kujipatia mali nyingi zaidi. Basi tunakuwa katika
mzunguko wa kutafuta mapato na kuyatumia na hii hutuletea namna fulani
ya mazoea mabaya au ulevi, na kwa
wengine kuwa watumwa wa kazi na
mapato, japokuwa kawaida tunachagua kuishi maisha yanayolingana na kipato
chetu. Tusifikiri kuwa ni mali tu ambayo tunaweza
kujikusanyia. Tunashuhudia tamaa ya kufaulu au kuwa na ustadi mwingi zaidi, kuwa na shahada nyingi za taaluma au kutenda yale ya kuvutia mahusiano na watu mashuhuri—vyote vikiwa viashirio vya mafanikio
yetu. Kisichofichika katika haya yote ni
uhusiano usiokwepeka kati ya mali tunayomiliki na utambulisho wa nafsi zetu. Tunakuwa katika kishawishi kikubwa sana cha kufikiri sisi ni zaidi kwa kuwa tunamiliki zaidi. Tunaanza kuwaweka watu
wenzetu katika ya vipimo hivi vya
mafanikio. Japokuwa hakuna chochote
kibaya kuhusu kuwa na mali au kuwa na mafanikio makubwa au kuwa mashuhuri mbele
za watu, haya yote yanaweza kutuvutia kirahisi sana katika kuwa na majivuno,
kiburi, na kujitenga na Mungu--mali kutuletea
sifa, sifa kutuletea majivuno. Ni
vema kuuelewa vema mfumo huu wa shauku au tamaa, hasa iwapo unaendelea katika
maisha yetu na ya jamii zetu.
Tayari tumeona kuwa mfumo wa Yesu ya kuwa
na shauku ni tofauti kabisa. Namna yake
ya kufanya maamuzi inafanywa na mpangilio wa shauku ambao tayari umetuvutia na
tunataka kuuelewa kwa undani zaidi juma hili. Yesu anatuvutia katika shauku mama ya kumtegemea na kumwamini
Mungu. Tunapoyaweka maisha yetu katika
mikono ya Mungu kama Yesu alivyofanya, tunashuhudia unyonge wa kujisalimisha huko. Pale tunapoona ukweli kuwa yote ni
zawadi, hatuwezi tena kujipima kwa kiwango cha yale tuliyojikusanyia au
kujilimbikizia. Huu umaskini wa roho, na
uhuru unaoendana nao mara nyingi vinaleta burudani ya pekee moyoni. Yesu, hata hivyo, anatutaka tuelewe kuwa hili
ni suala ambalo linapingana na tamaduni zetu—ni mapinduzi ya kitamaduni au
ujenzi wa utamaduni unaopingana na tuliouzoea. Kama mali hutuelekeza kwenye hutuletea sifa, basi umaskini wa aina
yoyote sharti utakuwa ukituletea fedheha au aibu. Sehemu kubwa ya jamii haithamini kumwamini
Mungu pekee. Baada ya shauku ya umaskini
wa roho, kinachofuata ni umaskini halisi au umaskini wa mali, iwapo hili
litakuwa jambo tunalozawadiwa. Tutakavyotamani kutojipatia mali, ni kwa
kadiri hiyo hiyo tutakosa dhamani mbele ya walimwengu. Hivyo basi, shauku ya kumwamini Mungu pekee
hutuongoza katika shauku kubwa ya kutokuthaminiwa, kudharauliwa na kuaibishwa
ambavyo vinatuweka pamoja na Yesu. Yote
haya ni kwa kuwa hatimaye hii ni njia pekee ya kuelekea unyenyekevu na upole
katika utumishi wowote pamoja na Yesu Kristu.
Umaskini wa roho hutupeleka katika kudharauliwa, na kudharauliwa kunatujengea
unyenyekevu. Juma hili tunataka
kuelewa njia hii ya kuwa na shauku.
Misaada inayofuata itatusaidia katika kuingia
katika tafakari hii kwa ndani zaidi. Itatusaidia kuzianza tafakari hizi na
kuzifanya ziwe sala. Picha ya waathirika
wa mabomu ya ardhini inaweza kutusaidia kutafakari kuhusu wale waliowekwe pembeni
kabisa na jumuiya.
Zana za Kukusaidia Kuanza Juma Hili
Kutafakari namna mbili za kuwa na shauku
juma hii ni rahisi sana kuliko inavyoweza kudhaniwa mara ya kwanza. Haihusu kuchagua kujitenga na Mungu na
kuungana na Yesu—tayari tumekwishafanya uchaguzi au uamuzi huo. Tunachoomba juma hili ni neema za kutuwezesha
kutambua namna za kuwa na shauku ambazo zipo hai zikituzunguka. Mapokeo yetu ya Imani ya Kikristu tangu hapo
awali yametuonyesha shauku hizi kama mapambano au vita kwa ajili ya roho
zetu. Juhudi yetu juma hili ni kuelewa
mivutano na misukumo iliyo hai katika vita hivi vya kiroho. Kuna mikakati miwili inayoshindana katika kuvutia mioyo yetu na katika kutuundia tabia ya
kuwa na shauku au kutamani—hivyo hatimaye kuathiri maamuzi au uchaguzi
wetu. Neema za uhuru wa kiroho ambazo
tunapewa zimejengeka katika busara tunayopata kutoka katika utambuzi wa
misukumo hiyo ya ndani.
Tunachopaswa kufanya juma hii ni
kuzitafakari namna hizo mbili. Nikiwa
nafanya lolote au nikiwa mahali popote, naweza kuwa nayarudia makundi haya
mawili ya maneno: Mali-heshima-majivuno;
Umaskini-fedheha-unyenyekevu.
Mwishowe natafuta njia za kuyaweka maneno
haya katika hali yakinifu zaidi ili yaweze kuingiliana na maiya yangu ya kila
siku: Kuwa na vingi zaidi kunanifanya nijidhani ni mtu wa heshima zaidi, na
hii inanifanya niwe na majivuno; kuwa na umaskini wa kiroho au umaskini wa mali
kunanifanya nionekane nisiye na maana na nikikubali hili, najengewa unyenyekevu.
Nia yangu ya kujua nguvu hizi ndani ya maisha
yangu inapewa nguvu na kukua kwa shauku yangu ya kumjua, kumpenda na kumtumikia
Yesu. Inatia matumaini na kusisimua sana
kuona wazi jinsi Yesu, ambaye ananipenda sana na ananivutia niwe naye, ndiye
anayenikomboa kwa kunipa utambuzi huo unaoniongezea shauku ya kutaka kuwa naye katika mfumo wake wa
maisha. Tukiwa waaminifu katika kufanya
tafakari hii wiki nzima, tunaweza kuona wazi jinsi misukumo hii inavyofanya
kazi katika maisha yetu ya kila siku. Tukiwa hapa tutaweza pia kuonjeshwa ladha ya shauku ya kufikia uhuru.
Tamaa yetu ya kuwa na Yesu inavyozidi kuongezeka, tunaweza kujaribu kujiundia
akilini igizo lenye uhalisi katika
maisha yetu: mtu aliyeacha utajiri ili amfuate Yesu—hili litaendana na kubezwa
na marafiki wake, kutokueleweka na ndugu zake, kukanwa na kutelekezwa na
wapendwa wake nk.—kisha nitajiuliza, “je, ni kweli kuwa nataka haya?”
Tunaweza kwanza kumgeukia Mariamu, mama mpendwa wa Yesu, ambaye tulitumia
muda wetu kumtafakari katika majuma yaliyopita. Tunaweza kumwomba amwombe mwanaye kwa niaba yetu, atupe neema hizi. Hapa ni vema kuzitaja neema
tunazohitaji. Tunaweza kusema tunahitaji
kuelewa njia hizi za kuwa na shauku na kupewa umaskini wa roho na hata umaskini
wa mali kama hivyo vitatuwezesha kumtumikia Mungu zaidi na kusaidia kuokoa roho
zetu. Kama inasaidia, sala yetu kwa
Mariamu inawenza kuhitimishwa kwa sala ya Salamu
Maria.
Kisha tunaweza kumgeukia Yesu na kumwomba amwombe Mungu Baba, kwa niaba
yetu, atupe neema hizo. Iwapo tunaona ni
vema sala yetu kwa Yesu imalizikie na sala ya ‘Sala ya Mt. Inyasi: Roho ya Kristu...’.
Mwisho, tunamgeukia Mungu na Baba yetu na kumwomba atupatie hizo neema.
Sala inayofaa kuhitimisha mazungumzo yetu na Baba yaweza kuwa Sala ya Bwana
(sala ya ‘Baba Yetu...’).
Tusisahau kwamba maendeleo yetu kiroho ni zawadi kutoka kwa Mungu, na
vilevile zawadi moja hutufungulia njia kupokea zawadi zingine. Tumeona jinsi neema tunazopokea
zinatutayarisha kupokea neema mpya. Tunachohitaji ni daima kuwa tayari kupokea na kuamini kuwa Yule
aliyetufikisha hadi hapa katika safari hii ya kiroho ataendelea kuwa mhisani wetu
mwaminifu hadi mwisho.
Kwa Ajili ya Safari: Sisi ni Nani?
Yesu anapobatizwa, anachuku nafasi yake au
anaanza utume wake hadharani kama Mwana Mpendwa wa Mungu. Tunatafakari tukio hili la kushangaza na
kujiuliza iwapo tunataka kwenda naye. Anaelekea kule ambapo atajaribiwa na shetani kwa kushawishiwa asitii
Sauti ile aliyoisikia. Anaendelea kuwa
mtii akiitunza hadhi na hatima ya ubatizo wake. Katika maisha yake yote,
atapata ‘miito’ mingine na kupewa ‘hadhi’ nyingi ambazo zitakuwa zikimvutia nje
ya njia yake ya kuwa Mwokozi.
Katika hatua hii katika mafungo yetu,
tunajaribu kuangalia jinsi tunavyoweza kulijibu swali linalowakabili watu wote,
“Nawezaje kujua mimi ni nani?” Utambulisho wetu ni dhaifu, na tunajiuliza mengi kuhusu nafsi zetu; na
pia kutoka pembe mbalimbali tunapata mialiko mingi isiyoshabihiana juu ya jinsi
ya kulijibu swali hili. Kuna Yule Mwovu
na jeshi la wafuasi wake, na kuna Yesu ambaye anatujia kwa amani na utulivu na
kutupa mwaliko wake.
Tunasali juma hili ili kuelewa jinsi
ambavyo mpango wa Yule Mwovu unatuvutia katika kujibu lile swali linalohusu
utambulisho wetu. Kwanza Roho Mwovu
atajaribu kutuvutia kujibu hilo swali kwa kujilimbikizia mali ili kwamba tuweze
kuona na kujiambia, “Ndiyo! Hakika mimi ninatambulika kwa hii miliki kubwa.”
Hivyo sala yetu inahusu jinsi tunavyoweza
kuvutiwa na mali ambayo kwa upekee wake ni nzuri, ila sababu ya kuwa nayo
inaweza kutia doa. Je tunaimiliki mali au inatumiliki sisi? Yule kijana tajiri alijikuta mfungwa wa mali
aliyokuwa nayo, kwa sababu mali yake ndiyo iliyomwambia yeye na watu wengine
yeye ni nani.
Hatua inayofuata ni adui wa asili ya
ubinadamu wetu anajaribu, baada ya kuona bado hakufaulu kutupa jibu kwa swali
letu kwa kutumia mali tunayomiliki, sasa anakuja na pendekezo la kutupa nafasi
muhimu katika jamii ambapo watu wengine watatuambia sisi ni nani. Fahari na mamlaka vinavutia sana, na Yule
Mwovu anamjaribu Yesu na sisi pia kujitambulisha na kujitambua kwa kutumia vyeo
vyetu na hadhi mbele za watu. Kusonga mbele
namna hii ni kuendelea kukua katika kujitegemeza katika mambo yaliyo nje ya
nafsi yetu ili kujijengea hadhi ya nafsi zetu. Mtego wa tatu na wa hatari sana wa Kiongozi wa Uharibufu ni wa kutufanya
tututumke kudai uhuru kutoka kwa Mungu. Hii huanzia na kujiangalia sisi wenyewe kwa majivuno kuwa mipango na
juhudi zetu ndizo zilizotufanya tuwe tulivyo na ndizo zinazotuendeleza katika
maisha. Hatumhitaji Mungu ila mali zaidi
na watu wa kushuhudia uhodari wetu.
Tunageukia kambi ya Yesu, yule ambaye amesikia kutoka kwa Baba yake kuwa
yeye ni nani hasa, na anatukaribisha tusikilize sauti hiyo hiyo ya uthibitisho
katika ubatizo ikituambia kuwa sisi pia ni wapendwa wa Mungu. Tumsikilize yule aliyetujaribu na kuona yote
aliyokuwa anatupa; tunatumia muda kuona jinsi ilivyotuvutia kwa mialiko yake
kutufanya kuamini sisi ni nani na kuwa hatuhitaji chochote kilicho nje yetu
kutuhakikishia sisi ni nani—kumbe hali inayohitajika ni ya uhuru na uwazi wa
kiroho, hali ambayo Yesu anaiita umaskini
wa roho. Tunajua mali ni nini, ipo
kwa ajili gani na imetokea wapi.
Tunasikia kuhusu ‘uhuru kutoka...’ na ‘uhuru kwa ajili...’ vikifafanuliwa
pale Yesu anapotualika tusijali pale ambapo tunapodhalilishwa au hata kufedheheshwa
kwa kuwa majina yetu na utambulisho wetu vinapewa na Muumba wetu. Uhuru kutoka katika mali na fahari za kidunia
vinatusaidia kutembea katika njia huru ya Yesu, ambaye matendo yake na namna ya
maisha tunatafakari juma hili. Alijua
yeye ni nani na anatuambia sisi pia katika siku hizi tujikubali kama wapendwa
wa Mungu ili kwamba kumuiga yeye kuwe namna yetu ya kujitambulisha sisi ni
nani. Hatuishi kama nafsi
zinazojitegemea tu, bali Kristu anaishi ndani yetu akifanya kazi kupitia nafsi
zetu vile vile.
Juma hili tukutana uso kwa uso na namna ambazo tunavutiwa na hila na bidii
za Mkuu wa Majaribu. Tunakuta pia mioyo
na akili zetu zikivutiwa kwenye njia na busara ya Yesu.
Katika Maneno Haya au Mengine Yanayofanana Nayo...
Mama Mariamu Mpendwa,
Nimetumia muda mwingi nikizungumza nawe
tangu utoto wangu. Sasa, ninapofanya
mafungo haya, nahitaji kuwa karibu zaidi na mwanao, na najikuta nikitaka kufahamu
wewe zaidi. Katika majuma yaliyopita
nilipokuwa nikisali, nimekuwa nikijiundia picha ya maisha yako na ulivyoyaishi
pamoja na Yusufu na Yesu. Naona jinsi
ulivyomfundisha Yesu, na ninapokuona katika kazi nyingi kama mama, mzazi, mlezi,
na mwanandoa, najikuta naweza kuhusiana nawe zaidi.
Nahitaji ndani moyoni mwangu kupokea neema
ya ujasiri wa kuishi maisha yangu jinsi Yesu alivyoishi. Tafadhali mwombe Yesu anipokee katika
harakati za kumtumikia. Naona namna
nyingi ambazo nimejing’ang’aniza kwenye majivuno, kiburi na kumkana Mungu—hii
ni njia yangu ya kujaribu kuwa Mungu. Tafadhali mwendee mwanao Yesu na kumsihi
anisaidie kujikubali kama mdhaifu ili kwamba hii iwe chanzo cha neema katika
maisha yangu. Mahangaiko yangu ya kuwa
mkamilifu hayatanifikisha karibu na Mungu, ila harakati zangu za kupokea
mapungufu yangu yanaweza kunisaidia.
“Salam Maria, Umejaa neema...
Ee Yesu,
Nakugeukia kwa unyenyekevu. Ninavutiwa sana na jinsi ulivyoishi duniani,
ila inaonekana haiwezekani kwangu kuishi namna hiyo! Nimebanwa katika kitendawili cha mahangaiko
ya kidunia: kupata heshima na tunzo hapa na pale inaonekana vema ila haikidhi
kiu yagu. Najikuta natafuta kutukuka
zaidi, kutambuliwa zaidi na watu wengi zaidi, sehemu nyingi zaidi. Nimeyabadili maisha yangu ili yalingane na
maoni ya walimwengu, na taratitu nimejikuta nazama katika upande tofauti wa
maisha niliyotaka kuyaishi.
Hapo mwanzo nilijiuliza: namwumiza nani
kama nikipata heshima kidogo kutoka kwa walimwengu? Nilijiambia “tazama ni kushangiliwa kidogo na
watu, watu kuniambia jinsi gani nilivyo hodari na mwerevu.” Lakini sasa nimesoma mwongozo wa mafungo wa
juma hili na najua kipi si sawa—jinsi gani ulimwengu ulikuwa mwerevu katika
kunihadaa kubadili mtazamo wangu wa maisha. Mara nilijikuta mimi mwenyewe ndiye heshima na tunzo za kila
namna—kutukuzwa na walimwengu ndiko kunakoniambia mimi ni nani! Je, kama hivi vikiondolewa kwangu au kufikia
kikomo, mimi nitakuwa nani? Nimepoteza
nafsi yangu katika mbio hizi za kutafuta umaarufu na kutukuzwa, na sasa sina
msimamo maishani. Siyo kwamba kazi yangu
ni mbaya au kwamba sifa zinadhuru; ila ni kwamba nimepoteza mtazamo wangu. Mpendwa Yesu, mwombe Mungu Baba anisaidie
kukataa yale ya hapa duniani ambayo yananizuia nisiwe na unyenyekevu na
umaskini katika maisha kama uliokuwanao.
“Roho ya Kristu...
Mungu Mpendwa, Baba Yangu Muumba,
Umemtuma mwanao duniani kuwa mmoja wetu, kwa ajili yetu. Nisaidie kuangalia jinsi alivyoishi na
kuyafanya maisha yangu yafanane na yake. Najua kwamba kwa sababu ya maringo na ubinafsi wangu napenda nifanye
haya mimi mwenyewe, lakini sasa, ingalao kwa leo katika muda huu natambua kuwa
siwezi. Tafadhali, Ee Baba Yangu, nipe
neema ya kumuiga Yesu katika yote, hata katika yale ambavyo yananitisha. Siangalii tu katika sehemu za maisha zisizo
za kawaida kama kuteswa na kusulibishwa, bali jinsi alivyoyapa kipaumbele
mahitaji ya wengine, na si yake binafsi. Baba mpendwa, nataka kuishi namna hiyo ila mara kwa mara najikuta niko
mbali sana na njia hiyo ya maisha.
Kuwa nami katika harakati zangu za
maisha. Nipe nafasi niwe natafuta kibali
chako tu cha jinsi ya kuyaishi maisha yangu. Nijalie niweze kutambua njia za yule mwovu za kunihadaa na kunivuta
kutoka katika kumfuasa mwanao, na kunifanya mtumwa wa malimwengu.
“Baba Yetu uliye mbinguni....
Maandiko Matakatifu:
Matayo 5:1-16
Wagalatia 5:16-26
Wafilipi 4:11-15
1 Timoteo 6:6-10,
17-19
1 Petro 5:1-11